NA MWANDISHI WETU, Dar es Salaam
KIONGOZI wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amesema Rais John Magufuli amejitoa mhanga kupambana na ufisadi, lakini wapinzani watalazimika kujitoa mhanga kulinda demokrasia inayoelekea kupotezwa na viongozi waliopo madarakani.
Akihutubia mkutano wa hadhara Dar es Salaam jana, Zitto alisema nchi inaweza kuingia katika madhara makubwa kama wapinzania hawatasimama kidete dhidi ya mbinu za kufifisha demokrasia na misingi ya uwajibikaji nchini.
Katika mkutano huo, Zitto vilevile alizungumzia kusimamishwa kazi za Bunge, suala la Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Zanzibar, mwelekeo wa Bajeti na tishio la nchi kuelekea kwenye utawala wa imla wa mtu mmoja.
“Ni imani yetu kuwa ufisadi utapigwa vita kwa ukamilifu siyo kwa kutegemea nia ya mtu mmoja bali kuboresha na kutumia misingi ya demokrasia kwa kujenga taasisi madhubuti zitakazomaliza janga la ufisadi bila ya kutegemea nia ya rais pekee,”alisema Zitto.
Huku akishangiliwa, kiongozi huyo wa ACT alisema baada ya uchaguzi, viongozi wapya wamekuwa wakichukua hatua mbalimbali nzuri na mbaya zikiwamo kubomoa demokrasia.
“Tumeshuhudia uamuzi mwingine ambao unatia hofu, ingawa tunaona dhamira ya dhati ya kupambana na ufisadi, lakini pia tunaona mbinu za chini chini za kutokomeza demokrasia ya nchi yetu ambayo tumeijenga kwa jasho na damu.
Wabunge kusimamishwa
Alisema Mei 30 mwaka huu, Bunge likiongozwa na Naibu Spika lilipitisha Azimio la kuwasimamisha wabunge wa upinzani, Esther Bulaya, Tundu Lissu, Halima Mdee, Pauline Gekul, Godbless Lema, John Heche na yeye Zitto.
“Mimi binafsi pamoja na wabunge wengine sita hatukufanya fujo yoyote ndani ya Bunge, kosa letu kubwa ni kutaka kuhoji uamuzi wa Serikali kuzuia kuonyeshwa live matangazo ya Bunge.
UDOM:
Alisema wanafunzi 7,800 waliofukuzwa Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM) wanasomea programu maalumu ya ualimu wa sayansi ni watoto wa masikini waliokubali kuacha kwenda kidato cha tano na sita ili wakawafundishe watoto wa masikini wenzao.
Alisema wanafunzi hao hawakuanzisha programu hiyo bali Serikali kupitia Baraza la Mawaziri ambalo Rais Magufuli alikuwa mjumbe, kwa mujibu wa kumbukumbu za Baraza la Mawaziri.
“Rais Magufuli hakupinga mpango huu na aliubariki kama wenzao walivyofanya na kuanza kutekelezwa, Tanzania ina uhaba wa walimu wa sayansi 26,000 na tukienda kwa utaratibu wa kawaida tutahitaji miaka 20 kuziba pengo hilo.
“Rais Magufuli anafikia kuita watoto vilaza? Rais huyu anayesema yeye ni Rais wa masikini anaita watoto wa masikini vilaza?
“Rais sifa zimempanda kichwani, hana budi kuwaomba radhi vijana hawa na wazazi wao. Rais ni Mwalimu, anajua madhara ya saikolojia kwa maneno aliyoyasema. Ni sawa na jenerali wa jeshi anayetukana askari wake walio mstari wa mbele. Hata Baba wa Taifa hakuthubutu kamwe kuita wanafunzi vilaza hata kama walimuudhi kiasi gani.
“Rais Magufuli anazungumza mno… Rais ajue kuweka akiba ya maneno. Yeye ni kiongozi wa wote, wenye akili na vilaza, anapaswa kuwa wa mwisho kuzungumza ili watu waweze kukata rufaa kwake, sasa akishazungumza wananchi waende kwa nani?”alihoji Zitto.
ZANZIBAR
Zitto pia alilaani kauli ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk. Ali Mohamed Shein kutamka kuwa hamwogopi Maalim Seif kwa sababu hana vifaru na mizinga, akiita ya kutisha.
“Kamwe huwezi kuzima haki za wananchi kwa vifaru na mizinga. Dk. Shein akumbuke kuwa Sultan alikuwa na jeshi, vifaru na mizinga na ulinzi wa dola kubwa kama Uingereza lakini aliangushwa na wananchi wa Zanzibar mwaka 1964.