Ningeshangaa kama CUF ingemkubali Lipumba

prof-lipumbaMIMI ni mshabiki mzuri tu wa muziki, kuanzia ule wa hapa nyumbani pamoja na wa nje.  Ushabiki huu unanifanya wakati mwingine nifuatilie habari ambazo si za kipuuzi, za baadhi ya wanamuziki.  Moja ya habari nilizozifuatilia mwaka 1999, ni uhusiano wa Jenifer Lopez na P Diddy, ambaye wakati huo alikuwa akijulikana kama Puff Daddy.

Desemba mwaka huo, Puff Daddy alikamatwa na kushtakiwa kwa kukutwa akimiliki silaha kinyume cha sheria.  Hiyo ilikuwa baada ya milio ya risasi kusikika katika klabu moja mjini Manhattan, ambako mwanamuziki huyo alikuwa na mpenzi wake, Jenifer Lopez, maarufu kwa jina la J.LO. Silaha ilikutwa baadaye usiku wa manane kwenye gari walilokuwamo na baadhi ya mashuhuda walidai kwamba Puff Daddy ndiye aliyekuwa akirusha risasi hizo.

Polisi walienda kutafuta ushahidi na hatimaye kesi ikafunguliwa dhidi ya mwanamuziki huyo.  Mwanzoni mwa mwaka 2001 wakati kesi imeanza kusikilizwa, Jenifer Lopez na Puff Daddy wakatangaza kwamba wameachana.  Tangazo hilo liliibua maswali mengi, kwani kila aliyewafahamu alijua kwamba wawili hao walikuwa wakipendana sana na mahusiano yao yalikuwa yakifuatiliwa kwa karibu na mashabiki wao.

Hata hivyo, taarifa zingine zilidai kwamba J.LO ameamua kuachana na Puff Daddy, ili kujinusuru yeye mwenyewe.  Hilo lilitokana na ukweli kwamba endapo Puff Daddy angekutwa na hatia na kufungwa, basi hata maendeleo ya J.LO kama msanii yangekuwa ya mashaka, kwani huenda asingepata tena kirahisi nafasi za kuigiza, na hata album zake za muziki huenda zingepwaya.

Kutokana na hilo, Jenifer ilibidi afanye maamuzi magumu na kuachana na Puff Daddy.  Mwezi mmoja baadaye Mahakama haikumkuta Puff Daddy na hatia na ikamwachia huru.  Baada ya hilo, sisi mashabiki tukawa tukisubiri kwa hamu kubwa kuona kama Puff Daddy na J.LO watarudiana, kwani tulipenda kuwaona pamoja.  Hata hivyo, halikuwezekana.

Kutowezekana kurudiana kwa wawili hao kulitokana na ukweli kwamba siku zote walikuwa pamoja wakati wa raha, lakini mwanaume alipopata matatizo makubwa ambayo yalitishia uhuru wake, J.LO aliamua kuachana naye.  Yeye kama mpenzi wake, alitarajiwa kuwa mtu wake wa karibu, kuambatana naye mahakamani, kumliwaza na kisha kushangilia pamoja naye siku aliyoachiwa huru; ama angefungwa, basi tulitarajia kuona machozi na huzuni kubwa usoni kwa mwanadada huyo.

Hata hivyo hilo halikutokea na badala yake akaamua kuendelea na maisha yake ya kawaida.  Kwa kifupi, Jenifer alimtelekeza mpenzi wake wakati ambao alikuwa akimhitaji sana.  Na licha ya Puff Daddy kuendelea kumpenda Jenifer, mama wa mwanaume huyo alimpiga marufuku kurudiana naye, kwani hakuwepo wakati aliomhitaji zaidi.

Wiki iliyopita nilijikuta nikikumbuka hii simulizi ya wanamuziki hawa wawili, baada ya kusikia taarifa kwamba aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye alikitelekeza chama mwaka jana, amejirudi na anaomba kuruhusiwa kugombea tena Uenyekiti wa chama hicho.

Kwanza sikuamini.  Baadaye nilivyohakikishiwa kwamba ni kweli amemuandikia barua Katibu Mkuu wa chama chake kuomba kuifuta barua yake ya mwaka jana ya kujiuzulu uenyekiti, nilishangazwa mno.  Nikajisemea moyoni mwangu ngoja nisubiri majibu ya Katibu Mkuu wa CUF.

Bahati nzuri, nikasikia kwenye taarifa ya habari kwamba Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad amesema kwamba hakuna njia ambayo chama hicho kinaweza kumkubali Profesa Lipumba kugombea tena uenyekiti.  Yupo na kiongozi mwingine wa CUF ambaye alidai kwamba hata Katiba ya chama hicho hakiruhusu hilo.

Mimi binafsi ninachoweza kusema ni kwamba hata Katiba ya chama ingeruhusu, isingekuwa sahihi na haki kwa nahodha aliyetelekeza meli wakati wa dhoruba na mawimbi makali, kisha alipoona bahari imetulia, akaamua kurudi na kudai ashike usukani.  Ni ajabu sana.

Profesa Lipumba alipojiuzulu Uenyekiti wa CUF mwaka jana, ilikuwa kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.  Kwa kifupi, hicho ni kipindi muhimu kuliko vyote kwa nchi pamoja na vyama vyote vya siasa, kwani ni wakati wa vyama hivyo kujipambanua na kujipima kuona wanakubalika na wananchi kwa kiasi gani.  Kipimo hicho kinajulikana kwenye sanduku la maoni.

Kipindi hicho, Profesa Lipumba alitoa tamko akisema kuwa amekerwa na hatua ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambao CUF ni chama shiriki, kushindwa kusimamia makubaliano ya kuundwa kwa umoja huo.  Badala yake, alisema, Ukawa inakaribisha waliokuwa wakiipinga Rasimu ya Katiba ya Warioba na kuwaruhusu kuwania uongozi wa nchi kupitia umoja huo.  Akatamka kwamba nafsi yake inamsuta.

Kama mwananchi na mwanachama wa CUF, Profesa Lipumba alikuwa na haki ya kuchukua uamuzi aliouchukua wakati ule.  Kila mtu anajua kwamba hatua yake ilitokana na kukaribishwa kisha kupitishwa kwa Edward Ngoyai Lowassa kuwa mgombea wa kiti cha Urais kupitia umoja huo.

Kuingia kwa Lowassa Chadema na kisha kupitishwa na Ukawa kugombea Urais, kuliibua hisia tofauti miongoni mwa watu wengi tu, mimi nikiwa mmoja wao.  Wapo walioupongeza uamuzi wa Lipumba wakati huo, kwani ni kweli kwamba kama dhamiri yake ilikuwa ikimsuta kutokana na Ukawa kumkaribisha mtu yuleyule waliyekuwa wakimtangaza kuwa fisadi na hasafishiki, huenda kujiuzulu kulikuwa uamuzi wa busara.  Huenda alidhani kwamba hilo lingesaidia kuisafisha dhamiri yake na akaendelea kubaki kuwa mwanachama wa kawaida.

Wakati ule sikuwa na tatizo lolote na uamuzi wa Profesa Lipumba, licha ya kujiuliza tu maswali machache juu ya umuhimu wa yeye kama Mwenyekiti wa chama kuamua kutelekeza chama kipindi kama kile.  Nikajiuliza pia endapo ingekuwa busara zaidi angeamua kubaki kama mwenyekiti lakini kutojihusisha sana na kampeni, hadi kipindi cha uchaguzi kipite. Hata hivyo, nilimpongeza kwa kutoamua kuondoka kabisa chamani na badala yake kuamua kuwa mwanachama wa kawaida.

Lakini sasa kitendo chake cha kujirudi wiki iliyopita na kudai anautaka tena Uenyekiti, kimenifanya nipate maswali mengi mengine kuhusu dhamira yake ya kweli.

Kisa kilichomfanya Profesa Lipumba ajiuzulu Uenyekiti na kubaki kuwa mwanachama wa kawaida, kimetatuliwa?  Maana nadhani hakijatatuliwa.  Lowassa bado yupo Chadema, na Ukawa bado wapo naye na CUF bado ipo Chadema.  Profesa Lipumba akirejea kuwa mwenyekiti, ataishije na mambo hayo?

Lakini vilevile, kama chama kilimhitaji zaidi kipindi kile muhimu cha uchaguzi lakini yeye akakitelekeza, haoni pengine kuna athari zilizotokea kutokana na kujiuzulu kwake?  Huenda angewashauri na kuwaongoza CUF kushiriki uchaguzi wa marudio wa Zanzibar, au huenda angewaongoza wangepata kura nyingi zaidi hata kwenye uchaguzi wa Muungano.

Ninachojaribu kukisema hapa ni kwamba Profesa alikitelekeza chama kikiwa kinamhitaji sana.  Kwa sasa, hakuna maana ya yeye kurejea Uenyekiti, ili iweje?  Ndio maana nasema kwamba CUF ingemkubalia Lipumba, ningeshangaa sana.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here