25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Wapinzani wamjibu Naibu Spika

Naibu Spika Dk. Tulia
Naibu Spika Dk. Tulia

KHAMIS MKOTYA, DODOMA na  Fredrick Katulanda, Mwanza

WABUNGE wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, wamebeza uamuzi uliofanywa na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson wa kusitisha posho zao na kusema hawakwenda bungeni kufuata malipo hayo.

Wamesema sasa ni wazi Dk. Tulia anaonekana kuchanganyikiwa kutokana na kufanya uamuzi unaopingana na kanuni za kudumu za Bunge.

Kutokana na hali hiyo, wamependekeza malipo ya posho za wabunge yalipwe kupitia kumbukumbu rasmi za Bunge (hansard) ili kuondoa malalamiko.

Kauli hiyo ilitolewa jana katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma na Mbunge wa Momba, David Silinde (Chadema), alipokuwa akizungumza na MTANZANIA.

“Kauli ya kusitishwa kwa posho za wabunge wa upinzani eti kwa sababu wanatoka kwenye Ukumbi wa Bunge ni ishara tosha kuwa kiongozi huyo hajatulia na anakurupuka.

“Lakini, aelewe kwamba uamuzi wake huo hautukatishi tamaa ya kuendelea na msimamo wetu dhidi yake.

“Nataka ieleweke kwamba sisi hatujasusia Bunge wala hatujasusia vikao vya Bunge, sisi tumemsusia Naibu Spika yeye kama yeye na ndiyo maana leo akikalia kile kiti mtu mwingine tunaingia bungeni wala hatutoki.

“Lakini pia Naibu Spika anatakiwa kuelewa kwamba sifa mojawapo ya mbunge kulipwa posho ni mbunge kusaini mahudhurio na si vinginevyo.

“Kwahiyo, Dk. Tulia anatakiwa kuelewa kwamba sisi tunafanya mambo kisomi hatukurupuki kama anavyofanya yeye. Tunaamini posho zetu tatalipwa kwa sababu kanuni na sheria za Bunge hazisemi sifa ya kulipwa posho ni kukaa bungeni muda wote.

“Kama wao wameacha kufuata utaratibu uliopo kikanuni wa kulipa posho, sisi tunapendekeza utaratibu wa aina hiyo hiyo, kwamba ni vema sasa wabunge walipwe kwa kutumia hansard.

“Kama wanataka wabunge wanaofanya kazi ndiyo walipwe, basi wabadili utaratibu ili malipo yazingatie mchango wa mbunge bungeni na si kwa kuingia na kukaa,” alisema Silinde ambaye ni katibu wa kambi hiyo.

Akitolea mfano, Silinde alisema wabunge wa CCM wapo zaidi ya 200, lakini wanaoingia bungeni hawazidi 150, na kwamba wanaochangia bungeni hawazidi 30 na wamekuwa wakijirudia rudia.

“Kama hansard itatumika kutambua nafasi ya wabunge, tunaamini hoja ya kulipana posho haiwezi kuwa na mashiko kama inavyosimamiwa na wabunge wa CCM na Naibu Spika.

“Lakini pamoja na kiburi cha Naibu Spika, tutaendelea kutafuta njia mbadala itakayotumika kutatua changamoto hiyo kwa njia ya amani,” alisema Silinde.

SUGU

Kwa upande wake, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema) maarufu kwa jina la Sugu, alisema jambo la kushangaza ni Naibu Spika kulazimisha kuongoza vikao kila siku bila kujali uwepo wa wenyeviti wa Bunge.

“Huyu Naibu Spika ni mbinafsi sana na anaona anatukomoa kumbe anawakomoa na wasaidizi wake kwani kila siku anataka aongoze yeye.

“Kuhusu hilo suala la posho, kwetu sisi posho si chochote si lolote, tutaendelea kufanya kazi tuliyotumwa na wananchi kwa kutetea masilahi yao na wala hatukufuata posho.

“Waendelee kutunyima posho waone kama tutatetereka. Haturudi nyuma kwani sababu hata katika Bunge Maalumu la Katiba kila mbunge aliacha shilingi milioni 30 kutokana na kusimamia masilahi ya taifa.

“Kwahiyo, hiyo posho ya shilingi 200,000 kwa siku si kitu kwetu. Sisi tuna ngozi ya kubeba hoja hii na tunaamini tutafanikiwa kwa sababu ina mashiko na haiwezekani mtu anaelekezwa mambo ya kufanya halafu sisi tumsikilize tu,” alisema Sugu.

Kwa mujibu wa Sugu, wabunge wa upinzani wamedhamiria kupigania demokrasia na kupinga udikteta, na kwamba hawatarudi nyuma kwani Tanzania si mali ya mtu mmoja kama baadhi ya watu wanavyofikiria.

Pamoja na hayo, mbunge huyo alisema Naibu Spika anapaswa kutumia busara katika kutatua matatizo ya wabunge badala ya kutumia nguvu kupambana na wabunge anaoona ni kikwazo kwake.

CHACHA

Naye Mbunge wa Serengeti, Marwa Chacha (Chadema), alisema uamuzi wa Naibu Spika ni wa kupotoka kwani anajichanganya mwenyewe.

“Wiki iliyopita alifanya uamuzi kutokana na mwongozo wa Dk. Mwakyembe akasema wabunge wanaotoka hawawezi kunyimwa posho na mshahara kwa kuwa malipo ya wabunge yapo kisheria.

“Jana (juzi) anatoa ‘judgment’ (hukumu) nyingine, kwamba amefuata uamuzi uliopita akaegemea maamuzi ya aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta kuhusu wabunge wa CUF.

“Hapa kuna tofauti, wabunge wa CUF walifukuzwa bungeni sisi hatukufukuzwa, tumetoka wenyewe na tumeazimia kususia vikao vyake, sasa anatulinganishaje na wabunge wa CUF?

“Sisi tunachotaka ni Bunge kuendeshwa kwa misingi ya haki na si vinginevyo, iwapo kiongozi huyo atabadilika hatuna nongwa, tutafanya naye kazi,” alisema Chacha.

MEISEYEK

Naye Mbunge wa Arumeru Magharibi, Gibson ole Meiseyek (Chadema), alisema posho kwake si jambo la msingi ila kipaumbele chake ni kuwatumikia wananchi waliomchagua.

“Kwangu posho si ‘issue’ (hoja), wajibu wangu ni kufanya kazi. Kwahiyo kama ni suala la kulipa posho au wasilipe, tutabaki na msimamo wetu wa kususia vikao vitakavyoongozwa na Naibu Spika,” alisema.

MBOWE

Naye Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amesema kamwe uamuzi huo hautawarudisha bungeni.

Akizungumza  MTANZANIA jijini Mwanza jana, Mbowe alisema iwapo Dk. Tulia na wabunge wa CCM wanadhani kuwafutia posho wapinzani kutawarudisha bungeni, wamekwama.

Alisema wapinzani hawalalamikii posho, bali wanataka Dk. Tulia aondolewe au kutosimamia vikao vya Bunge.

Mbowe alisema kukimbilia kuwakata posho kumedhihirisha kiwango cha juu kuwa CCM inaongozwa kwa rushwa na tamaa ya fedha na kuamini kimakosa kuwa wabunge wa vyama vya upinzani wapo bungeni kwa ajili ya tamaa ya fedha.

“Nimeshangazwa na uamuzi wa Naibu Spika, ndani ya siku tatu kwa jambo moja ametoa uamuzi unaotofautiana, kwanza alieleza kanuni haziruhusu kukatwa posho wabunge, jana anasema ameangalia kanuni zinaruhusu, iweje mtu mmoja ajipinge mwenyewe,” alisema.

Alisema Dk. Tulia anatambua wazi kutoka nje kwa wabunge wa upinzani kuna sababu maalumu.

“Naibu Spika akiondolewa hata kesho wabunge wa upinzani wataingia bungeni kama kawaida.

“Kama yupo makini na msimamo wake autoe kwa wabunge wa CCM ambao wamekuwa wakifika na kusaini, kisha hutoka nje kwa ajili ya shughuli zao binafsi au kushinda kwenye mgahawa wa Bunge.

“Naomba huyu Spika Tulia ajipe ujasiri, afanye utafiti yeye na CCM wake kwa kuangalia ni wabunge wangapi ambao hufika bungeni na kusaini kisha kuondoka kwenda kwenye shughuli zao,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles