*Wenyewe waomba uzalendo utumike kuwasaidia
NA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limesema klabu ya soka ya Yanga iache kutumia njia ya mkato kutafuta mwafaka wa kupata barua kutoka Simba, ili imruhusu mchezaji wake wa zamani, Hassani Ramadhani ‘Kessy’, kucheza timu hiyo.
Yanga juzi iliiandikia barua TFF ili kuisaidia kuiomba Simba kuandika barua ya kumruhusu Kessy kucheza kwenye timu hiyo, hasa baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kumbania mchezaji huyo hadi hapo atakapokuwa na barua itakayoonyesha Simba imemruhusu acheze michezo ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Alfred Lucas, alisema klabu hiyo haiwezi kufanikiwa jambo hilo kwa njia ya mkato badala yake wanatakiwa kuipelekea TFF nakala ya barua inayothibitisha ruhusa ya mchezaji huyo kutoka Simba si kuingilia kati kuiomba Simba barua hiyo.
“Tatizo kubwa la klabu zetu ni kukimbia semina za usajili zinazotolewa ndio maana leo hii hazifahamu majukumu yao na kukimbilia TFF ili kuingilia kati wakati si kazi yake.
“Yanga walitakiwa kuiandikia barua Simba kuiomba imruhusu Kessy ili aweze kucheza michezo ya kimataifa na si kukimbilia TFF kwa kuwa suala la usajili linafanyika na klabu zenyewe kwa kumshirikisha mchezaji na baadaye kuhakikiwa na TFF kwa kupewa nakala ya barua ya ruhusu kutoka kwa timu husika,” alisema Lucas.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa klabu ya Yanga, Baraka Deusdedit, aliwaomba TFF na Simba kuwa wazalendo ili kufanikisha barua hiyo itakayotoa ruhusa mchezaji huyo kucheza michezo ya Kombe la Shirikisho.
“Tumepeleka barua hiyo kama wanachama wa TFF ili kutupatia kibali cha usajili wa ndani ambacho kitakuwa kinatoa ruhusa moja kwa moja kwa mchezaji huyo kucheza michuano hiyo.
“Tunajua vibali vya kuthibitisha wachezaji wapya vitatolewa mwishoni mwa usajili lakini tuliiomba TFF itusaidie kwa kujaribu kuwa na uzalendo kutokana na umuhimu wa mchezo na mchezaji mwenyewe katika kikosi,” alisema Deusdedit.
Aliongeza kuwa klabu hiyo ililazimika kupeleka barua hiyo TFF si Simba kutokana na klabu hiyo kuwa mwanachama wa TFF ambao wanahusika na matatizo ya klabu na wachezaji.