25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mwinyi: Mabasi ya mwendo kasi ni uroda

Rais mstaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi na mkewe, mama Sitti Mwinyi, wakiwa ndani ya basi la mwendo kasi wakati walipofanya ziara ya kutembelea mradi huo jijini Dar es Salaam jana. Picha na Jumanne Juma.
Rais mstaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi na mkewe, mama Sitti Mwinyi, wakiwa ndani ya basi la mwendo kasi wakati walipofanya ziara ya kutembelea mradi huo jijini Dar es Salaam jana. Picha na Jumanne Juma.

NA EVANS MAGEGE, DAR ES SALAAM

RAIS mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, ameyasifia mabasi ya mwendo kasi yaliyopo Dar es Salaam na kusema ni uroda kuyapanda.

Alitoa kauli hiyo jana jijini hapa baada ya kuhitimisha ziara yake ya kukagua mradi wa mabasi hayo.

Mwinyi ambaye ni maarufu kwa jina la Mzee Ruksa, alianza ziara hiyo kwa kupanda basi la mwendo kasi katika eneo la Morocco, Kinondoni na kwenda hadi Gerezani Kariakoo. Baadaye alielekea Kivukoni ambako alihitimishia ziara yake hiyo.

Kwa mujibu wa Mwinyi, usafiri huo ni mzuri na mabasi husika yana mazingira bora yanayomfanya abiria afike katika eneo alilokusudia kwa wakati.

“Usafiri huu ni mkombozi kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kwani kwa muda mrefu wamekuwa wakipata shida ya usafiri unaosababishwa na msongamano wa magari katika maeneo ya mjini.

“Leo nimejionea ujuzi na uroda kama mnavyosema, kwa kweli nimefurahia mazingira ya mabasi haya kwa sababu ni bora na hayana usumbufu.

“Hata msongamano wa abiria kama ilivyokuwa zamani haupo, huu ni usafiri mzuri sana,” alisema Mwinyi.

Kutokana na hali hiyo, aliutaka uongozi wa mabasi hayo (DART), uangalie uwezekano wa kuleta mabasi yenye ghorofa ili kuwawezesha abiria kuburudishwa na mazingira ya Jiji la Dar es Salaam.

“Nadhani ni vema pia wakaleta mabasi ya ghorofa ambayo yapo wazi juu ili kuwapa nafasi abiria kutalii mji wetu huu,” alisema.

Katika hatua nyingine, aliwataka wananchi kuheshimu njia za mabasi hayo ili kuepusha ajali zisizokuwa za ulazima.

“Najua kuna changamoto mbalimbali kama ile ya kunyang’anyana abiria ambapo wenye daladala wanataka na bodaboda nao wanataka. Yote hayo ni sawa, lakini mabasi haya yanatakiwa kuachiwa uhuru katika njia zake ili yafanye kazi kama inavyotakiwa.

“Tumeona msongamano wa magari umepungua sasa, lakini nadhani kuwekwe mfumo maalumu ambao mwisho wa mabasi yaendayo kasi ndio uwe mwanzo wa usafiri binafsi,” alisema.

Wakati Mwinyi akisema hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa DART, David Mgwassa, alisema wananchi wameanza kuelimika juu ya matumizi ya barabara za mabasi yaendayo kasi.

Alisema mazingira hayo ya kuelimika yamesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza ajali zinazotokea katika maeneo hayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles