JOHANES RESPICHIUS NA BARAKA MASSAWE (TSJ), DAR ES SALAAM
WAKALA wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) imekamata na kutaifisha madini yenye thamani ya Sh bilioni 1.3 yaliyokuwa yanatoroshwa kwenda nje.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Habari TMAA, Yisambi Shiwa, alisema ukaguzi uliofanyika Julai 2015 hadi Januari 2016 kwenye viwanja vya ndege umewezeshwa kukamatwa watoroshaji wa madini katika matukio 16.
“Matukio haya yalihusisha madini yenye thamani ya Sh bilioni 3.2 na kati ya hayo madini yaliyokamatwa na kutaifishwa yalipigwa mnada na kuingizia Serikali Sh bilioni 1.3
“Pia katika matukio hayo utoroshwaji huo karibu asilimia 70 ya madini hayo ni Tanzanite ikiwa asilimia kubwa yanatoka kwa wachimbaji wadogo kutokana na hali ya usimamizi katika vizimba huku Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) ukiongoza kwa utoroshwaji
“Na tangu kuanzishwa kwa ukaguzi matukio 89 ya utoroshaji wa madini yaliripotiwa hadi Desemba mwaka jana yakiwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 10.8 ,” alisema Shiwa.
Alisema TMAA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewezesha wachimbaji kuanza kulipa mapato ambako katika kipindi cha mwaka 2009 hadi Machi mwaka huu, kampuni mbalimbali zimelipa Sh bilioni 732.6.
Wakala huyo ataendelea kusimamia na kukagua shughuuli za uzalishaji na mauzo ya madini yote nchini na imekwisha kuweka wakaguzi katika viwanja vya ndege na mipakani kudhibiti biashara na utoroshaji wa madini.
Naye Giky Shamika Kaimu Mtendaji Mkuu TMAA, alisema Wakala huyo anaangalia namna nzuri ya kuwadhibiti watoroshaji madini wote na kubaini njia wanazopitisha.
“Kazi hii itatekelezwa kwa kushirikiana na na Polisi, TRA, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Idara ya Madini na Usalama wa Taifa kuhakikisha inaziba mianya ya utoroshwaji wa madini mipakani na kwenye Viwanja Vya Ndege,” alisema Shamika.
Alisema wamekuwa wakitoa elimu kwa mamlaka hizo ili kuyafahamu madini hayo iwe rahisi kuwabaini watoroshaji.