25.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Rushwa kikwazo kwa wawekezaji wazawa   

majaliwaDHAMBI ya kuona kuwa Watanzania hawataweza na kuamini kuwa wanaotoka nje ndio wanaweza kama ambavyo Rais John Pombe Magufuli alivyobainisha hivi karibuni kuwa ndio kanuni ambayo imekuwa ikitumiwa na wapanga sera na wafanya Uamuzi na hilo halina ubishi.

Ukichokonoa  katika mtazamo wa kina licha ya Rais kusema kuna kuoneana wivu katika masuala ya uwekezaji upande wa pili wa shilingi unaonesha kuwa kukwama kwa wazawa kupata fursa au kupewa kipaumbele kunasababishwa na rushwa.

Ukweli unabakia kuwa hakuna mwekezaji mzawa atakayekubali kutoa rushwa ya kiwango kinachotolewa na wawekezaji kutoka nje na kwa kasumba ya kuoneana wivu mpokeaji atataja kiwango cha kukatisha tamaa.

Mazingira ya aina hiyo yanaonesha kuwa ile kanuni mahiri ya ‘Rushwa ni adui wa haki sitapokea wala kutoa rushwa’  imekuwa haiwasuti wala kuwakeresha tena wapanga sera na Uamuzi, zaidi ya kuukumbatia uliberali kwa kujineemesha na kusahau maslahi mapana ya jamii ambayo inaundwa na wavuja jasho.

Lakini katika kuthibitisha kuwa rushwa ndio inayokwamisha wazawa katika kupata fursa za kuwekeza  Benki ya Dunia imeliweka hilo wazi katika tafiti ambazo imekuwa ikifanya na kuchapisha ripoti jinsi hali ya biashara  katika nchi mbalimbali imekuwa ikiathiri uwekezaji.

Tafiti hizo zimekuwa zikifanywa kwa kuwapeleka watafiti katika nchi kadhaa duniani ambao huzungumza na  watu mbalimbali  hususani wawakilishi wa kampuni za biashara  kuhusu vikwazo wanavyopata katika kuwekeza vitega uchumi katika nchi husika.

Mwaka 2006 kwenye utafiti wake zaidi ya kampuni 67,000 katika nchi tofauti 103  zilizohojiwa  kujua maoni yao kuhusu hali ya uwekezaji katika nchi husika.

Kwa Tanzania mwaka 2006 utafiti huo ulihusisha kampuni 419 zilizohojiwa ili kubaini  mtazamo wao kuhusu hali ya uwekezaji na biashara kwa jumla hapa nchini. Kabla ya utafiti huo wa mwaka 2006 utafiti mwingine kama huo ulifanyika mwaka 2003.

Tafiti hizo za Benki ya Dunia huwa ni muhimu kwa sababu zinasaidia kampuni na wawekezaji duniani kwa jumla kufanya tathmini na uamuzi pale wanapotaka kwenda kuwekeza katika nchi za nje.

Kigezo kimojawapo kinachotazamwa katika tafiti hizo ni suala zima la rushwa. Kampuni zinazohojiwa huulizwa kama wanalazimika kutoa rushwa ili kupata vibali vya kufanya biashara ama kuwekeza katika nchi fulani. Vile vile huulizwa kiwango cha rushwa wanachotoa ili kuruhusiwa kuwekeza.

Kilichojitokeza ni kwamba kampuni nyingi zilidai kuwa zimekuwa zinatoa rushwa ili kuruhusiwa kuwekeza katika miradi mikubwa ya Serikali nchini Tanzania.

Malipo hayo ni yale yasiyokuwa rasmi na hayaingii kwenye kumbukumbu za Serikali kwa mfano pale mwekezaji anapopaswa kutoa zawadi ama kiasi fulani cha fedha kwa kiongozi fulani wa Serikali ili amsaidie kufanikisha azma yake ya kuwekeza. Vile vile pale ambapo  wawekezaji wanalazimika kutoa chochote ama waweze kupata misamaha ya kodi au kupunguziwa kodi.

Wawekezaji wengine wanadai kuwa kila wanapokutana na wakaguzi wa kodi huwapa chochote ili mahitaji yao ya uwekezaji yaweze kutekelezwa kama walivyotarajia.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo Benki ya Dunia kiwango cha rushwa kinachotegemewa kutolewa ili kupata uwekezaji katika miradi ilikuwa ni asilimia 2.94 mwaka 2006 na kwa jumla wawekezaji walikuwa wakitarajia  kutoa kiasi cha asilimia 2.7 ya mradi kama rushwa na malipo mengine yasiyokuwa rasmi ili mambo yaweze kuwanyookea.

Hiki kiwango cha asilimia 2.7 kilikuwa juu ya wastani  wa rushwa kama hiyo katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambayo ilikadiriwa kufikia asilimia 2.14 ya mradi.

Wakati wa utafiti kama huo uliofanyika mwaka 2003 kampuni zilidai kuwa kiasi cha rushwa walichokuwa wakitoa ili mambo yao yaweze kwenda vizuri kilikuwa ni asilimia 2.90 ya mradi. Hii ilikuwa chini ya kidogo ya asilimia 2.94 iliyoripotiwa mwaka 2006.

Mambo mengi yamezungumziwa kwenye utafiti huo. Jambo la msingi ni kwamba wahusika kwenye Serikali waliobahatika kuipitia ripoti hiyo wanaweza kuwa na majibu kuhusu yaliyoelezwa ndani yake.

Hata hivyo jambo la msingi zaidi ni kwamba hatua za kurekebisha hali hiyo ni lazima zichukuliwe kwa kurekebisha kasoro mbalimbali zilizoripotiwa kwenye taarifa hiyo hususani kwenye madai kuwa wawekezaji wanatoa rushwa, zawadi au malipo mengine yasiyokuwa rasmi ili waweze kufikiriwa kupewa uwekezaji kwenye miradi mikubwa ya Serikali.

Tangu ripoti hiyo ichapishwe hayajawahi kuwapo matamshi ya Serikali hususani kitengo kinachohusika na uwekezaji iwapo mambo yaliyoripotiwa ndani ya ripoti hiyo yalikuwa na ukweli ndani yake au la?

Hoja nyingine ni kwamba katika mazingira ya aina hiyo bado wawekezaji wanalazimika kutoa kitu kidogo ili wakubaliwe kuingia kwenye miradi mikubwa na hata midogo hapa nchini?

Jambo la kuzingatia hapa ni kwamba utafiti huo wa Benki ya Dunia ulihusisha maoni ya wawekezaji na kampuni ambazo tayari zinafanya shughuli zake hapa nchini. Katika mazingira hayo ni kwamba inaweza kuchukuliwa kuwa yale waliyoyasema walikuwa na uhakika nayo kwa kuwa walikuwa tayari wameshapitia mkondo huo.

Pamoja na hali hiyo sio kwamba kila kitu kilichopo kwenye utafiti kama huo kinaweza kuwa ni kibaya. Kwa mfano kwenye  upande wa usalama wa wawekezaji Tanzania wanaona kuna unafuu ikilinganishwa na nchi nyingine zilizofanyiwa utafiti.

Gharama za wawekezaji zinazotokana na wizi, unyang’anyi, hujuma, majanga ya moto  na kadhalika ziliripotiwa kupungua sana kwa Tanzania mwaka 2006 ikilinganishwa na hali ilivyokuwa miaka minne iliyopita.

Mwaka 2006  gharama hizo zilikuwa ni asilimia 0.47 ya mauzo, ikilinganishwa na asilimia 1.94  mwaka 2003. Pamoja na hayo usalama kwa wawekezaji, ikilinganishwa na asilimia ya  mauzo, ilikuwa ni asilimia  2.71  mwaka 2006 wakati mwaka 2003 ilikuwa ni asilimia 2.29 ikionyesha kuwa  kulikuwapo na kudorora kwa usalama.

Kwa hiyo pamoja na mambo machache mazuri ambayo Tanzania  kwa ujumla imepata  alama nzuri  bado yapo mambo mengi ambayo yanastahili kurekebishwa ili kukidhi malalamiko ya wawekezaji.

Kwa mfano wafanyabiashara na wawekezaji bado wanalalamika kuwa inawachukulia siku  nyingi zaidi kuondoa bidhaa kutoa bandari za Tanzania ikilinganishwa na nchi jirani.

Katika dhana nzima ya utafiti huo ni kwamba suala la msingi ni matokeo yake yasipuuzwe bali mara kwa mara yanatakiwa kufanyiwa kazi na kubaini wahusika.

Hali kadhalika ingefaa taasisi zinazohusika na uwekezaji ziwe zinatoa maoni kuhusu ripoti kama hiyo kwani moja kwa moja inaathiri taswira ya nchi kwenye macho ya wawekezaji wa nje.

Tafiti hizi zimekuwa zikifanyika kila baada ya miaka kadhaa  hivyo kutoa mwanya kwa nchi kujirekebisha au kufanya masahihisho na kujipima  na kujilinganisha na nchi nyingine.

Ukweli unabaki kuwa rushwa ndio imekuwa inawakwamisha wazawa katika kuwekeza na hilo lilijionesha kuanzia wakati wa kubinafsisha zilizokuwa kampuni na mashirika ya umma na matokeo yake walioyanunua  hawakuwa na uzalendo  yakaishia kubadilishwa shughuli na au vipuri vilivyokuwa katika baadhi ya viwanda kuuzwa kama chuma chakavu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles