Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesitisha utoaji wa vibali vya uvunaji wa mbao kutoka katika mashamba nane ya miti ya kupandwa yanayosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana, Majaliwa, alilitoa agizo hilo na kufafanua kuwa usitishaji huo unalenga kutathmini taratibu, kanuni na vigezo sahihi vinavyotakiwa kutumika katika kugawa malighafi kutoka katika mashamba hayo.
Alisema wadau wote wa viwanda vinavyojikita katika malighafi ya misitu na hasa wamiliki wa viwanda vya kupasua mbao wanashauriwa kuwa watulivu.
“Wadau wote wanatakiwa kuwa wavumilivu wakati utaratibu huu ukifanyiwa mapitio na umma utatangaziwa rasmi pindi uboreshaji huo utakapokamilika,” alisema Majaliwa.
Serikali kupitia (TFS) chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii inamiliki mashamba ya miti ya kupandwa 18 na kati ya hayo uvunaji umekuwa ukifanyika katika mashamba nane ambayo ni Sao Hill (Mufindi), Buhindi (Sengerema), Meru/Usa (Arumeru), West Kilimanjaro (Hai), Shume (Lushoto), North Kilimanjaro (Rombo), Kiwira (Rungwe) na Kawetire (Mbeya Vijijini).