31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

ATCL, UDA, Bandari kutikisa Bunge lijalo

 Profesa Assad
Profesa Assad

Na ARODIA PETER -DAR ES SALAAM

RIPOTI ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) itawasilishwa na hatimaye kujadiliwa katika Mkutano wa nne wa Bunge la 11 unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi Ndogo ya Bunge  Dar es Salaam jana ilisema mkutano wa Bunge uliopangwa kuanza Septemba 6 mwaka huu utatanguliwa na vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge Agosti 22 mwaka huu.

Taarifa hiyo ilisema Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) zitachambua taarifa ya  CAG ya mwaka 2014/ 2015.

Kamati hizo mbili zinazoshughulikia mambo ya fedha za umma baada ya kukamilisha uchambuzi wa ripoti ya CAG itaipeleka bungeni kwa ajili ya kujadiliwa na wabunge.

Taarifa hiyo ya mwaka wa fedha 2014/15 iliyotolewa Dodoma na CAG,  Profesa Mussa Assad, Aprili mwaka huu, pamoja na mambo mengine, mashirika ya umma, Serikali kuu  na halmashauri mbalimbali yalionekana kuwa na ufisadi uliokithiri.

Mashirika ya umma ambayo yanatarajiwa kuongoza mjadala katika Bunge hilo ni pamoja na Kampuni ya simu ya ATCL, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) na Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC).

Ripoti ya CAG aliyoikabidhi kwa Wenyeviti wa Kamati hizo mbili, ilizimulika kwa kuzikagua taasisi za Serikali Kuu 199, Mamlaka ya Serikali za Mitaa 164 na Mashirika ya Umma 102 kati ya mashirika 186.

Shirika la Ndege Tanzania (ATCL)

Ripoti hiyo ya Profesa Assad alisema katika ukaguzi wake,   amebaini shirika hilo halina ndege za kutosha, gharama za uendeshaji zisizohimilika, uhaba wa mtaji wa kujiendesha   na udhaifu wa menejimenti.

Shirika hilo pia lina upungufu wa wafanyakazi katika sekta muhimu na wafanyakazi katika eneo la uendeshaji (operational staff) wanaozidi mahitaji huku shirika  likiendelea kutumia Cheti cha Uendeshaji kilichokwisha muda wake tangu Machi 30, mwaka 2010.

Mamlaka ya Bandari (TPA)

Alisema katika ripoti zake kila wakati amekuwa akiishauri Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kutumia mita za kupimia mafuta yanayoingizwa nchini  kupitia bandari ambako hadi anakamilisha ukaguzi wa mwaka 2014/15, Mamlaka hiyo ilikuwa haitumii mita hizo.

Kasoro za mkataba kati ya TPA, TICTS

Alisema ukaguzi umebaini kasoro kadhaa katika mkataba baina ya TICTS na Mamlaka ya Bandari ambako ni pamoja na umiliki wa asilimia 51 ya hisa wa Kampuni ya TICTS uliohamishwa kwenda kwa Kampuni ya Hutchison International Port Holding Desemba 30, 2005, kinyume na matakwa ya mkataba.

Alisema kulingana na mkataba, endapo kiwango cha ufanyaji kazi kwa mwaka kitashuka chini ya asilimia 25, mkataba unaweza kutenguliwa. Pamoja na upungufu huo kugunduliwa, mkataba huu haukuvunjwa bali ulihamishiwa kwa Kampuni ya Hutchison International Port Holding.

“Hata hivyo kwa miaka mitano mfululizo tangu kuingiwa  mkataba huo mwaka 2000, TPA haikufanya tathmini ya ufanisi kinyume na makubaliano ya mkataba.

“Hata hivyo nimebaini Mamlaka ya Bandari Tanzania haina uwezo wa kufahamu na kusimamia taarifa za makontena yanayopokelewa na TICTS kwa kuwa   haina haki ya kuingia katika mfumo wa kompyuta wa TANCIS ambao unatumiwa na TICTS.

Utata wa meli 85 kupotea

Profesa Assad alisema  ukaguzi uliofanyika kwa mwaka 2014/15 umebaini kati ya meli 1,253 zilizotia nanga meli 145 hazikuonekana katika mfumo wa mapato wa Mamlaka hiyo.

Alisema menejimenti ilifanikiwa kupata nyaraka zinazohusu meli 60 tu kati ya meli 145 huku ikishindwa kutolea ufafanuzi wa kutoonekana kwa meli 85 zilizosalia.

TTCL

Alisema Kampuni ya Simu Tanzania imekuwa ikipata hasara kubwa kwa muda mrefu na kufikia mwisho wa mwaka 2014, kampuni ilikuwa imepata hasara ya   Sh bilioni 361  ambako mwaka 2013 ilikuwa  Sh bilioni 334.

Hali hiyo inatokana na mtandao wake wa mawasiliano ya simu za mkononi kutopatikana maeneo mengi; kutokuwa na teknolojia za kisasa, kutokuwa na njia za usambazaji zenye ufanisi na kukosa fedha za kukuza biashara ikilinganishwa na makampuni mengine ya simu, alisema.

Mauzo ya UDA

Alisema   Bodi ya Wakurugenzi ya UDA iliuza hisa za shirika bila kupata kibali cha Serikali.

Hisa za   UDA zilithaminishwa kwa bei ya Sh 744.79 kwa kila hisa mwezi Oktoba, 2009, na  Novemba, 2010 thamani ya kila hisa ikawa 656.15.

Hata hivyo,  alisema katika uuzaji huo, Bodi ya Wakurugenzi ya UDA ilitoa punguzo la asilimia 60 kwa kila hisa kwa mwekezaji huyo (kwa tathmini ya bei ya hisa ya   Oktoba, 2009), bila kuwapo sababu za kufanya hivyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles