NA FARAJA MASINDE, DAR ES SALAAM
RAIS Dk. John Magufuli, amehutumia kwa lugha ya Kiswahili katika hafla ya dhifa ya kitaifa aliyomwandaliwa Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi ambaye alikuwa nchini kwa ziara ya mbili.
Alisema lengo la kutumia lugha hiyo ni kuikuza na kukitangaza Kiswahili kama lugha mama ya taifa.
Hafla hiyo ilifanyika Ikulu Dar es Salaam jana na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Katika ziara hiyo, Tanzania na India zilisaini mikataba ya miradi ya maendeleo katika sekta za maji, kilimo, viwanda, teknolojia ya habari na mawasiliano na afya katika kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili kusaidia wananchi wake.
Mikataba hiyo ilisainiwa na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi baada ya kumalizika mazungumzo na Rais Magufuli.
Mikataba iliyosainiwa ni ya mradi wa kusambaza maji katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam, mradi wa kusambaza maji Zanzibar wenye gharama za Dola za Marekani milioni 92. Mradi huo unatarajiwa kufikia miji 17 nchini.
Mikataba mingine ni unaohusisha mafunzo ya ufundi yatakayosaidia kuzalisha wataalamu mbalimbali ambako Waziri Mkuu, Modi alisema utasaidia kuimarisha uhusianao kati ya nchi hizo mbili.
Waziri Mkuu Modi alisema Serikali ya India itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuongeza wigo wa biashara na hatimaye kukuza uchumi wa nchi hizo.
Naye Rais Dk. John Magufuli, alisema Serikali India imekua na ushirikiano mzuri na Tanzania hasa katika masuala ya maendeleo na imeweza kuwekeza nchini dola za Marekani bilioni 2.4 na kuzalisha ajira 54,176.
Alisema baadhi ya misaada iliyotolewa na Serikali ya India ni pamoja na mashine ya vipimo vya saratani katika Hospitali ya Bugando.
India pia imeahidi kuanzisha viwanda vya kutengeneza dawa za binadamu zitakazotibu magonjwa mbalimbali ikiwamo malaria, figo na kisukari, na kutengeneza vifaa tiba vitakavyotumika katika hospitali mbalimbali nchini.
Rais Magufuli alisema India ina uhitaji mkubwa wa mazao ya kilimo hasa jamii ya kunde hivyo akawataka wakulima kutumia fursa hiyo kuzalisha mazao hayo kwa wingi.
“India ina uhitaji wa tani 200 za mazao jamii ya kunde, wakulima mnatakiwa kuzalisha mazao hayo kwa wingi kwa vile tayari kuna soko la uhakika, na tutahakikisha madalali hawatakuwapo ili mkulima asikandamizwe,” alisema Rais Magufuli.
Katika sekta ya uwekezaji nchini, India ni nchi ya tatu kwa uwekezaji Tanzania ikifuatiwa na Uingereza na China.