Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
BARAZA Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Tanga limesema kuwa matukio ya mauaji yaliyotokea Tanga hayahusiani na Uislam kwa vile vitendo hivyo ni kinyume na imani ya dini hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Sheikh wa Mkoa wa Tanga, Ali Jumaa Liwuchu aliomba serikali kuhakikisha wahusika wanachukuliwa kama wahalifu wengine.
Sheikh Liwuchu alikanusha uislam kuhusishwa na matukio hayo akisema dini hiyo haielekezi uovu bali Imani na amani katika jamii.
Sheikh Liwuchu ambaye ni mwenyekiti wa baraza la amani Mkoa wa Tanga, alilaani matukio hayo na watakaobainika wahesabiwe kama wakosaji wengine na hakuna dini ya Mungu yenye uhusiano na
uhalifu.
Alisema matukio hayo yanatisha na kutaka wadau wa amani kuisaidia serikali kuangalia namna bora ya kukabiliana na uhalifu huo ambao unalichafua taifa hili.
Shekh Liwuchu alichukua nafasi hiyo kuwapa pole ndugu, jamaa na marafiki waliopatwa na msiba huo mzito na kuwataka wanaTanga na Tanzania kwa ujumla kuwa wavumilivu wakati serikali ikishughulikia matukio hayo.