30.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Mponda: Ningeendelea kuwa waziri ningekosa ubunge

Pinda  Mponda *Asema haikuwa sahihi kwa madaktari kuweka sharti ajiuzulu

NA ELIZABETH HOMBO

MWAKA 2012 ulikuwa mchungu kwa aliyekuwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda baada ya kukumbana na mgomo wa madaktari uliodumu kwa awamu mbalimbali zaidi ya miezi mitatu.
Dk. Mponda ambaye ni Mbunge Malinyi (CCM), alipoteza nafasi hiyo ya Uwaziri baada ya kuwapo kwa shinikizo la kutakiwa kujiuzulu kutoka kwa madaktari, wanaharakati na hata wabunge wa CCM.

Baada ya shinikizo hilo, Rais mstaafu Jakaya Kikwete alifanyia mabadiliko katika baraza la mawaziri na kuwatupa nje Dk. Mponda na Naibu wake, Dk. Lucy Nkya, ambapo nafasi zao zilichukuliwa na Dk.Husein Mwinyi na Dk. Seif Rashid.

MTANZANIA  imefanya mahojiano na Dk. Mponda ambaye tangu alipojiuzulu nafasi hiyo ya uwaziri hajapata kuzungumzia mgomo huo wa madktari uliosababisha akapoteza nafasi hiyo. Endelea…

MTANZANIA: Hebu tueleze historia yako kwa ufupi kisiasa na kiuongozi?

  1. MPONDA: Historia yangu ya siasa niliianza siku nyingi tangu nikiwa mwanafunzi wa shule za sekondari. Nimepata kuwa kiongozi wa Umoja wa Vijana wa TANU katika ngazi ya Wilaya ya Kisarawe 1976-1977.

Baada ya hapo niliendelea kuwa mwanachama na mshiriki mkubwa katika shughuli za Chama Cha Mapinduzi.

Pia nimeshawahi kushika nafasi za uongozi katika ngazi ya kata, tawi ndani ya chama kuanzia kipindi cha 2000 hadi 2010. Kuanzia mwaka 2010 ndio rasmi nilianza kujikita zaidi katika siasa na kuacha kuwa mtumishi wa umma kwa kugombea nafasi ya Ubunge.

MTANZANIA: Umekuwa  Mbunge kwa mara nyingine tena, nini mikakati yako kwa wapiga kura wako katika kipindi cha miaka mitano ijayo?

MPONDA: Mikakati yangu kwa wapiga kura katika kipindi hiki cha miaka mitano ijayo ni kusimamia utekelezaji wa ilani ya CCM katika jimbo langu.

Nimeahidi kwa ujumla kukuza uchumi kupitia kilimo cha biashara na ufugaji na uvuvi. Aidha, kipindi hiki nitajikita zaidi katika kuboresha au kuondoa kero katika huduma za jamii zikiwamo; miundombinu (barabara na madaraja) elimu, afya, maji, nakadhalika.

Mponda na MagufuliPili kwa jitihada zangu mwenyewe binafsi nikishirikiana na wananchi wa Malinyi pamoja na halmashauri na wadau wa maendeleo ya wilaya; tumejipanga kuwawezesha wananchi kumiliki ardhi.

Wananchi watamilikishwa ardhi kihalali watapatiwa hati miliki za kimila ili iwawezeshe kupata mikopo benki kwa maendeleo ya kilimo au mifugo.

Kuboresha miundombinu ya madaraja hususan kukamilisha ujenzi wa daraja la Mto Kilombero na mengineyo.

Kuweka mazingira rafiki ya ufugaji kwa kuweka miuundombinu ya mifugo ikiwamo Malambo ya maji, majosho, visima virefu vya maji nakadhalika.

Kuboresha kilimo kuwa cha kisasa chenye tija pamoja na kuwezesha kuwapo na soko la uhakika kwa mazao ya wakulima.

Kupunguza na hata ikiwezekana kumaliza kero ya upatikana wa maji safi na salama.

Kuboresha huduma za afya kwa kuongeza miundombinu ya afya (zahanati, vituo vya afya na hospitali) na kuongeza idadi ya watumishi katika sekta ya afya.

MTANZANIA: Ni mambo gani ambayo uliwaahidi wananchi wako katika awamu iliyopita na hukuyatimiza?

MPONDA: Ni mambo mengi ambayo nimeyafanya lakini kwa uchache ni; matumizi bora ya ardhi na upatikanaji wa hati miliki za kimila, ufumbuzi wa migogoro ya ardhi kati ya Pori Tengefu la Kilombero na migogoro ya matumizi ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima.

MTANZANIA: Ni mambo yapi ambayo uliyaahidi katika awamu iliyopita na ukayatimiza?

MPONDA: Uanzishwaji wa wilaya na halmashauri mpya, usambazaji wa umeme katika vijiji 20, uanzishaji na ukamilishaji wa madaraja ya Mwatisi na Kilombero, uboreshaji wa barabara kuu ya Ifakara-Lupiro, Malinyi-Kilosa Mpepo na mengineyo.

Pia ujenzi wa minara ya mawasiliano katika kata zisizokuwa na mawasiliano ya simu, nimewezesha mradi mkubwa wa usambazaji maji katika mji mdogo wa Lupiro na kuanza miradi mipya katika vijiji vya Minepa, Igota, Kichangani, Lupunga, Malinyi, Kipingo na Makerere.

Pia nimewezesha watoto 141 wanaoishi katika mazingira hatarishi wamelipiwa ada na kupatiwa sare na vifaa vya shule.

Kwa upande wa afya, nimehakikisha upatikanaji wa dawa, jimbo lina vituo vya afya viwili. Kituo kimoja kilikabiliwa na ukosefu wa gari la wagonjwa, gari limepatikana kwa Kituo cha Mtimbira na Kituo cha Lupiro limefanyiwa ukarabati mkubwa.

MTANZANIA: Pengine ni kero gani sugu ambayo utatuzi wake umeshindikana katika jimbo lako?

MPONDA: Katika jimbo hakuna kero ambayo utatuzi wake umeshindikana. Naomba ieleweke kuwa ni vigumu katika kipindi cha miaka mitano au hata zaidi kwamba kero zote ziwe zimetatuliwa!

MTANZANIA: Unautazamaje mwenendo wa Bunge la 11 ukilinganisha na lililopita?

MPONDA: Mwenendo wa Bunge hili la 11 naona litakuwa Bunge lililokamilika katika majukumu yake badala ya lile la mwanzo ambalo liligubikwa zaidi na itikadi za kisiasa.

Aidha, kuwapo na mchanganyiko wa wabunge wengi ni wapya (zaidi ya asilimia 60). Aidha, wengi wao ni vijana wasomi tena wa taaluma mbalimbali wakiwamo pia wa viti maalumu. Nina imani kubwa kupata michango mizuri na yenye tija katika kuisimamia, kuishauri na kuielekeza Serikali bungeni na nje ya Bunge.

MTANZANIA: Unazungumziaje kitendo cha wabunge saba wa upinzani kusimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge? Unadhani ina tija kwa Watanzania?

MPONDA: Ninakubaliana wazi na uamuzi wa kusimamishwa kwa wabunge saba. Na ninafikiri adhabu waliyopata ni ndogo wangestahili kupewa kubwa zaidi. Kwa sababu tabia zao za utovu wa nidhamu bungeni linadhalilisha Bunge kama mhimilii mkuu.

Uamuzi huu ni sahihi kabisa kwa kuwa Bunge letu linaongozwa kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Kudumu za Bunge ambazo tulizitunga sisi wenyewe kwa ajili ya kutuongoza katika kutekeleza shughuli za Bunge.

Kwa kuwa, sheria na kanuni hizo zimeweka masharti kuhusu utaratibu unaotakiwa kufuatwa katika majadiliano bungeni na kwamba katika majadiliano hayo, wabunge wanapaswa kuheshimu na kutii kanuni zilizopo na pia kutii mamlaka ya Spika.

MTANZANIA: Hili la vijembe, kuzomeana kutawala ndani ya mhimili wa Bunge nalo unalizungumziaje?

MPONDA: Hili nalilaani kabisa kama nilivyosema hapo juu. Lakini yote haya yametokana na kulegalega kwa kiti yaani Spika, Naibu wake na wenyeviti kwa kutosimamia ipasavyo kanuni za Bunge na sheria husika.

Vingineyo tusingefika hapa tulipo! Lakini kwa utawala mpya tulionao ambao umeanza kwa kuwa makini katika usimamizi wa majadiliano yetu bungeni nina hakika hili litafikia ukomo wake.

MTANZANIA: Nini ushauri wako kwa wabunge wa vyama vyote na hata kiti cha Spika?

MPONDA: Ushauri wangu kwa wabunge wenzangu ni kwamba tujiheshimu na tujikite zaidi katika kile kilichotuleta hapa bungeni na si vinginevyo. Tusilifanye Bunge kama jukwaa la kampeni za siasa. Aidha namuomba Spika asimamie sheria na kanuni katika kusimamia majadiliano bungeni, yaani asiyumbe awapo katika kiti chake.

MTANZANIA: Kwa mtazamo wako unadhani ni sahihi kusitishwa kwa matangazo ya moja kwa moja ya Bunge?

MPONDA: Mimi naona ni sahihi kwa kuwa Watanzania wengi hatutumii muda wetu kwa tija zaidi. Tumejikita sana kutumia muda mwingi katika mambo yasiyo na tija kwa uzalishaji badala yake wengi tunapanga muda kidogo sana katika kazi za uzalishaji.

Baadhi yetu tumejijengea tabia hata wakati wa saa za kazi kati ya saa mbili hadi saa kumi jioni bado tuko katika kuangalia video, Tv nakadhalika.  Wengi wetu bado hatujaelewa kwa ukamilifu dhana ya demokrasia na badala yake wananchi sasa wamelichukua suala la siasa kama ni jambo la ushabiki zaidi kama ilivyo katika mpira wa Yanga na Simba.

Hali hii ndio inayosababisha mjadala wa matangazo ya Bunge live kuendelezwa. Hususani ndugu zangu wapinzani wao ndio wanaona kama hoja ya kisiasa.  Nafikiri ni vyema sana wakati wa Bunge likiendelea na vikao vyake Watanzania wajikite zaidi katika shughuli za uzalishaji. Baada ya kazi ni vizuri sasa wananchi wakapata nafasi ya kuangalia yaliyojiri katika Bunge.

MTANZANIA: Ulipata kuwa Waziri wa Afya, unadhani ulikosea wapi mpaka ukang’olewa katika nafasi hiyo?

MPONDA: Hapana sijakosea mahali popote wakati nikiwa Waziri wa Afya ilikuwa katika kutekeleza majukumu yangu ya uwaziri.

Aidha, sijang’olewa kwa nafasi hiyo bali mimi mwenyewe ndiye nilimwomba aliyeniteua nijiuzulu katika nafasi hiyo baada ya mwendelezo wa mgomo wa madaktari mwaka 2012. Rais alitekeleza ombi langu baadaye katika mabadiliko aliyofanya katika baraza lake la Mawaziri.

MTANZANIA: Ni kweli kwamba ulishindwa kutatua kero za madaktari mpaka ikasababisha ukapoteza uwaziri?

  1. MPONDA: Kwanza naomba niseme wazi kwamba si kweli kuwa nilishindwa kutatua kero za madaktari na ndio ikawa sababu ya kupoteza uwaziri. Kero za madaktari ni za muda mrefu ni mwendelezo wa madai ya muda mrefu kama utakumbuka tangu ule mgomo wa mwaka 2005.

Maelezo ya kina kuhusu suala la kuondoka kwangu katika nafasi ya uwaziri yalishatolewa na Rais Jakaya Kikwete wakati alipofanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri Mei mwaka 2012.

Sioni sababu ya kurudia aliyosema kiongozi wangu. Lakini kwa Kifupi kwa mazingira yale ya mgomo wa madaktari ilipaswa busara zitumike kwa faida ya Watanzania.

MTANZANIA: Pengine unadhani ulionewa au nini kilikuwa kikwazo kikubwa mpaka ikafikia hali ile?

MPONDA: Nafikiri haikuwa sahihi sana kwa madaktari katika mgomo wao kuweka sharti kwamba Waziri na Naibu wajiuzulu kwa kuwa sisi hatukuwa chanzo cha kutotimizwa kwa madai yao.

Haya ndio yalikuwa madai ya Madaktari mwaka 2012

(a) Posho ya Kulala Kazini (on Call Allowance)
(b) Posho ya Kufanya Kazi katika Mazingira Hatarishi (Risk Allowance)
(c) Posho ya Nyumba
(d) Posho ya Kufanya Kazi katika Mazingira Magumu (Hardship Allowance)
(e) Kupatiwa posho ya usafiri
(f) Nyongeza ya Mshahara.Wanadai mshahara wa Sh 700,000 kwa Daktari anayeanza kazi ni mdogo sana, hivyo wanapendekeza Daktari anayeanza kazi alipwe Sh. 3,500,000 kwa mwezi.
(g) Kupatiwa Bima ya Afya
Inapendkezwa Madaktari pamoja na familia zao wapewe kadi za kijani za Bima ya Afya.
(h) Kutaka wenzao warudishwe Muhimbili. Dai hili linahusu Madaktari waliokuwa katika mafunzo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na baadaye kurudishwa wizarani, warejeshwe Muhimbili bila masharti yoyote.

(I) Kutaka Waziri, Naibu Waziri, Katibu mkuu na Mganga Mkuu wa Serikali wajiuzulu

MTANZANIA: Ulikuwa unajisikiaje pale madaktari walipokutaka wewe na Naibu wako kujiuzulu lakini hamkufanya hivyo mpaka pale mlipong’olewa?

MPONDA: Nilijisikia kawaida tu kwa kuwa kila kitu kina mwanzo na mwisho wake. Aidha, ninamshukuru Mungu kwa kuniwezesha kumaliza kazi yangu ya uwaziri kwa ufanisi na ubunifu katika changamoto, mfano uboreshaji wa mfumo wa usambazaji dawa, uhaba wa watumishi nakadhalika.

Lakini pia kuondoka kwangu nafasi hii imenipa nafasi zaidi ya kuwatumikia wananchi niliowekeana nao mkataba kwa kupitia kura zao kwa kuwawakilisha bungeni katika utatuzi wa kero zao.

Vinginevyo ningekuwa na wakati mgumu kurudi tena bungeni awamu ya pili. Tumeshuhudia mawaziri wengi wameanguka au kupata wakati mgumu katika chaguzi zilizopita. Kuna changamoto kubwa kuwatumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles