27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Zitto na sura zake mbili zinazojirudia kila upande -2  

kabwWIKI iliyopita tuliweza kuona sura mbili za Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), pia tuliona ni kwa namna gani sura hizo zinavyobadilika kila muda kutoka kwenye harakati mpaka usaliti na kurudi tena kwenye harakati.

Leo katika sehemu hii ya pili na ya mwisho, tuangalie upande wa pili wa chama tawala.

Kwa watawala mara nyingi mbunge anayeweza kusimamia hoja na kuibana serikali huyo huwa si mpinzani ambaye huwavutia inawezekana kwa sababu siasa zetu zinaendeshwa sana na ule mtindo wa wanaosema ndio waseme ndio na wengi huitika ndioooooooo!

Siasa zetu haziruhusu kuhoji, mara nyingi tunapenda kufuata maagizo ya wakubwa hata kama masuala hayo hayana maslahi kwa taifa lakini kwa bahati mbaya Zitto si mwanasiasa anayepatikana katika kundi hili, yeye mara nyingi huwa anahoji na nafikiri uwezo wa kuhoji unatokana na namna ambavyo anajaribu kufuatilia siasa za ulimwenguni na kuna msemo husema kama huna utafiti basi huna haki ya kuzungumza kwa Kiingereza; ‘no research no right to speak’ yawezekana pia mwanasiasa huyu hupenda kujisomea ili kupata taarifa nyingi.

Mara nyingi watu wa aina hii si chaguo la watu wanaopenda kuendesha masuala yao kwa porojo. Kama kuna kipindi upinzani ulionekana kuwa unaanza kupanda bungeni basi ni kipindi ambacho wanasiasa wa aina ya Dk. Willbrod Slaa na Zitto walikuwa mstari wa mbele kwenye kuihoji Serikali.

Ndio maana Zitto akafukuzwa bungeni na kuzuiwa kwa muda wa miezi minne baada ya kuhoji Mgodi wa Buzwagi, lakini pia alipata kuhoji kuhusu suala la Waziri Karamagi kusaini mkataba akiwa hotelini nchini Uingereza hivyo alimtaka Waziri huyo kujieleza bungeni.

Baada ya kuonekana kuwa mwanasiasa machachari inasemekana zikaundwa njama za kumpunguza kasi na ndipo baada ya muda, ikaanza kusemekana kuwa mwanasiasa huyu amehongwa na hapo ndipo tukaanza kuyasikia malalamiko ndani ya chama chake kuwa mwanasiasa huyu ni msaliti na si mwanaharakati kama tulivyomuona hapo awali.

Lakini pamoja na yote bado rekodi ilibaki pale pale kwamba Zitto alishawahi kuisumbua Serikali ya Awamu ya Nne na kuisumbua huko alijitengenezea alama kama mwanasiasa kijana mashuhuri.

Baada ya misukosuko ya muda mrefu sura ya Zitto ya usumbufu kwa watawala ikaanza kuondoka na hatimaye ikageuka na kuwa mpinzani wa kweli lakini mpinzani wa kweli huyo kwa watawala na si kwa wapinzani.

Sura ya mpinzani wa kweli

Ama kweli wahenga walikuwa ni watu wenye busara sana na ukitaka kuzifahamu busara zao basi ipitie vizuri misemo yao na katika misemo yao msemo ambao niliouona ukifanya kazi kwenye maisha ya siasa za Tanzania ni msemo wa ‘Vita ya panzi, furaha ya kunguru’

Kama kuna kipindi CCM walikuwa wakifurahia basi ni kipindi ambacho Zitto alipokuwa hana maelewano na viongozi wengine wa chama chama chake.

Ni kipindi hiki ambacho Zitto hakuwa anaonekana kwenye majukwaa ya chama chake na wakati yeye alikuwa ni Naibu Katibu wa chama, ni kipindi hiki ambacho Chadema walitangaza kutoyakubali matokeo ya urais na kutomtambua Rais lakini Zitto alikuwapo ukumbini yalipotangazwa matokeo yaliyompa ushindi Rais Kikwete na hakuishia hapo bali alimpongeza huku tamko la chama likimkataa, ni kipindi hiki ambacho Zitto hakukubaliana na maazimio ya upinzani kutoka bungeni siku ambayo Rais Kikwete alikwenda kuhutubia na ndio maana sishangai wala sikushangaa kuona kwa kipindi hicho wanachama wengi wa chama tawala walimuita Zitto mpinzani wa kweli, nafikiri walitumia ule msemo wa ‘Adui wa adui yako ni rafiki’ na walifurahi sana kwa kuwa ile dhana ya ‘Divide and rule’ yaani wagawe uwatawale ilikuwa imefanya kazi.

Hiki ndio kilikuwa kipindi ambacho nilimsikia Mwigulu Nchemba akisema Zitto ndiye mpinzani wa kweli, Ridhiwani naye alipata kusema vivyo hivyo na wanasiasa wengine wengi ambao ni wanachama wa chama tawala. Sura hii ya mpinzani wa kweli alikaa nayo kwa muda mrefu na kadiri ambavyo wanachama wa Chadema walivyokuwa wakitimuana kwenye chama basi chati ya Zitto ilikuwa ikizidi kupanda maana wapinzani (Chadema) walikuwa wakipata mashambulizi kutoka pande mbili yaani upande wa watawala na wale wanasiasa waliofukuzwa akiwamo Dk. Kitilla Mkumbo na Samson Mwigamba.

Lakini kama ilivyo kawaida maji hata yachemshwe vipi lazima yataurudia ubaridi hata kama si kwa haraka na huku uswahilini watu husema mkorogo haubadili asili zaidi ya rangi ndivyo ilivyokuwa kwa Zitto, tukaja kumshuhudia Zitto mwanaharakati, Zitto tuliyemkosa kwa muda mrefu kwenye kashfa ya Escrow, akiwa Mwenyekiti wa PAC Zitto akishirikiana na wanakamati wenzie walishirikiana kuhakikisha wananchi wanafahamu nini kinaendelea katika sakata lile na baada ya ripoti ya kamati kusomwa bungeni na mjadala kuanza nikaanza kumuona Zitto akilakiwa na wabunge wa upinzani na kushambuliwa na wabunge wa chama tawala na hili likaenda mbali maana kuna mbunge alidiriki kusema Zitto naye alipatiwa mgao na ilienda mbali zaidi mpaka mama yake kuhusishwa hali iliyosababisha Zitto kutoa chozi akitaka mama yake asihusishwe maana ni kipindi hicho Zitto alikuwa ametoka kumpoteza mama yake mzazi.

Baada ya sakata hilo mikasa ikaendelea kumuandama maana ubunge wake ambao kimsingi ulikuwa umeshikiliwa na mahakama ukafika ukingoni baada ya Chadema kushinda kesi hivyo Zitto akawa amekosa ukuta wa kuegemea na kubaki kama mwana mkiwa.

Akafanikiwa kurudi bungeni kwa tiketi ya ACT, Rais alipokwenda kuhutubia wana Ukawa wakatoka Zitto akabaki hali iliyosababisha Rais kusema Zitto ndiye mpinzani wa kweli lakini nina uhakika hakuna mwanaCCM yeyote ambaye utamwuliza hivi sasa akakujibu kuwa Zitto ni mpinzani wa kweli na ndio maana bungeni amefukuzwa na hata mikutano ya nje ya Bunge anazuiwa na siku hizi jina lake linatajwa sana polisi kuliko sehemu nyingine lakini ukiwauliza wapinzani kwa muda huu watakwambia Zitto ni kamanda.

Kwa wapinzani karudi kwenye harakati kwa watawala kawa msumbufu tunasubiri tuone kama mzunguko huu unaendelea na hizo ndio sura za Zitto Zuberi Kabwe kwa pande hizo mbili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles