PRITORIA, AFRIKA KUSINI
MWANARIADHA mlemavu wa Afrika Kusini, Oscar Pistorius, juzi alifikishwa mahakamani bila ya miguu yake bandia wakati wa kusikilizwa kwa kesi yake ya mauaji inayomkabili.
Mwanariadha huyo alisimama kizimbani kwa kutumia fimbo huku akiinamisha kichwa chake chini, wakati huo wakili wake, Barry Roux, akirejea kilichotokea usiku wa mauaji ya Reeva Steenkamp ambaye alikuwa mpenzi wake Pristorius.
Kifo hicho kilitokea mwaka 2012 siku ya sikukuu ya wapendanao, inadaiwa kwamba mwanariadha huyo alimshambulia kwa risasi mpenzi wake usiku akidhani mvamizi.
Hata hivyo, ndugu wa familia ya Reeva, Kim Martin, aliiambia mahakama hiyo kuwa mwanariadha huyo amekataa kuelezea namna mauaji hayo yalivyotokea.
Baba wa marehemu Reeva, amesema kwamba lazima Pistorius alipe fidia kwa familia hiyo kutokana na usumbufu uliojitokeza tangu kifo hicho.
Hata hivyo, Pistorius ameweka wazi kwamba, hana mpango wa kurudi kwenye mashindano yoyote ya kukimbia hata kama kesi yake itamalizika.