25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Wabunge Ukawa wampinga naibu Spika kwa mabango

1NA AZIZA MASOUD, DODOMA

WABUNGE wa Kambi rasmi ya Upinzani bungeni jana kwa mara nyingine wametoka nje ya Ukumbi wa Bunge na kushindwa kusikiliza uwasilishwaji wa Bajeti Kuu ya Serikali kwa 2016/17 wakipinga kikao hicho kuendeshwa na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson.

Katika hali isiyo ya kawaida, jana wabunge hao wa Ukawa walikuwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali wa kumshutumu Dk. Tulia.

Mgomo huo ambao umeingia siku ya nane ni mwendelezo wa msimamo wao wa kususia vikao vyote vinavyoendesha na Naibu Spika ambapo wiki iliyopita  waliwasilisha hoja ya kutaka kumng’oa kwenye nafasi hiyo kwa madai kuwa hawatendei haki.

Kabla ya kutoka ndani ya ukumbi huo, wabunge hao walitumia staili mpya kwa kunyoosha juu karatasi nyeupe zenye ujumbe mbalimbali.

Baadhi ya ujumbe huo ulisomeka; ‘Bunge linaendeshwa na Serikali’, ‘Naibu Spika hufai hata kuwa Balozi wa nyumba kumi’, ‘Shut Up Opposition’, ‘Naibu Spika jiuzulu’, ‘Bunge linaloburuzwa haliwezi kusimamia Serikali’ na ‘Bunge kibogoyo Spika jiuzulu’.

Akitoa maoni yake katika viwanja vya Bunge, Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), alisema kitendo cha wapinzani kufungwa mdomo kupitia Naibu Spika wananchi wanapaswa kukifahamu, hivyo wanatafuta njia ya kufikishia suala hilo kwa jamii baada ya mikutano ya hadhara kuzuiwa.

“Hata kama wamekataza mikutano ya hadhara, tutatumia mfumo wa nyumba kwa nyumba kuwafikishia Watanzania wanyonge kile tulichokusudia kuwafikishia. Kama wanawapuuza wawakilishi wa wananchi je, Watanzania mmoja mmoja itakuwaje?” alihoji mbunge huyo.

Aidha Mbatia alisema hadi sasa hawaridhishwi na vitendo vinavyofanywa na Naibu Spika kwani vinadumaza demokrasia na kuondoa dhana nzima ya kuwapo kwa upinzani.

“Utaratibu unaotumiwa na mabunge yote ulimwenguni, hasa yale ya Jumuiya ya Madola ambayo Tanzania ni mwanachama, unaruhusu mijadala na maelewano baina ya upinzani na chama tawala, sasa hapa kwetu kuwa mpinzani kunamaanisha adui.

“Ukiona  wabunge zaidi ya 114 wanatoka nje ya Bunge, ujue kuna tatizo kubwa, hatuwezi tukakaa kimya wakati Katiba ambayo ndiyo sauti ya watu na wanyonge inakanyagwa, tutasema popote, tutasimamia sauti hizo za Watanzania zinazopuuzwa hadi zisikilizwe,” alisema Mbatia.
Mbunge wa Mbozi, David Silinde (Chadema) alisema kitendo cha wabunge hao kutoka nje hakumaanishi kuwa wamesusia bajeti, isipokuwa ni kuendeleza msimamo wa kutomtambua Dk. Tulia.

“Watanzania waelewe hatujasusia bajeti, hatuwezi kuongozwa na Naibu Spika, tulishakataa, Kambi rasmi ya upinzani tutaiwasilisha hotuba yetu Ijumaa (kesho),” alisema Silinde.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles