Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amehimiza wanawake wajasiriamali Tanzania Bara na Visiwani kujiunga na majukwaa ya kuwezesha wanawake katika uchumi yatakayoanzishwa nchini kwa ajili ya kuwapatia elimu ya ujasiriamali.
Aliyasema hayo Dar es Salaam jana alipofungua mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo wanawake wajasiriamali yaliyoandaliwa na Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF) JKT Mgulani.
Alisema kama wanawake watayatumia majukwaa hayo ya uchumi watakuwa na uwezo wa kuzalisha bidhaa bora, kutafuta masoko, kupanga bei nzuri za bidhaa na kupata fursa za mikopo.
Makamu wa Rais aliwataka wanawake wajasiriamali kuichukulia ajira hiyo kama ajira yo yote rasmi kwa kuwa serikali itaweza tu kutimiza azma yake ya kupunguza ukosefu wa ajira kupitia sekta ya viwanda vidogo ambavyo vingi vinaendeshwa na wajasiriamali.
“Kupitia majukwaa niliyoyataja ya kumwezesha mwanamke katika uchumi nitajihidi kuhakikisha majukwaa haya yanatoa majibu ya changamoto zinazowakabili wanawake wajasiriamli na kuchangia ukuaji wa ajira, kuondoa umaskini na kuwezesha ujenzi wa taifa la viwanda,” alisema.
Mwenyekiti wa EOTF, Mama Anna Mkapa, alisema tangu Mfuko huo uanzishwe miaka 19 iliyopita umetoa mafunzo kwa zaidi ya wanawake wajasiriamali 30,000 na umewezesha wajasiriamali 14,500 kushiriki maonyesho ya Sabasaba ili kutangaza na kuuza bidhaa zao.
“Wanawake hawa wamejenga nyumba bora, kusomesha watoto, kulipia huduma za matibabu, shughuli za familia kutokana na mafanikio ya biashara zao zilizoborehwa na mafunzo hayo,” alisema Anna.
Mama Mkapa alimwahidi Makamu wa Rais kuwa mfuko huo utaendelea na jitihada zake za kutoa elimu kwa wanawake wajasiriamali na kuwawezesha kushiriki katika maonyesho ya biashara.