RAIS Daniel Ortega wa Nicaragua amemteua mkewe, Rosario Murillo kuwa mgombea mwenza wa urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Novemba mwaka huu.
Ortega (70), mwenye siasa za mrengo wa kushoto anapewa nafasi kubwa ya kushinda kwenye uchaguzi huo.
Alimtaja mkewe kama mgombea mwenza na makamu wa rais wakati ambao anawania kuchaguliwa kwa mara ya tatu.
“’Ni serikali ya umoja na Rosario Murillo ambayo ni kama ishara ya usawa wa jinsia,” alisema Rais Ortega.
Murillo tayari ni msemaji wa serikali na anaonekana kuwa anagawana mamlaka na mumewe.
Ortega aliwahi kutawala nchi hiyo miaka ya 1980 na baadaye akarudi katika madaraka mwaka wa 2007 kupitia chama chenye mrengo wa kushoto cha Sandinista National Liberation Front (FSLN).
Wachambuzi wa masuala ya siasa wanawashutumu wanandoa hao kwa kuiendesha Nicaragua kama chombo chao cha binafsi.