NA MWANDISHI WETU
KATIKA kukuza ubunifu, taasisi ya Perfect InfoTech International Limited (PII) kwa kushirikiana na Max Malipo imezindua huduma ya kudhibiti matukio ya uhalifu kwa kutumia simu za kiganjani.
Ubunifu huo utawezesha kutambua matukio ya wizi yanayofanyika majumbani, kwenye bajaji, magari na kwenye jenereta.
Mkurugenzi Mkuu wa PII, Amos Oyomba, alisema vifaa hivyo vikifungwa kwenye vyombo hivyo vinarekodi matukio yote na kutoa taarifa kupitia simu ya kiganjani.
Alisema lengo la kuzindua huduma hiyo ni kuhakikisha kwamba wananchi wanakuwa salama na mali zao pamoja na kuongeza ajira itakayoinua kipato kwa wananchi.
“Mfumo huo hufungwa ndani na nje ya nyumba, kwenye gari na utakuwa ukiona mazingira ya eneo lako lote moja kwa moja, kusikia sauti ya mazungumzo, kutunza taarifa zote kwenye ‘server’ yenye zaidi ya zaidi ya Gb 32.
Naye mkuu wa Kitengo cha Ubunifu na Ukuzaji biashara Kampuni ya Max Malipo, Magesa Wandwi, alisema kwa upande wa jenereta inatoa taarifa ya mafuta yaliyojazwa, yaliyotumika, uwiano wa saa ya kufanya kazi na mafuta yaliyotumika, ripoti kuhusu mafuta yatakapopungua, itatoa taarifa mafuta yakiibiwa, joto likizidi pia kutoa taarifa inapotaka kuzimika na kuwaka.