Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JCKI), imejitenga rasmi na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) hatua itakayoifanya kuwa taasisi kamili itakayoendesha shughuli zake za matibabu kwa kujitegemea.
Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi kwa njia ya simu Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi, alisema sasa watatoa huduma chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
“Awali, JCKI-Muhimbili ilifanya shughuli zake chini ya uongozi wa MNH, lakini kuanzia Julai mosi, mwaka huu imeanza kujitegemea kutoa huduma za matibabu chini ya Wizara ya Afya.
“Hivyo basi tunapenda kuwahamasisha wagonjwa wetu wote wanaopata huduma katika taasisi yetu kuwa huduma zetu zitaendelea kutolewa kama kawaida na kwamba tumejipanga kuwahudumia vizuri zaidi kwa kushirikiana na wenzetu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili na Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI),” alisema Profesa Janabi.
Pia alisema tangu JKCI ilipoanza mwaka jana kutoa huduma ya matibabu hadi kufikia Juni, mwaka huu wameweza kutibu wagonjwa 26,052.
“Kati ya wagonjwa hao, 24,408 walikuwa ni wagonjwa wa nje (wanaotibiwa na kuondoka nyumbani), 1,644 walikuwa ni wagonjwa wa ndani (waliolazwa) na vifo vilivyotokea katika kipindi hicho ni 115 sawa na asilimia saba,” alisema Profesa Janabi.
Alisema mbali na Watanzania, pia wamefanikiwa kuwatibia wagonjwa kutoka katika mataifa mengine ikiwamo Nigeria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Italia na Comoro.
“April 25, mwaka huu wataalamu wetu walisafiri pia kwenda nchini Rwanda ambako walifanikisha upasuaji kwa wagonjwa 25. Haya kwetu ni mafanikio makubwa,” alisema Profesa Janabi.
Pia katika kipindi cha Januari hadi Juni, mwaka huu, jumla ya wagonjwa 197 walifanyiwa upasuaji huku watoto wakiwa ni asilimia 61.7, watu wazima ni asilimia 38.3, waliofanyiwa upasuaji wa wazi ni 148 na upasuaji bila kupasua kifua ni 49.
“Hii ni asilimia 95.1 ya upasuaji wote tuliofanya mwaka jana (tulifanya wagonjwa 207). Asilimia 62 ya upasuaji huu umefanywa na madaktari Watanzania kwa asilimia 38 kwa kushirikiana na wataalamu kutoka nje ya nchi,” alisema Profesa Janabi.
Kuhusu wagonjwa waliopelekwa kutibiwa nje ya nchi, alisema waliopelekwa India katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya mwaka huu ni 10.