26.6 C
Dar es Salaam
Sunday, November 3, 2024

Contact us: [email protected]

Sare za bil 60/- zayeyuka polisi

RAIS Dk. John Magufuli
RAIS Dk. John Magufuli

TUNU NASSOR, DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli, amefichua ufisadi wa kutisha wa fedha kati ya Sh bilioni 20 hadi 60 zilizotolewa kwa ajili ya kushona sare za polisi, lakini hakuna sare hata moja iliyoshonwa.

Akizungumza wakati wa hafla ya kula kiapo cha utumishi wa umma kwa maofisa 25 ambao wametoka cheo cha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) na kuwa Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Ikulu, Dar es Salaam jana, Rais Magufuli alisema fedha hizo zimechotwa mwishoni mwa mwaka jana.

Alisema taarifa alizonazo ni kwamba, kuna mtu amelipwa fedha hizo ambazo zilitolewa ndani ya wiki moja na jeshi hilo, lakini hakuna sare hata moja iliyokabidhiwa.

“Kuna minong’ono  kuwa mwishoni mwa mwaka jana kuna mtu amelipwa fedha kati ya bilioni 20 na 60 kwa ajili ya kushona sare za polisi, hakuna hata sare moja iliyokabidhiwa kwa Jeshi la Polisi,” alisema.

Rais alisema kwa kuwa viongozi wote wa ngazi za juu wa jeshi hilo wamesikia jambo hilo, anaamini watalifanyia kazi.

“Nina uhakika Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP),Ernest Mangu na  Katibu Mkuu, Meja Jenerali Rwegasira mmelisikia, ninategemea siku moja hao wahusika hasa wakuu watapelekwa mbele ya haki,” alisema.

WATUMISHI

Akionekena kutofurahia hali hiyo, Rais Magufuli ameagiza kuondolewa mara moja watumishi wote ambao si askari ndani ya jeshi hilo na kuagiza wapangiwe kazi nyingine uraiani.

“Kama mnafikiri kuwa na raia kwenye Jeshi la Polisi wanawaharibia kazi zenu, hamisheni wote muwapeleke Utumishi, kwani hakuna mhasibu  ambaye ni polisi? Hakuna mhandisi ambaye ni polisi, hakuna administrator (mtawala) ambaye akawa ni polisi,nafikiri kama wizi na utumishi hewa unasababishwa  na raia waliomo ndani ya jeshi na majeshi yetu,waondolewe,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema taasisi za kijeshi kufanya kazi na raia, kunaweza kusababisha wizi na utumishi hewa jambo ambalo linaingiza hasara ya mamilioni ya fedha kwa taasisi hizo .

“Kwanini mnakaa na raia wakati  hajui hata kupiga saluti, akikosea huwezi kumpiga ‘extra deluge’, hawezi hata kulala ‘lockup’,  mambo mengine mnayatafuta wenyewe au wapo kwa misingi fulani.

“Kuna wachache ambao inawezekana ni asilimia 0.0001 ya watendaji ndani ya polisi ambao kwa makusudi au kwa nia yao mbaya wanalichafua Jeshi la Polisi, naomba mkawashauri, mkawaelekeze na ikishindikana mkawaondoe ndania ya jeshi,” alisema Rais Magufuli.

Alisema jeshi hilo, ni chombo muhimu kwa ajili ya usalama wa nchi, hivyo yanapojitokeza mambo madogo madogo yanayosemwa kila siku husababisha ukakasi.

“Mfano mzuri ni juzi juzi palikuwa na mhasibu ambaye aliorodhesha watumishi wake ambao si askari na kulipwa penseni ‘allowance’ wanayolipwa askari, zimelipwa fedha nyingi mamia ya mamilioni.

“Lakini inawezekana huyu mtu alikuwa muhimu sana pale wizarani,alikuwa ‘very powerful’, mtu mwenyewe wala sio askari alikuwa na mamlaka hata ya kukemea askari kwa sababu anashika pesa, nikampigia Meja Jenerali (Rwegasira),alikuwa  Mbeya nikamwambia huyu mtu asimamishwe mara moja na apelekwe mahakamani,” alisema.

Alisema pamoja na kuwa jeshi hilo linafanya kazi ya kukamata wahalifu, walishindwa kumkamata muhasibu huyo.

“Kitu cha kujiuliza nyie polisi ndio mnashika na kupeleka mahakamani wahalifu,  hata raia akiiba kuku mnakamata kikamilifu, leo mwizi mliye naye makao makuu mnashindwa kumshika?, mnajua kupeleleza na mna vyombo vyote ofisi ya IGP, DCI makamishina wanazunguka wanarudi pale polisi naye yuko pale mnashindwa kumshika,” alisema Rais Magufuli.

Alisema kulikuwapo na ofisa mmoja  ndani ya jeshi hilo, lakini sasa ameondolewa alikuwa akiombwa mafuta anajibu tulikupa cheo nenda ukatumie utapata mafuta.

Kuhusu mchakato wa kuwapandisha vyeo maofisa hao, Rais Magufuli alisema  ulikuwa mrefu ambapo alimwagiza IGP kwa zaidi ya miezi mitano.

“Nawapongeza nyinyi ambao mmefikia nafasi hii ya kuteuliwa,  ninafahamu mchakato ulikuwa mrefu na mzito waliokuwa wamependekezwa na kufika kwangu wametoka cheo cha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) na kuwa Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) walikuwa 31, wamerudi 25 huku Naibu Kamishina walikuwa 46, wamerudi 35,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema waliosikia majina yao yamekwenda, lakini hayakurudi amewapa muda wa kujirekebisha.

“Naomba mkawaambie majina hayakurudi kwa ajili yangu, wasihangaike kumtafuta mchawi, baada ya kupata taarifa  na data zote tulizonazo tukaona tuwape muda wa kujirekebisha,” alisema Rais Magufuli.

Alisema hivi sasa, jeshi hilo limeanza kumwelewa kwa kuwa hakuna mahali kituo kimevamiwa na askari akauawa  bila mvamizi kunyang’anywa silaha hiyo.

“Kwa sababu hata niliokuwa na mashaka nao, hapa baada ya kuhamishwa maeneo yao ya zamani na kupelekwa mahali pengine wamefanya kazi vizuri,” alisema.

“Polisi mfanye kazi zenu za kiaskari na inawezekana yule kwa kuwa ni raia mlishindwa, hata kumchukulia hatua, najiuliza raia wa jeshi la polisi hashughulikiwi  mbona raia wa huku uraiani wanashughukiwa? alihoji Rais Magufuli.

Alisema makamanda hao wanawategemewa katika nchi hii kutekeleza wajibu wao bila woga kwa kuzingitia sheria .

“Wapo watu waliwahi kuumizwa humu siku za nyuma, ukishika basi likawa la ndugu fulani wa polisi  utakipata…kulikuwa na basi linaitwa Buffalo ninyi mnalijua ukiligusa hilo basi ujue mahali ulipo utaondolewa tu,” Alisema Rais Magufuli.

Alisema polisi wadogo wanaowaongoza wawape madaraka ya kutekeleza kazi zao, hata akishika gari la IGP amwache.

“Kama amekamata gari la IGP, waziri ama la Rais, mwache akatekeleze majukumu yake, sheria ni msumeno wanapotimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria msiwakataze, akishatoka pale aliyeshikwa anatamba na polisi huyo mnamvunja nguvu za kufanya kazi,” alisema Rais Magufuli.

MELI ZA MIZIGO

Akizungumzia kuhusu kupungua kwa meli za mizigo bandarini, Dk. Magufuli alisema ni bora zisije kama zinaleta bidhaa ambazo hazilipiwi kodi.

“Watu wanasema  hoteli hazina wateja na watalii watashindwa kuja, baada ya kuongeza VAT bora kuwa na watalii watano wanaolipa kodi kuliko kuwa nao 200 wasiolipa kodi,” alisema Rais Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles