32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Thomas Mwakijege: Mganga wa kienyeji amenisababishia upofu

PC 3.Na Eliud Ngondo, Mbeya

HUJAFA hujaumbika, ndivyo ninavyoweza kusema kutokana na
kisa cha kijana Thomas Mwakijege (25) kupata upofu baada ya kudaiwa kuingiwa na mdudu machoni.

Mwakijenge ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Lupembe wilayani Kyela mkoani Mbeya, alipatwa na mkasa huo katika jicho lake la kulia wakati alipokuwa katika mihangaiko ya kujipatia riziki.

Ambapo alikuwa akifanya kazi ya kuendesha bodaboda katika mpaka wa Kasumulu unaotenganisha Tanzania na Malawi.

Anasema siku moja akiwa katika shughuli zake aliingiwa na mdudu katika jicho lake la kulia na kusababisha apate maumivu makali.

Anasema baada ya kupatwa na hali hiyo aliondoka na kurejea nyumbani ambako alimkuta mke wake na kumsimulia yaliyomkuta.

“Baada ya kuingiwa na mdudu nilijaribu kumtoa kwa kunawa macho lakini hali ilizidi kuwa mbaya zaidi ya matarajio yangu.

“Hivyo nilichukua uamuzi wa kwenda katika Hospitali ya Wilaya Kyela kupatiwa matibabu lakini jicho liliendelea kuniuma bila mafanikio yoyote,” anasema Mwakijenge.

Anasema alipofika katika hospitali hiyo alionana na daktari wa macho kisha kupatiwa dawa ambazo alizitumia kwa muda wa siku tatu.
“Daktari aliniambia kuwa mdudu huyo aliyeniingia alikuwa ameshakula ndani ya jicho na kusababisha kidonda kwa ndani kilichopelekea jicho kutoona,” anasema.

Kijana huyo anasema baada ya kumaliza dawa alirudi tena hospitalini na kuambiwa aende katika Hospitali ya Rufaa mkoani Mbeya kufanyiwa uchunguzi zaidi.

Kijana huyo anasema alilazwa katika Hospitali ya Rufaa kwa mwezi mmoja bila mafanikio na hivyo kuamua kuomba kuondoka nyumbani.

“Niliporudi nyumbani nilikwenda kutibiwa kwenye tiba za asili (kwa mganga wa kienyeji),” anasema.

Anasema mganga huyo alianza kumtibu kwa kutumia miti shamba na hali iliendelea kuwa mbaya zaidi huku akipewa matumaini kuwa tatizo hilo litaisha.

“Baada ya kuona jicho langu linazidi kuziba kwa kutoona nilimwuliza yule mganga akanijibu kuwa yeye ndiyo ameamua kulifunga kutokana na kuona wachawi wanalichezea lakini atalifungua baadae nitakapokuwa nimekamilisha tiba yake.

“Niliendelea kukaa kwa mganga huyo kwa kuamini kuwa nitapona na
baada ya siku chache tena jicho la pili likafunga. Nilipomuuliza aliniambia kuwa ni yeye ameamua kuyafunga yote kutokana na wachawi kuendelea kuyachezea,” anasema Mwakijenge.

Kijana huyo aliendelea kutiwa imani na mganga huyo kuwa atayafungua macho yake mara baada ya wachawi kuacha kuyatumia kwa nguvu za giza na kurudi katika hali yake ya kawaida ya kuona.
Baada ya kukaa kwa muda wa miezi saba bila mafanikio yoyote kijana huyo aliamua kuondoka kwa mganga huyo.

Anasema aliendelea kuzunguka kwa waganga mbalimbali kupata msaada wa matibabu bila mafanikio yeyote.

Mwakijege anasema tatizo hilo limedumu kwa mwaka mmoja na miezi tisa sasa huku maisha yake ykiendelea kuwa mabaya zaidi kutokana na kuwa tegemezi katika familia.

“Naomba Watanzania wenzangu mnisaidie niweze kupata fedha za matibabu,”anasema Mwakijege.

Macho ya kijana huyo sasa yamebadilika na kuwa rangi ya kijivu japokuwa yanacheza kama kawaida ya macho yote.

MKEWE

Mpewa Mwakasola (23), anasema tangu mumewe apatwe na tatizo hilo hali imekuwa mbaya kwa sababu ndiye alikuwa tegemeo katika familia hiyo na kwa upande wa wazazi.

Anasema sasa amekuwa akihangaika na majukumu ya kulea mtoto mwenye umri wa miaka miwili ambaye hatembei, pamoja na mume ambaye amekuwa kipofu.

KISA CHA MTOTO

Mama huyo anasema mtoto wao huyo tangu amezaliwa hajawahi kunyonya maziwa na hadi sasa ameshindwa kukaa, kusimama na hata kutembea.

Anasema alipompeleka katika Hospitali ya Wilaya aliambiwa kuwa mtoto huyo ana tatizo la shingo na kushindwa kupata fedha za kuweza kumtibu hadi sasa.

“Naiomba serikali, wananchi wote, wadau mbalimbali, taasisi za kiserikali na zisizokuwa za kiserikali zinisaidie ili mume na mtoto wangu waweze kupata matibabu,” anasema kwa uchungu.

MKUU WA WILAYA

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Dk. Thea Ntara, anasema kijana huyo aliwahi kufika ofisini kwake kuomba msaada.
“Kwa maelezo ya huyo kijana anasema alivyokwenda kupima katika Hospitali ya Rufaa Mbeya aliambiwa macho yake hayawezi kupona kwa hapa Mbeya vinginevyo akatibiwe nje ya nchi kama vile India.

“Hivyo nilimwagiza mkuu wa kituo cha Polisi wilayani humo kuhakikisha anamkamata mganga huyo wa kienyeji (jina linahifadhiwa) ili kufikishwa mahakamani,” anasema Ntara.

Anasema alipofuatilia juu ya mganga huyo alitaarifiwa kuwa amekuwa ni tapeli wa muda mrefu na amewaumiza wananchi wengi.

“Wilaya ya Kyela ina waganga wengi wa jadi na wengine ni matapeli, wadanganyifu waliokaa kwa lengo la kupata fedha tu na hakuna chochote wanachosaidia wananchi,” anasema Dk. Ntara.

Dk. Ntara ameshauri watu wenye mapenzi mema, taasisi za kiserikali na
zisizo za kiserikali, wadau mbalimbali kuweza kumsaidia kijana huyo aweze kupona na kurejea katika hali yake ya kawaida.
MGANGA MKUU

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo ya Wilaya, Dk. Hashim Mvogogo, anasema kijana huyo alifika katika hospitali hiyo na kwenda kupatiwa matibabu katika kitengo cha macho.

Anasema baada ya kuona hali bado haijatengamaa mganga wa kitengo hicho alimhamisha kwenda katika Hospitali ya Rufaa mkoani Mbeya ili kupata vipimo na kuweza kuendelea na matibabu zaidi.

“Baada ya kupimwa ilionekana kuwa mdudu aliyekuwa amemwingia alikuwa amemsababishia kidonda ambacho kilitengeneza kovu kwa ndani, hivyo alipatiwa dawa ambazo alizitumia kwa siku 14 na aliambiwa arudi tena. Aliporudi akapewa tena dawa na alipoona hakuna maendeleo akaamua kutumia dawa za kienyeji.

“Suala la kupona inawezekana kama atapelekwa kwa watalaamu wa juu, tulimpiga picha na tumeipeleka wizarani ili kuweza kutambua ni jinsi gani anaweza kusaidiwa,” anasema Dk. Mvogogo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles