Na ADAM MKWEPU – DAR ES SALAAM
WAPINZANI wa Yanga katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika timu ya Medeama, wametamba kujua udhaifu wa timu hiyo kwani wiki mbili walizotumia kuwasoma wapinzani wao zinatosha kuwapa pointi tatu muhimu kwenye mchezo wao unaotarajiwa kuchezwa kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga itaingia dimbani ikiwa tayari imepoteza michezo miwili ya awali ya Kundi A, ukiwamo wa Mo Bejaia ya Algeria ilipofungwa bao 1-0 ugenini pia dhidi ya TP Mazembe, ilipofungwa bao 1-0 ikiwa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Kocha Mkuu wa Medeama, Prince Yaw Owusu, alisema wachezaji wake watapambana ili kupata pointi tatu muhimu zitakazowawezesha kuwa katika nafasi nzuri ya kusonga hatua inayofuata.
“Siwezi kusema moja kwa moja kwamba naijua Yanga au siijui, lakini muda niliotumia kuisoma utanisaidia kupata matokeo mazuri katika mchezo huo kwani nimeona udhaifu wao,” alisema Owusu.
Kwa upande wake nahodha wa timu hiyo, Mohammed Tagoe, alisema kwa pointi moja waliyonayo haitoshi kujiamini na kudharau mchezo huo.
“Wengi wetu hatuifahamu vizuri Yanga, lakini haitoshi kusema mchezo huo utakuwa rahisi au mgumu kwani hata hii pointi moja tuliyonayo bado haitupi hali ya kujiamini,” alisema Tagoe.