25.7 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Mnaweza kuoana dini tofauti?

happy-coupleVIJANA wengi wamekuwa wakiwasiliana nami wakiuliza sana kuhusu uhalali wa kuoana katika imani za dini tofauti. Ni jambo lenye changamoto kubwa sana na limesabisha migogoro mara nyingi kwenye uhusiano wa vijana wengi.

Kutokana na uzito wake nimeona ni vyema niandike hapa mada, yenye mwendelezo zaidi kuhusu pia suala la kabila na mila.
Je, ni vitu vya msingi kuangalia kabla ya kuoana? Watu wanaweza kuwa na mitazamo tofauti, lakini hapa nitakupa hoja za kitaalamu zaidi.

SUALA LA DINI

Inasemwa sana kuwa, mapenzi hayachagui dini, kabila, rangi wala kitu kingine chochote cha kufananisha. Inaweza kuwa sawa, lakini wakati mwingine siyo sawa hususani kwenye suala la imani ya dini.
Imani ni msingi wa maisha ya binadamu. Ni kile unachokiamini kimapokeo ambacho ni mwongozo sahihi wa maisha yako ya baadaye.
Wakati mwingine mtu anaweza kubadili imani yake baada ya kuwa mtu mzima na huenda akapata mafundisho mapya ambayo yatamvutia na kuona ndiyo njia sahihi ya mwongozo wa safari yake hapa duniani.
Mwongozo huo ndiyo msingi. Kwa maneno mengine, kwa sababu kila dini ina msingi wa imani yake, ina miiko na taratibu zake, hutokea baadhi ya makatazo ya upande mmoja, upande wa pili ikawa halalisho.
Ni sahihi zaidi kuoana mkiwa katika imani moja ya dini, tena mnaoabudu katika tawi moja – ni nzuri zaidi. Hii itasaidia wote kuwa na mafundisho yanayofanana – hofu zinazofanana juu ya taratibu za maisha (ya ndoa) kwa utashi wa dini.

 

NI SAHIHI KUOANA DINI TOFAUTI?

Kisheria inakubalika. Pamoja na kukubalika huko, kama nilivyozungumza katika kipengele kilichopita ni rahisi kusababisha msuguano na kushindwa kupata utatuzi mzuri wa kiimani hasa kwa sababu imani ndiyo kimbilio na msingi wa kwanza katika maisha ya binadamu.
Wengi ni mashahidi juu ya ndoa za Kiserikali, hazina uhakika wa kudumu. Mnaoana leo, ukiona mwenzako huelewani naye baada ya wiki moja inaweza kubatilishwa na talaka kutolewa mara moja.
Hii ni tofauti na zile za imani za dini, maana kabla ya kufikiria suala la talaka kuna njia za mazungumzo – mafundisho na ushauri wa kiimani zaidi.
Imani nyingi zinasisitiza suala la upendo na kusamehe, wakati kwenye sheria huangalia kwenye matatizo na matakwa ya ninyi mnaoamua kutengana!
NI SAHIHI KUBADILI DINI KWA SABABU YA NDOA?

Hili limekuwa likizua migogoro mara nyingi sana kwenye uhusiano wa vijana wengi. Wameanza uhusiano bila kugusia kabisa suala la dini. Baada ya kuzoeana na kila mmoja kuridhishwa na mwenzake, wanakuja kugundua kuna kikwazo cha dini.
Hapa huanza kushawishiana mmoja wao (hasa msichana) kugeukia dini yake mwenzake ili waweze kufunga ndoa. Kiukweli si sahihi na kuna athari nyingi ambazo mtu anaweza kuzipata kwa kubadilisha imani yake ili aoe/aolewe.

 

KWANINI USIBADILI KAMA UMEMPENDA?

Hapa kwenye kubadili dini huwa na changamoto nyingi sana. Kwanza kunaweza kusababisha mgongano wa wazazi na mtoto – wakati mwingine hufikia hatua ya kutishia kulaaniwa.
Ndugu zangu, hatupaswi kuchanganya vitu viwili kwa wakati mmoja. Upendo unabaki kuwa upendo na dini inabaki kuwa dini. Kubadilisha dini hakumaanishi unavyompenda mwenzako bali kunadhihirisha usivyo na msimamo na maisha yako.
Imani ya dini ndiyo dira, kubabaika ndani yake maana yake hata kwenye mapenzi utakuwa unakokotwa tu! Kuwa na msimamo. Simamia unachokiamini.
Kama ulibadili dini kwa sababu ya imani (kuamini mwenyewe baada ya kuona inafaa) kabla hamjakutana na ukaamua kuoana naye ni sawa na si kubadilisha dini ili uingie kwenye ndoa.

NDOA YA MSETO

Siku hizi kuna utaratibu wa ndoa za mseto; baadhi ya madhehebu yanaruhusu maharusi waoane chini ya msimamo wa imani yao hata kama kila mmoja anaabudu kwake. Kisheria halina tatizo hasa kwa kuwa suala la ndoa ni la kisheria zaidi.
Tunaporudi katika utaratibu wa maisha ya kawaida ndipo tunapokutana na matatizo. Yapo matatizo mengi ambayo yanaweza kutokea kwa kuishi wanandoa wawili huku kila mmoja na imani yake.
Nilieleza kwa uchache sana hapo juu, lakini katika kipengele hiki nitafafanua zaidi katika mwendelezo wa mada hii wiki ijayo, USIKOSE!

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. nimefurahishwa na mada yako ya ndoa mseto uliyoandika tar 4 june 2016, sasa nilijaribu kutafuta mwendelezo nimeshindwa kuupata, je unaweza kunitumia au kunisaidia kupata mwendelezo wa mada hiyo ambayo ulisema itaendela wiki lililofuata, kama inawezekana naomba unitafute kwa 0754839310. kuna vitu zaidi nahitaji toka kwako

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles