AZIZA MASOUD NA JAFARI JUMA (TSJ), DAR ES SALAAM
BAADHI ya wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF) ambao walikuwa wakiwania nafasi ya Ujumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la chama hicho, wamelazimika kuingia katika vyumba vya kuhesabia kura kwa hofu ya kuchakachuliwa kura zao.
Wabunge hao walikesha usiku kucha wakihesabu kura wenyewe badala ya kuweka mawakala kama walivyofanya baadhi ya wagombea katika nafasi hiyo.
Chanzo cha kuaminika kiliiambia MTANZANIA Jumamosi kwamba wakati wakijieleza, wabunge hao walikuwa wakifanyiwa kampeni chafu na baadhi ya wajumbe kutoka Zanzibar, wakidai kuwa wamekuwa hawakisaidii chama.
Wabunge hao (majina tunayo), walikuwa wakihaha kutafuta kuungwa mkono ndani ya chumba cha kuhesabia kura na hata kufikia kutoa onyo la kura zao kutochezewa.
“Kilichotokea wakati wakijinadi kuomba kura wabunge wa Bara walikuwa katika wakati mgumu kutokana na swali kubwa kuulizwa kwanini hawakichangii chama, licha ya posho wanazopata kila wanapokuwa katika vikao vya Bunge na wakawa hawana majibu sahihi ambayo wajumbe waliridhika nayo.
“Na baada ya wao kuona hali imekuwa ngumu wakaona ni vema waingie wawe mawakala wenyewe wa kuhesabu kura zao ili kuzuia hujuma dhidi yao,” alisema mmoja wa wajumbe ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
MTANZANIA ilifanikiwa kupata baadhi ya matokeo ambapo baadhi ya wajumbe waliofanikiwa kuingia katika Baraza Kuu ni pamoja na Katibu wa Jumuiya ya Wanawake CUF Taifa, Nuru Bafadhili na Masoud Mhina, Mkiwa Kimwanga na Jeremia Karume kutoka Mkoa wa Mara pamoja na Moza Abeid.