YASSIN ISSAH NA WILLIAM BAZOMBANZA (TSJ), DAR ES SALAAM
MWENYEKITI wa Mtaa wa Sharif Shamba Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam, Joseph Kimoko, amewataka wakazi wote wa mtaa huo kujisajili upya katika daftari la makazi.
Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya agizo lililotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Juni 16 mwaka huu, ambapo alisema kutakuwa na msako maalumu wa nyumba kwa nyumba jijini humo ili kuhakiki watu wasiokuwa na kazi maalumu ili kudhibiti usalama.
Akizungumza na MTANZANIA ofisini kwake jana, Kimoko aliwataka waliohamia katika mtaa huo bila kusajiliwa na wale ambao wanatarajia kuhamia, kujisajili katika daftari la makazi. Mpaka sasa mtaa huo una jumla ya wakazi 70,000.
“Wajumbe waongee na wenye nyumba na wanaohamia katika maeneo yao ili kuhakikisha wanakuja na barua zao zinazowatambulisha walipotoka na kuhakikisha wanasajiliwa katika daftari la wakazi wa mtaa huu ili watambulike,” alisema Kimoko.
Aidha, mwenyekiti huyo alizungumzia suala la usafi huku akisisitiza kila mwananchi kushiriki vyema ili kuweka mazingira salama katika mtaa huo kwa kulipa Sh 10,000 kwa kila kaya kwa ajili ya uzoaji taka.
Kimoko pia aliiomba Serikali kuweka michoro ya pundamilia katika makutano ya barabara ya Uhuru, kituo cha msaada gereji, kwa kuwa inatumiwa kwa kiasi kikubwa na wanafunzi.