32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Lema atajwa kung’olewa RC Arusha

Godbles Lema
Godbles Lema

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbles Lema (Chadema), ametajwa kuwa ni kati ya watu waliosababisha kuondolewa kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda.

Taarifa za uhakika zilizolifikia MTANZANIA zilieleza kuwa, hatua ya Ntibenda kushindwa kumdhibiti Lema na harakati zake ndani ya Halmashauri ya Jiji la Arusha inayoongozwa na Chadema, imehusishwa na kung’olewa kwake.

Ntibenda anakuwa ni mkuu wa mkoa wa tatu kung’olewa na Rais Dk. John Magufuli huku akitanguliwa na aliyekuwa  Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela, ambaye alitumikia wadhifa huo kwa siku 22 pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Magesa Mulongo, ambaye anaye uteuzi wake ulitenguliwa Juni 26, mwaka huu.

Ntibenda ambaye aliteuliwa na Rais Magufuli, Machi 13, mwaka huu hadi kufikia jana alikuwa ametumikia wadhifa huo kwa siku 159.

Taarifa ya kutenguliwa kwake ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kupitia taarifa yake iliyotolewa kwa vyombo vya habari, ambapo alisema Rais Magufuli,  amefanya mabadiliko madogo ya uongozi na kumteua aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mrisho Gambo, kuwa Mkuu mpya wa Mkoa wa Arusha kuanzia jana.

Majaliwa alisema Gambo anachukua nafasi  hiyo baada ya Felix Ntibenda uteuzi wake kutenguliwa.

“Ntibenda anahamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu ambako atapangiwa majukumu mengine. Kabla ya uteuzi huo, Gambo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha,” ilieleza taarifa hiyo ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mkuu huyo mpya wa mkoa ataapishwa leo saa tatu asubuhi Ikulu jijini Dar es Salaam.

Kauli ya Lema

MTANZANIA ilimtafuta Mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema (Chadema), ambaye alisema alimweleza Ntibenda juu ya kutafutwa kwake, jambo lililothibitika kuondolea kwake.

Alisema tangu alipowasili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mrisho Gambo kumekuwa na kutoelewana huku kiongozi huyo akitajwa na kuandika barua zenye taarifa ambazo si sahihi hasa kwa Jiji la Arusha.

“Wiki moja iliyopita nilimwambia aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda, kwamba anatafutwa yeye na leo (jana)  imethibitika baada ya Rais Magufuli kutengua uteuzi wake.

“Tunaujua mkakati huu wa kuendelea kudhoofisha demokrasia na haki katika taifa. Arusha tumejipanga na mimi  (Lema) nimejipanga kukabiliana na matendo yoyote ya ukandamizaji na uonevu utakaoletwa na mkuu huyu wa mkoa (Gambo) kwa gharama ya maisha yangu.

“… sasa tutavaa kombati na atairudisha Arusha kama ilivyokuwa, nami nitakuwa imara zaidi maana yeye haamini katika demokrasi ila anamini katika ubabe na kuchongea wenzake kwa hili nitapambana naye kwa nguvu zangu zote,” alisema Lema.

Lema alimtuhumu Gambo kutoheshimu mipaka yake ya kiutawala kwa kuingilia maamuzi ambayo yamejadiliwa kwenye vikao halali vya halmashauri lakini alishangazwa na hatua ya Rais Magufuli, kusikiliza taarifa hizo bila kuifanyia kazi kwa kina.

“Kwa mfano, Baraza la Madiwani lililopita ndilo lililopitisha kiwango cha posho kwa madiwani kutoka Sh100,000 hadi Sh120,000, jambo la kushangaza DC ameandika barua Tamisemi na nakala kwa Takukuru ili wachunguze jambo ambalo limeshapata baraka za Tamisemi haya yalifanyika mwaka 2008 wakati huo Chadema haina diwani hata mmoja,” alisema Lema ambaye kwa wiki kadhaa amekuwa na misuguano ya kiutendaji na Gambo.

Ntibenda avunja ukimya

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa aliyetenguliwa, Felix Ntibenda amevunja ukimya na kusema kuwa tuhuma zinazolengwa kwake na Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wa Mkoa wa Arusha, Philemon Mollel, hazina ukweli wowote.

Alisema kuwa tuhuma za kunyang’anywa Kiwanda cha Usagishaji cha NMC hahusiki nazo na wenye mali ni Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko.

Mbali na tuhuma hizo Ntibenda alidai kuwa mfanyabiashara huyo alitumia UVCCM kudai kuwa anahusika na uchomaji wa moto katika Shule za Sekondari katika matukio yaliyotokea hivi karibuni.

Alisema UVCCM waliamuru mkuu huyo ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kutoa taarifa kwa umoja huo.

Kauli hiyo aliitoa juzi muda mfupi kabla ya kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa bweni la Shule ya Sekondari ya Korona iliyoko nje kidogo ya Jiji la Arusha.

Alidai kuwa anasikitishwa na kitendo cha Mollel kushirikiana na UVCCM ambao wamekuwa wakieneza propaganda kupitia mitandao ya kijamii kwamba alihusika katika njama za kumnyang’anya kinu hicho.

“Mimi sifanyi  kazi kwa amri za chama wala jumuiya bali nafanya kazi na kutoa taarifa kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa au kwa Rais Dk. John Magufuli na si mtu mwingine wala taasisi nyingine yoyote.

“… nakerwa na tabia ya chama kuingilia shughuli za Serikali kwani maamuzi ya kunyang’anya wawekezaji vinu yalifanywa na Baraza la Mawaziri ambalo lilitaka mali zote zirudi serikalini,” alisema Ntibenda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles