SERIKALI imesema walimu wote ambao hawaridhiki na mishahara yao ni bora watafute shughuli nyingine za kufanya.
Pamoja na hali hiyo, pia amepiga marufuku uchangishaji wa michango kwa wanafunzi.
Mbali na hilo, amesema ni marufuku kwa walimu kuwafungia nje watoto wanaochelewa na atakayekiuka agizo hilo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Salum Hapi, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yenye kaulimbiu ya ubakaji na ulawiti kwa mtoto vinazuilika chukua hatua kumlinda mtoto.
“Mwalimu yeyote ambaye haridhiki na mshahara wake aende kutafuta kazi nyingine kwani hatutamfumbia macho atakayewachangisha wazazi,” alisema Hapi.
Alisema watoto wanapofungiwa nje wanaweza kujiunga na makundi mabaya ikiwemo ya uvutaji wa bangi.
Alisisitiza kuwa mtoto aachwe asome hata kama amechelewa na baada ya kumaliza masomo anaweza kupewa adhabu hata ya kufanya usafi.
“Kwa njia ya kuwafungia nje tunaenda kutengeneza kizazi cha watoto wavuta bangi wanaojiunga na magenge mabaya ambao watahatarisha taifa letu,” alisema Hapi.
Aliwataka walimu hao kubuni adhabu ambazo hazina athari kwa mtoto kwani hatua kali zitachukuliwa kwa atakayebainika kumnyanyasa mtoto kwa kumfungia nje asiingie darasani.