Veronica Romwald na Asifiwe George, Dar es Salaam
RAIS Dk.John Magufuli, ametangaza vita dhidi ya viongozi wa Serikali na wawekezaji wanaofanya dhuluma na kuchukua mali za madhehebu ya dini nchini.
Aliyasema hayo jana alipozungumza katika Baraza la EId el Fitir lililoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kwenye viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam.
Alisema viongozi hao wamekuwa wakiwahadaa viongozi wa dini na kuingia nao mikataba ya kitapeli na baadaye kuwadhulumu mali za taasisi za dini.
“Nakumbuka nilipokuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pale, viongozi wa Bakwata mlikuwa mnakuja ofisini kwangu kulalamika juu ya suala hili, wanawadanganya mnaingia nao ubia kumbe ni wa kitapeli.
“Nawashauri Bakwata kuwatumia mawakili mlionao pamoja na viongozi wa madhehebu mengine kuhakikisha mnakomboa mali za taasisi zenu zisije zikasababisha migogoro itakayoleta uvunjifu wa amani,” alisema.
Rais Magufuli aliahidi kuwa Serikali yake itashirikiana na viongozi wa dini kuzikomboa mali zao.
“Tunawapenda wawekezaji, lakini haiingii akilini taasisi mnatafuta eneo kwa ajili ya kujenga msikiti, halafu mtu anawadanganya kwamba anawekeza kwa kujenga sheli… kipi kilicho bora hapa kuabudu au kujenga sheli?” alihoji.
Hata hivyo, aliwasihi Waislamu kuendelea kutenda mema kama walivyokuwa wakifanya wakati wa Mfungo wa Ramadhani.
“Nawasihi mfanye kazi, bila kufanya kazi kwa bidii ili tukuze uchumi wa nchi, wapo wanaolalamika fedha haipo, hawa ni miongoni mwa wale wachache waliokuwa wanadhulumu.
“Msichoke kutombea, tumeamua kufanya kazi, tunataka kuifikisha Tanzania mahali na kurudisha heshima yake, hatutamuonea mtu katika hili lazima wachache wataguswa,”alisema.
MUFTI
Akizungumza katika baraza hilo, Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubery aliwataka viongozi wa dini kuendelea kuhimiza umoja, amani na mshikamano uliopo.
“Tumepata Rais Magufuli ambaye ni mfano kwetu, leo (jana) amepamba baraza letu, hii inaonyesha ukarimu alionao wa kujali wananchi wake. Hii inaonyesha kwamba tumepata kiongozi katika muda mwafaka.
“Magufuli ni mvua inayonyesha kwa muda mwafaka. Katika mafunzo ya dini tuliyojifunza katika mwezi wa Ramadhani ni ucha Mungu, uadilifu, ukweli, kuishi na watu vizuri. Natarajia kwamba yatafanyiwa kazi,” alisema.
Alikemea ndoa za jinsia moja akisema zinaharibu maadili na zinaweza kuleta balaa katika taifa.
“Lazima tuseme hili, vinginevyo taifa litaangamia. Tumesikitishwa pia na kitendo cha mtu aliyejilipua katika msikiti ulioko Saudi Arabia, Mecca,” alisema.
Katibu wa Bakwata
Akisoma tamko la Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Katibu wa baraza hilo, Sheikh Suleiman Lolila alisema wanamuunga mkono Rais Magufuli kwa kasi ya utendaji wake.
“Mungu anetupa viongozi wenye maono ya mbali na wenye mahaba na wananchi wao, Mheshimiwa Rais Waislamu tupo nawe bega kwa bega kwa jitihada zako unazochukua katika kulikomboa taifa kiuchumi,” alisema.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, akiwamo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Rais mstaafu, Alhaj Ally Hassan Mwinyi na Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita.
Rais Magufuli alimzawadia Sh milioni mbili, Salmu Mussa ambaye anatarajiwa kwenda Urusi kushiriki mashindano ya kusoma Quruan.
Vilevile alitoa kiasi kama hicho kwa kikundi waumini watakaosafiri kwenda kuhiji Agosti, mwaka huu.
Majaliwa
Naye Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisisitiza umuhimu wa kudumisha amani na akakemea vitendo vyovyote vile vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Majaliwa alitoa kauli hiyo jana, wakati wa Swala ya Eid iliyofanyika kitaifa katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wanasiasa na waumini wa dini hiyo.
Akitoa salamu za Serikali, Majaliwa aliwataka waumini hao kuwaombea marehemu waliofariki dunia katika ajali ya mabasi ya City Boy iliyotokea mkoani Siginda juzi na kuua watu 31, akisema ajali hiyo ilisababishwa na uzembe wa madereva.
Dk. Shein
Na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.Ali Mohamed Shein amewakumbusha viongozi wa vyama vya siasa kuwa ni wajibu wao kuhimiza utiifu wa sheria, amani, utulivu na usalama wa nchi na kuhamasisha upendo miongoni mwa jamii.
Akizungumza wakati wa Baraza la Eid jana, Dk. Mohamed Shein alisema viongozi hawapaswi kuhamasisha wafuasi wa vyama vyao kufanya vitendo vya hujuma na kuleta sintofahamu katika jamii.
Alisema viongozi kuwachochea wafuasi wao kufanya vitendo kama hivyo ni “kinyume na maamrisho ya Mwenyezi Mungu”.
Dk. Shein alitoa mfano wa vitendo ambavyo vimekuwa vikifanyika kisiwani Pemba baada ya kumalizika uchaguzi mkuu wa marudio Machi, mwaka huu.
DODOMA
Naye Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Ahmed Saidi ameiomba Serikali kuwachukulia hatua kali madereva wazembe wanaosababisha ajali kwa wananchi wasiokuwa na hatia.
Alisema ajali hizo hazisababishwi na Mungu,bali wanadamu wenyewe.
Alitoa ombi hilo jana wakati alikitoa mawaidha kwa waumini wa dini ya Kiislamu katika ibada ya sikukuu ya Eid el Fitri katika Msikiti wa Gadaffi.
Sheikh Saidi alisema ni wakati wa Serikali kutoa adhabu kali kwa madereva ambao wanasababisha ajali na vifo kwa Watanzania wasiokuwa na hatia.
‘’Ajali anapanga Mungu, kuna madereva wamekuwa wazembe mno, Serikali iwawajibishe ili wengine wajifunze kupitia adhabu hizo.
“Angalieni kama ile ajali iliyotokea Kijiji cha Maweni wilayani Manyoni. Mabasi mawili tena ya kampuni moja ya City Boy jinsi madereva wake walivyokuwa wazembe na kusababisha vifo vingi,” alisema.