32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Azam watambia makocha vijana

AZAM-FC_0NA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM

UONGOZI wa klabu  ya soka ya Azam, umesema kwamba  ubora wa klabu hiyo msimu ujao utaimarika mara dufu  baada ya kuajiri makocha vijana kuwazidi wapinzani wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambao  bado wanahaha na makocha wenye umri mkubwa.

Kauli hiyo ya Azam inatokana na hivi karibuni kuajiri makocha wawili vijana kutoka klabu ya Deportivo Tenerife ya Hispania  akiwamo Kocha Mkuu, Zeben Hernandez na msaidizi wake, Jonas Garcia, baada ya kuachana na kocha wao wa zamani, Stewart Hall.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Saad Kawemba, alisema  klabu zinatakiwa kuendana na mabadiliko ya soka duniani ndio maana wao waliamua kuajiri  makocha vijana ili  kuendana na kasi iliyopo.

“Ni makocha hodari na imara hawatayumbishwa na  jambo lolote,  hata hivyo tumeamua kuwa  tofauti na klabu nyingine hapa nchini.

“Pia tumeamua suala la usajili liwe chini yao na kuondoa dhana ya lazima usajili ufanywe na viongozi kama ilivyo kwa wapinzani wetu,” alisema Kawemba.

Kawemba aliongeza kwamba ingawa hadi sasa hawajafanya usajili wa aina yoyote hadi pale makocha hao watakapowasili kutoka  mapumziko nchini Hispania, hawatishwi na wapinzani wao kwa kuwa hawazingatii utaratibu wa kufanya usajili wenye tija.

“Klabu pinzani zinafanya usajili  lakini hauna tija kwa kuwa  unafanywa na viongozi  badala ya kocha wa timu husika,  ndio maana kunakuwa  na vitendo vya kuwafukuza makocha mara kwa mara,” alisema Kawemba.

Akimzungumzia Hall, Kawemba alisema kwamba  bado angeweza kuwa kocha wa timu hiyo  kama  angependa kuendelea kukinoa kikosi hicho.

“Hall ni kocha ambaye anajua kila kitu kuhusu Azam FC, ndio maana tunamtumia mara kwa mara tukiona haja ya kufanya hivyo,” alisema Kawemba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles