24.8 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

Wanafunzi UDOM warejeshwa

Profesa Ndalichako
Profesa Ndalichako

Na JONAS MUSHI, DAR ES SALAAM

SERIKALI imewaondoa rasmi wanafunzi 1,500 huku ikiwahamishia katika vyuo vingine vya ualimu wanafunzi 5,913 kati ya 7,805 waliokuwa wanasomea stashahada maalumu ya ualimu wa shule za msingi na sekondari kwa masomo ya sayansi na hisabati katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Idadi hiyo ya wanafunzi waliotemwa inajumuisha wanafunzi 290 ambao hawakuwa na sifa za kujiunga na stashahada hiyo maalumu na wote waliokuwa wanachukua stashahada ya ualimu wa elimu ya msingi ambao idadi yao ni 1,210.

Kutokana na hali hiyo, kuanzia sasa Serikali haitaendelea na mpango huo na badala yake itatumia utaratibu wa kawaida wa kuwapata walimu wa masomo hayo.

Akizungumzia uamuzi huo Dar es Salaam jana, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, alisema wanafunzi wote wa stashahada ya ualimu wa elimu ya msingi wameachwa kwa sababu masomo hayo hayakuwa katika mpango wa Serikali, na kwamba stashahada maalumu ilikuwa kwa walimu wa sekondari peke yake.

“Serikali imefanya uchambuzi wa wanafunzi waliokuwa wanasoma UDOM na tumegundua wapo makundi mawili.

“Kundi la kwanza ni la wale wa stashahada maalumu ya ualimu wa sayansi na hisabati na kundi la pili ni la wale wa stashahada ya ualimu wa elimu ya msingi,” alisema Profesa Ndalichako.

Kuhusu hatma ya wanafunzi wa stashahada ya ualimu wa elimu ya msingi, alisema kuwa walichomekwa tu kwa sababu mpango wa Serikali ulikuwa ni kwa walimu wa sekondari.

Hata hivyo, alisema walichambua sifa za wanafunzi hao na kugundua kuwa wanafunzi 29 wa mwaka wa kwanza na wa pili walijiunga na masomo hayo kwa sifa za cheti cha ualimu daraja la tatu A na wengine 1,181 walijiunga kwa sifa za kidato cha nne wakiwa na daraja la pili hadi la nne.

“Kwahiyo, wale wanafunzi 29 waliojiunga kwa sifa ya cheti cha ualimu, watahamishiwa katika Chuo cha Ualimu Kasulu wamalizie masomo yao kwa gharama zao wenyewe,” alisema.

Kwa upande wa kundi la stashahada maalumu ya ualimu wa sayansi na hisabati, alisema walichambua sifa za wanafunzi ndipo wakabaini kuwa 290 kati ya 6,595 waliojiunga na masomo hayo hawakuwa na sifa.

“Sifa za kujiunga na masomo haya zilikuwa mbili. Sifa ya kwanza ilikuwa ni mwanafunzi awe na ufaulu wa daraja la kwanza hadi la tatu na sifa ya pili ni kuwa na ufaulu wa masomo mawili atakayokwenda kufundisha kwa alama A, B au C.

“Wale wanafunzi 21 kati ya 290 ambao hawakuwa na sifa, walikuwa na ufaulu wa daraja la nne badala ya daraja la kwanza hadi la tatu na wengine 269 walikuwa na ufaulu wa kati ya daraja la kwanza hadi la tatu, lakini hawakuwa na ufaulu wa kiwango cha alama A hadi C kwa masomo mawili ya sayansi.

“Kutokana na hali hiyo, wanafunzi hao hawatarudishwa katika vyuo vya Serikali na badala yake tunawashauri waombe mafunzo yanayolingana na sifa walizonazo kwenye chuo chochote wanachotaka,” alisema.

Alisema pia kwamba uchambuzi umebaini kuwa wanafunzi wenye ufaulu wa daraja la kwanza na la pili ambao pia wamefaulu masomo mawili kwa alama A hadi C ni 382  na hao ndio watakaorudishwa UDOM.

Kwa mujibu wa Profesa Ndalichako, wanafunzi wengine wenye vigezo vya ufaulu watahamishiwa katika vyuo vya ualimu vya Serikali.

“Wanafunzi 4,586 wa mwaka wa kwanza waliokidhi vigezo vya ufaulu watahamishiwa katika vyuo vya ualimu vya Morogoro, Butimba, Mpwapwa, Songea na Tukuyu.

“Wanafunzi 1,337 wa mwaka wa pili watahamishiwa kwenye vyuo vya ualimu vya Korogwe na Kasulu ili wamalize masomo yao,” alisema.

Alisema pia kwamba Serikali itaendelea kuwapatia mikopo wanafunzi watakaorudishwa UDOM na waliohamishiwa kwenye vyuo vya Serikali vya ualimu, na pia watapewa mkopo wa Sh 600,000 ambazo ni ada ya mafunzo ya ualimu itakayolipwa moja kwa moja chuoni.

“Kwa hiyo, wanafunzi wote waliorejeshwa UDOM wataanza masomo Oktoba mwaka huu, na wale waliohamishiwa vyuo vya ualimu wataendelea na mafunzo yao Septemba mwaka huu.

“Kwa maana hiyo, wanafunzi wote watatakiwa kufika na vyeti vyao halisi vya kidato cha nne vitakavyokaguliwa kabla hawajapokewa rasmi kwenye vyuo walivyopangwa,” alisisitiza.

Kuhusu fedha za wanafunzi wa vyuo wanazoidai Serikali kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo, Profesa Ndalichako alisema wanaendelea na uhakiki wa majina ya wanaostahili kupata fedha hizo ili kuepuka kulipa wanafunzi hewa.

Mei 28 mwaka huu, Serikali iliwarejesha nyumbani wanafunzi 7,805 waliokuwa wanasoma stashahada maalumu ya ualimu wa sayansi na hisabati katika chuo cha UDOM kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutokana na mgomo wa walimu uliokuwa umedumu kwa wiki tatu na uwepo wa wanafunzi wasio na sifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles