28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Ni bajeti ya tarakimu – Wananchi

NA WAANDISHI WETU

WANANCHI wilayani Kiteto mkoani Manyara wamesema bajeti yenye tija, ni ile inayoboresha maisha ya Watanzania na si inayoongeza tarakimu.

Mmoja wa wananchi hao, Paulo Gwacha alisema amesikiliza hotuba ya bajeti ya Serikali, lakini ana wasiwasi kama itaweza kuimarisha maisha ya mwananchi wa kijijini.

“Huwezi kujivunia bajeti iliyotengewa fedha nyingi wakati uwezekano wa kuitekeleza ni hafifu, kutokana na mfumko wa bei za bidhaa uliopo.

“Serikali inapaswa kuangalia maisha ya wananchi wa kawaida hasa vijijini ndipo iweze kusema kuwa maisha ya mtanzania yana hali gani,” alisema Gwacha.

Hassani Konki ambaye ni mwangalizi wa haki za binadamu wilayani hapa, alisema Serikali bado ina safari ndefu katika kutimiza majukumu yake kwa wananchi huku akitolea mfano kuadimika kwa sukari nchini ni kielelezo tosha kwamba hata bajeti inaweza isiwasaidie sana wananchi.

 

ARUSHA

Mhadhiri Mwandamizi wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Dk. Amani Laltlaika alipongeza bajeti hiyo akionyesha kuwapo kwa neema endapo itafanyiwa kazi.

“Mimi huwa ni ‘critical’ (mkosoaji) katika masuala mbalimbali yanayoendeshwa hovyo. Lakini kwa bajeti hii naona kuna dalili njema huko mbele,” alisema Dk. Laltlaika na kuongeza:

“Hii imeonekana kuwa bajeti ya kubana matumizi, ni bajeti ya vipaumbele vya msingi, kwa kiasi kikubwa imejielekeza katika miradi itakayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi wa kawaida.”
Diwani wa Kata ya Levolos, Efatha Nanyaro (Chadema) alisema kwamba bajeti hiyo imeshindwa kuakisi matarajio ya wananchi wa maisha ya kawaida.

“Sitarajii mambo mapya kutoka katika bajeti iliyosomwa bungeni, kwani vyanzo vya mapato havijaongezeka ni vile vile vya miaka yote,” alisema.

Nao baadhi ya wananchi waliozungumza na MTANZANIA mara baada ya bajeti hiyo kusomwa jana, walionyesha tofauti zao kutokana na baadhi kupongeza Serikali kwa kufanya marekebisho katika suala la sheria ya manunuzi ya umma.

Juma Mwinyi, mkazi wa Kaloleni jijini hapa, alisema eneo hilo la manunuzi ya umma limetumika kwa miaka mingi kufuja fedha za umma ikiwamo kuwa njia ya mafisadi kuchota fedha za walipakodi kwa kigezo cha kutumia sheria ya manunuzi.

NA MOHAMED HAMAD (KITETO), ELIYA MBONEA, ABRAHAM GWANDU NA JANETH MUSHI (ARUSHA)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles