Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa timu ya Simba Mcameroon, Joseph Omog, ameeleza kuwa katika kikosi chake anahitaji wachezaji wenye uchu wa ushindi, wenye vipaji na wapambanaji, pia walio na uwezo ndani na nje ya uwanja.
Omog anatamani wachezaji alionao katika kikosi chake waendelee kuwa makini na kuonyesha nidhamu siku zote ndani na nje ya uwanja kama wanavyofanya sasa kambini Morogoro, ili aweze kujenga timu anayotaka.
Simba imeweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara Morogoro, ambapo kocha huyo ameeleza kwamba katika siku nne walizokaa huko, ameshuhudia vipaji mbalimbali kutoka kwa wachezaji waliopo kambini.
Akizungumza na MTANZANIA, Omog alisema wameanza kufanya kazi ya kujiandaa kwa kasi, wachezaji wanaonyesha umakini na nidhamu ya hali ya juu, hivyo anaomba juhudi hizo ziendelee siku zote atakapokua na timu hii na isiishie Morogoro.
“Natamani kuwa na timu ya ushindi, wapambanaji na yenye nidhamu, sasa hivi ni mapema sana kuzungumzia uzuri au aina ya wachezaji tulionao, labda wiki ijayo ila naona kuna vitu vizuri tu katika timu.
“Tuna tatizo kubwa la umakini na nidhamu kwa wachezaji wetu wa Afrika, lakini naomba hili lisiishie wakati huu tukiwa kambini, liendelee hata tukianza ligi litatusaidia kupata matokeo mazuri tukiwa uwanjani kwani nidhamu ni msingi bora wa mafanikio,” alisema.
Omog alieleza kuwa ana imani baada ya wiki moja atakua amekisoma vizuri kikosi chake, kujua anahitaji nini kabla ya kuanza kwa ligi ili arekebishe mapema.