32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

‘Yanga ifanyie kazi nidhamu uwanjani’

6*Kadi huenda zikaigharimu kukosa wachezaji tegemeo

*Wakacha kambi ya Uturuki, kutua leo Dar

NA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM

WAWAKILISHI wa kimataifa klabu ya soka ya Yanga, wanaweza kujikuta katika wakati mgumu kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, kama watashindwa kufanyia kazi suala la nidhamu ndani ya uwanja.

Hatua hiyo inatokana na kitendo cha wachezaji watano wa timu hiyo, Donald Ngoma, Haruna Nyonzima, Simon Msuva, Amissi Tambwe, kupewa kadi za njano huku beki, Haji Mwinyi, akipewa  kadi nyekundu kwenye mchezo wa kwanza wa Kundi A uliochezwa juzi dhidi ya Mo Bejaia kwenye Uwanja wa Unite Maghrebine mijini, Bejaia, Algeria.

Hata hivyo, mchezo huo ulimalizika kwa Yanga kukubali kichapo cha 1-0, hivyo kuifanya timu hiyo kuanza vibaya hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Kaimu Mkurugenzi wa Mashindano Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jonas Kiwia, alisema kadi hizo za njano zinaweza kuiathiri timu kwenye mchezo ujao, ambapo Juni 28 mwaka huu timu hiyo itacheza na timu ya TP Mazembe, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

“Sina uhakika kama kuna adhabu nyingine ambayo klabu hiyo inaweza kupewa kutokana na kadi hizi, lakini ninavyofahamu inaweza kutokea kwa mchezaji mmoja mmoja kama kadi hizo zitaongezeka na kufikia mbili anaweza kukosa mchezo unaofuata.

“Kitendo hicho ambacho sababu yake ni utovu wa nidhamu uwanjani, kinaweza kuigharimu timu kwa kukosa wachezaji tegemeo kutokana na adhabu kama hiyo,” alisema Kiwia.

Naye Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro, alisema wamekubali matokeo ya mchezo huo na kuwatoa hofu mashabiki wake kwa kudai kwamba kufungwa katika mchezo huo si sababu ya wao kupoteza matumaini ya kufanya vema mbeleni.

“Tumekubaliana na matokeo sasa tunajipanga kuangalia wapi tulikosea, tumeanza robo fainali kwa kufungwa lakini hii isituvunje moyo kwani sisi tuna kawaida moja, huwa tukianza na kufungwa basi tunamalizia kwa ushindi, hivyo nawaambia mashabiki Yanga bado ipo kamili,” alisema.

Jerry alisema licha ya Yanga kufungwa katika mchezo huo, wachezaji walionyesha umahiri wa hali ya juu jambo alilosema kuwa hiyo imedhihirisha wazi kuwa timu hiyo kwa sasa ni moto wa kuotea mbali.

Katika hatua nyingine, Jerry alisema timu hiyo itawasili mapema leo ikitokea nchini Algeria na itaendelea na kambi hapa jijini Dar es Salaam badala ya kurudi tena Uturuki kama ilivyopangwa hapo awali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles