JONAS MUSHI NA CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM
RAIS mstaafu wa Kenya, Mwai Kibaki, ameibukia katika kongamano la Wiki ya Maji Afrika na kusema upatikanaji wa maji safi na salama bado ni changamoto kubwa barani Afrika.
Kutokana na changamoto hiyo, aliwataka viongozi kuongeza jitihada katika kumaliza tatizo la maji Afrika.
Kibaki kwa sasa ni Balozi Maalumu wa Maji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Elimu Sayansi na Utamaduni (Unesco) barani Afrika.
Kibaki ambaye alikuwa kivutio katika mkutano baada ya kutoa hotuba yake, wajumbe karibu wote walisimama na kumpigia makofi.
“Maji ni tatizo linalolikumba bara la Afrika hivi sasa kwani licha ya kwamba asilimia 15 ya watu duniani wapo barani Afrika, ni asilimia tisa tu ya vyanzo vya maji safi duniani vinapatikana Afrika,” alisema Kibaki.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo la sita, alisema Tanzania ina vyanzo vingi vya maji lakini bado kuna tatizo la upatikanaji wa maji vijijini.
Alisema kongamano hilo ni fursa kwa wataalamu wa maji kuja na maazimio ya namna ya kuhakikisha vyanzo vya maji vilivyopo vinatumika na wananchi wote wanapata maji.