29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

Mkapa kuwasilisha ripoti kwa wakuu wa EAC

Benjamini Mkapa
Benjamini Mkapa

NA ELIYA MBONEA, ARUSHA

MWEZESHAJI wa mazungumzo ya kusaka suluhu ya mgogoro wa kisiasa nchini Burundi, Rais mstaafu, Benjamini Mkapa, anatarajiwa kuwasilisha ripoti yake mbele ya wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), mjini Kigali Rwanda.

Akitoa taarifa kwa wajumbe wa mkutano huo mjini hapa jana baada ya kumalizika kwa kikao kilichokutanisha makundi yanayotofautiana nchini Burundi, Msaidizi wa Rais mstaafu Mkapa, Balozi Gabriek Kapya, alisema mazungumzo hayo ya siku mbili yalimalizika kwa amani.

“Rais mstaafu Mkapa anawashukuru wote kwa kuhudhuria kikao hiki na anatarajiwa kuondoka leo (jana) kwenda Kigali, Rwanda kutoa taarifa kuhusu mazungumzo ambayo tumekuwa tukiendelea nayo mjini hapa,” alisema Balozi Kapya.

“Baada ya kuwasilishwa kwa taarifa hiyo na kupatiwa mwongozo utakaotolewa huko, tunatarajia kukutana tena kwenye vikao vitakavyokuwa vimepangwa. Kwa hiyo, amewatakiwa safari njema na muendelee salama,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Upinzani cha RADEBU cha nchini Burundi, Jean De Dien Mutabuzi, alipokuwa akizungumza baada ya kumalizika kwa kikao hicho, aliomba kikao kingine kitakachopangwa kisifanyike jijini Arusha badala yake kifanyike nchini Burundi.

Akifafanua kuhusu hoja yake hiyo, Mutabuzi alisema wahusika wengi wa mgogoro huo wanaishi Burundi hivyo ni vema mazungumzo hayo yakafanyika huko.

Akitolea mfano wa hoja yake hiyo, alisema Burundi kuna baadhi ya vyama vingi vilivyoshiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ambavyo navyo vinastahili kushiriki mazungumzo hayo.

Akizungumzia kuhusu swali waliloulizwa na Rais mstaafu Mkapa kuhusu taarifa za malalamiko ya watu kuhusu jeshi la nchi hiyo kuipendelea Serikali na chama tawala, Mutabuzi alisema taarifa hizo hazina ukweli wowote.

Kuhusu ushiriki wa asasi za kiraia katika mazungumzo hayo, aliendelea kusisitiza kwamba wamemuomba Rais mstaafu Mkapa kutowaalika tena viongozi wa asasi hizo kutokana na kutokuwa na ushirikiano wala msaada wa upatikanaji wa amani.

Wakati mazungumzo hayo yakiendelea katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), juzi mjini hapa vyama vitano vya kisiasa vilitoa tamko la kupinga viongozi wa asasi za kiraia kushiriki mazungumzo hayo kwa kile kilichoelezwa kuwa hawahusiki.

Naye Katibu Mkuu wa Chama Tawala nchini Burundi, CNDD –FDD, Gelase Ndabirabe, alimuomba Mkapa kuangalia suala la ukabila kwani ndilo limekuwa chanzo kikuu cha mgogoro huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles