RAIS Francois Hollande wa Ufaransa amesema ushindi wa mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Republican, Donald Trump katika uchaguzi ujao, unaweza kurejesha siasa za zamani duniani kote na anawafanya watu ‘kujisikia kichefuchefu’.
Ushindi wa Trump Novemba mwaka huu unaweza pia kuathiri uchaguzi wa urais Ufaransa utakaofanyakia 2017, alisema Hollande.
“Kama Wamarekani watamchagua Trump, watakuwa na wakati mngumu kwa sababu uchaguzi wa Marekani ni uchaguzi wa dunia,” alisema alipozungumza na waandishi.
Taarifa ya Shirika la Habari la Uingereza, Reuters, inasema kiongozi huyo wa Ufaransa ametoa kauli hiyo baada matamshi ya Trump kuhusu wazazi wa mwanajeshi Mmarekani muislamu aliyeuawa vitani nchini Irak.
Rais Barack Obama wa Marekani pia amemshambulia Trump hana sifa zinazostahili za kuwa rais wa Marekani.
Naye Trump alijibu mashambulio kwa kumshutumu Obama kama kiongozi aliyeshindwa na kwamba mgombea urais wa Democrat, Hillary Clinton, naye hafai kuwania nafasi hiyo au hata ofisi yoyote ya serikali.
Katika siku za karibuni, Tramp amekuwa akishambulia kila kona wakiwamo wanachama wa chama chake cha Republican kama Richard Hanna mwanachama mkongwe kutoka New York ambaye alisema mgombea urais huyo ni aibu kwa taifa.
Wanachama wengine wa Republican wamejitenga kumshabikia Trump au hata kutomuunga mkono.