Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAKURUGENZI wateule wa halmashauri walioteuliwa na Rais Dk. John Magufuli, leo wanatarajiwa kupewa semina elekezi na kuapa kiapo cha utumishi wa umma.
Pamoja na hatua hiyo pia wakurugenzi hao wametakiwa kufika na nakala za vyeti vya elimu na taaluma.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, iliwataka wakurugenzi wa halmashauri za majiji, manispaa, miji na wilaya walioteuliwa Julai 7, mwaka huu kufika Ikulu Dar es Salaam wafike na nakala zao halisi za vyeti vya taaluma (Original Academic Certificates).
“Ieleweke kuwa uhakiki wa vyeti halisi vya taaluma (Original Academic Certificates) unafanywa kwa lengo la kujiridhisha baada ya mchakato wa kawaida wa uhakiki kufanywa kwa kutumia vyeti visivyokuwa halisi (Photocopies).
“Uhakiki huu wa vyeti utaanza saa 2.00 asubuhi na wahusika wote mnaombwa kuingia Ikulu kwa kupitia lango kuu la lililopo upande wa mashariki,” ilieleza taarifa hiyo.