POMBE: Adui namba moja wa ndoa, afya anayeongeza watoto wa mitaani – 2  

beer-224651Na Hamisa Maganga

MAKALA hii inalenga kuangalia athari za pombe kwa jamii, jinsi inavyochochea masuala ya ukatili kwa wanawake na watoto.

Mwandishi wa makala haya alipata fursa ya kuzungumza na baadhi ya wanandoa wanaovumilia vituko vya waume zao walevi, watoto wanaoteseka kwa sababu ya ulevi wa wazazi wao na wale waliovunja ndoa zao.

Mume akilewa ni ngumi na vituko mtaani

 Mama mmoja ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini, mkazi wa Mbagala Zakiem, anasimulia jinsi ambavyo mume wake akilewa anageuka kuwa kituko mtaani.

Anasema kuwa mume wake kila ifikapo mwisho wa wiki ni lazima arudi nyumbani alfajiri.

Anasema kuanzia siku ya Ijumaa hadi Jumapili, yeye ndio hugeuka kuwa ‘alarm’ ya kuamsha watu alfajiri.

“Mume wangu anafanya kazi na ni mtu mkubwa tu kazini, lakini vituko anavyovifanya hapa mtaani ni vya aibu na nikimwambia naambulia kipigo.

“Siku zote akilewa ni lazima ajikojolee na kutukana watu ovyo mtaani… majirani huwa wananifuata nyumbani na kunieleza jinsi mume wangu anavyojidhalilisha huko nje.

“Nikimfuata ili nimrudishe nyumbani nami naambulia matusi na kipigo juu,” anasema mama huyo na kuongeza kuwa;

“Siku moja alirudi akiwa amelewa, ilikuwa ni mida ya saa 11 alfajiri, alipofika karibu na nyumbani akaanza kutukana matusi ya nguoni, anaimba nyimbo zisizoeleweka.

“Kuna jirani yangu mmoja yeye ni nesi, alikuwa akielekea kazini, akaja kuniamsha nikashuhudie vituko vya mume wangu, nilipotoka nilimkuta amekaa mtaroni, akiwa amelewa huku akiimba nyimbo zisizoeleweka na kutukana wapita njia.”

Anasmea alimfuata na kumsihi waende nyumbani lakini alikataa na kuanza kumpiga hadi akapoteza fahamu.

Anabainisha kuwa wapita njia ndio waliomsaidia hadi kumfikisha hospitalini na kupatiwa matibabu.

Anasema baada ya yeye kufikishwa hospitali, huko nyuma watu walimpiga mumewe kwa kuwa walishachoshwa na vituko vyake.

“Pamoja na kipigo kile bado hajakoma, anaendelea na ulevi… familia pia haijali kama anavyojali pombe.

“Nimechoka kuishi naye lakini sijui wapi pa kukimbilia, sina kazi wala ndugu wa kumtegemea kunilisha na kunisomeshea watoto.

“Hivyo, navumilia mateso haya na sijui yatakwisha lini, najaribu tu kuomba Mungu siku moja ambadilishe mume wangu maana pombe imemteka,” anasema.

 

Hali ilivyo Kiteto

 Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, unywaji pombe umekithiri hadi kusababisha watu kuuawa na wengine kushindwa kusomesha watoto wao.

Akizungumzia suala hilo, Kiongozi wa mila za Kimasai, (Laigwanani), Mbambire Oleikurukuru, anasema hakuna sherehe inayoweza kufanywa na Wamasai bila kuwapo pombe.
“Wamasai huwa wanakunywa pombe hadi wanakata moto (kuzimia), ikitokea hivyo humwagiwa maji ili waamke na kuondoka katika eneo husika,” anasema kiongozi huyo.

Anasema kuwa wakazi wengi wa eneo hilo huuza mifugo yao kwa sababu ya kupata fedha ya kununulia pombe.

“Wakishapata fedha basi hata familia wanaisahau, wanawaacha watoto wakitaabika huku wakiwanyima haki yao ya msingi ya kupata elimu.

Oleikurukuru anasema ili kukabiliana na hali hiyo, wameamua kuweka utaratibu wa kuwa na vikao vya kukumbushana kuacha ulevi uliokithiri.

Anasema katika vikao hivyo wamekubaliana kila mmoja wao amdhibiti mwenzie na kuhakikisha wanajali familia zao.

Nassinyari Lenyirai, ni mama wa familia kutoka jamii ya
wafugaji, anasema moja ya matatizo makubwa yanayoisumbua jamii hiyo ni
ulevi ambao huchangia kuvunja ndoa na watoto kukimbia mji.
Anasema wanawake wengi wa jamii ya wafugaji Kiteto, wamekumbwa na
tatizo hilo hadi kufikia hatua wanaharakati kuingilia kati.

Wanaume wengi wakishalewa hawajishughulishi kujua mwanawe amekula nini, anaumwa au kama anakwenda shule.

 

KINNAPA wajitosa kuwasaidia

Shirika lisilo la kiserikali la KINNAPA, linalojihusisha na masuala mbalimbali ya kijamii na kielimu, limejitosa kuhakikisha jamii hiyo inaachana na ulevi uliokithiri.

Mratibu wa Kitengo cha Jinsia katika shirika hilo, Paulina Ngurumo, anasema wanahakikisha jamii inaondokana na ukatili ambao chanzo chake ni ulevi uliokithiri.
Anasema wanawake wengi si wa Kiteto tu, hata katika maeneo mengine wameachika na kuamua kwenda kuishi kwa ndugu zao au kuanza maisha mapya ya kujitegemea kutokana na kufanyiwa ukatili
unaotokana na vitendo vya ulevi.
Afia baa kwa ulevi

Mwanamume mmoja maarufu kwa jina la Maziwa, mkazi wa mjini Kibaya, wilayani Kiteto, wiki iliyopita alifariki dunia akiwa  baa.

Inasemekana kuwa Maziwa  alianguka ghafla na kupoteza maisha baada ya kuzidiwa na pombe.
Mashuhuda wa tukio hilo wanasema kuwa marehemu alifika baa
ijulikanayo kwa jina la Safari, asubuhi ya saa moja akiwa tayari amelewa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Francis Massawe, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

 

Watoto walivyokimbia familia

Ongezeko la watoto wa mitaani hapa nchini ni matokeo ya ukatili wa wazazi au walezi, kufiwa na wazazi, ukorofi wa watoto wenyewe, mkumbo rika, umasikini miongoni mwa jamii, kuvunjika kwa ndoa, mimba zisizotarajiwa na ulevi wa kupindukia.

Mmoja wa watoto niliozungumza nao, ambaye anaishi mitaani, James Emmanuel (15), anasema yeye na mdogo wake Masija Emmanuel (13), (si majina yao halisi), walilazimika kukimbia nyumbani kwao baada ya mama yao kushinda kilabuni na kuwatelekeza.

“Mama alikuwa na tabia ya kushinda tu vilabuni, hatujali wa kututhamini… akiondoka asubuhi nyumbani yeye na baba wanarudi tukiwa tumelala na hawajali kama tumekula au la.

“Wakati mwingine walikuwa hawarudi kabisa nyumbani, hivyo maisha hayo yalitushinda na kuamua kuja hapa Dar es Salaam kujitafutia kipato kwa kuosha vioo vya magari,” anasema James ambaye analala katika Kituo cha mabasi ya Mikoani Ubungo, akitokea mkoani Musoma.

Anasema walikuwa hawana chakula, majirani walikuwa wakiwapa chakula hadi wakachoka ndipo walipoamua kuja Dar es Salaam na kuishi mitaani.

James anasema wakati mwingine huwa wanafukuzwa na wenzao hapo Ubungo na kwenda kulala katika vibanda vya kuuzia chakula.

Naye Anna Machumu (16), ambaye pia alitoroka kwao baada ya shangazi yake kuwa na desturi ya kulewa na kumpiga, anasema ukatili aliokuwa akifanyiwa ulimlazimu kukimbia nyumbani.

“Baba na mama walipofariki, alinichukua shangazi yangu kwa lengo la kunilea kwani nilikuwa nimezaliwa peke yangu sina kaka wala dada, lakini alinitesa na kunigeuza mfanyakazi wake wa ndani,” anasema.

Anna anasema amesoma hadi darasa la sita na kwamba ndoto zake za kuwa daktari zilikufa mara baada ya wazazi wake kufariki.

Anasema tangu shangazi yake amchukue hakuwahi kwenda shule tena na kazi yake ilikuwa ni kukaa nyumbani na kufanya kazi zote zilizopo.

“Alikuwa akirudi nyumbani kutoka kwenye vilabu vya pombe na kunikuta nimelala hata kama nimemaliza kazi zangu, atanipiga kama mbwa na kunitukana mimi na wazazi wangu ambao ni marehemu,” anasema mtoto huyo.

Anasema kuwa maisha ya mtaani ni magumu lakini hana jinsi anayavumilia kwa kuwa hana ndugu huku mjini wa kumkimbilia.

Akisimulia mikasa aliyowahi kukumbana nayo nyakati za usiku, anasema ameshawahi kubakwa mara moja na walevi usiku na kunusurika mara tatu.

“Unaona hizi alama (anaonyesha mikwaruzo mwilini mwake), kuna siku nilibakwa na kijana mmoja ambaye alikuwa amelewa.

“Nilijitahidi kupambana naye lakini nilishindwa. Pia nimeshanusurika kubakwa na vijana usiku kama mara tatu hivi, maana tangu nibakwe nikajifunza jinsi ya kukabiliana nao.

“Mmoja alikuja usiku, nilikuwa nimelala katika kibaraza cha dukani kule Kariakoo… nilisikia mtu akitaka kunivua nguo nilichofanya ni kumpiga kwa goti kwenye uume wake nikamuacha anaugulia mimi nikakimbia,” anasema.

Itaendelea wiki ijayo…

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here