APRIL 28, 2016 ni siku ambayo Shule ya Wasichana ya Bwiru iliyoko Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza ilifanya mahafali ya kuwaaga wanafunzi wa Kidato cha Sita baada ya safari ndefu ya masomo.
Akisoma risala kwa mgeni rasmi, Makamu Mkuu wa Shule, Mark Paul alisema tangu kuanzishwa kwa shule hii mwaka 1952 mpaka sasa kuna mafanikio mengi yaliyopatikana kama vile ongezeko la wanafunzi na ufaulu wao.
Penye mafanikio hapakosi changamoto ndivyo ilivyo kwa Shule ya Wasichana ya Bwiru. Makamu Mkuu huyo katika risala yake aliendelea kusema baada ya kuona usalama wa shule ni mdogo, uongozi wa shule pamoja na bodi yake waliamua kuchukua hatua madhubuti.
Hatua zilizochukuliwa ili kuweka usalama katika eneo hilo  ni kuingia mkataba na kampuni ya ulinzi ya ‘Mara Security Company Ltd’ ambayo walinzi wake hulipwa kwa michango inayotokana na wazazi.
Kitendo cha uongozi wa shule kutafuta suluhisho la usalama kinastahili pongezi lakini swali la kujiuliza ni Je, hawa walinzi wa kampuni binafsi wanayo mafunzo ya kutosha ili kukabiliana na uhalifu uliokomaa kutokana na nguvu ya Sayansi na Teknolojia?
Inawezekana walinzi wakawa na mafunzo ya kutosha kwa maana ya kwamba pengine wamepitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) au baadhi yao ni wastaafu wa vyombo vya ulinzi na usalama kama vile JWTZ, Polisi, Magereza nakadhalika. Lakini cha kujiuliza wanapatiwa zana za kisasa ili kuupiku uhalifu mamboleo?
Hatuombei mabaya yatokee katika Taifa letu lakini ikumbukwe Tanzania siyo kisiwa kwani kutokana na kasi ya mawasiliano dunia imekuwa kijiji na hivyo yanayotokea katika mataifa mengine yanaweza kutokea kwetu.
Usiku wa Aprili 14 kuamkia Aprili 15, 2014 ni siku ambayo watoto wa kike wapatao 276 katika Shule ya Sekondari ya Serikali  walitekwa na kikundi cha Boko Haram katika Mji wa Chibok Jimbo la Borno nchini Nigeria.
Kati ya wasichana 276 waliotekwa ni wasichana 57 tu waliofanikiwa kutoroka na tangu wakati huo mpaka sasa imepita zaidi ya miaka miwili mateka hao wameendelea kuwa mikononi mwa magaidi mbali na kelele za kimataifa bila kusahau kauli mbiu ya ‘‘Bring back our girls’’ kuwapo.
Ni kama ndoto lakini inaumiza kwamba inawezekana vipi watoto zaidi ya 200 watekwe ndani ya nchi halafu Serikali na jamii ya kimataifa ikiwamo Marekani iliyotuma wataalamu wa masuala ya utekaji na upelelezi vishindwe!
Shule nyingi za sekondari zenye kidato cha kwanza mpaka sita wanafunzi wengi huwa na miaka kati ya 15-18. Hapa unaweza kujiuliza katika umri huu wa kitoto, wanafunzi hao wameathirika kisaikolojia na kibaolojia kiasi gani?
Hivi juzi kituo cha luninga cha CNN kutoka Marekani kimeonyesha kuwa wasichana waliotekwa huko Nigeria bado ni hai wakiwa wenye afya nzuri na wangetamani kurudi nyumbani kwao, lakini nani mwenye uhakika kama mabinti hao hawajaingiliwa kimwili kwa nguvu?
Nani aielezee dunia kinaga ubaga kwamba mabinti hao kwa muda wa miaka miwili waliyotekwa hawakuwahi kufanyiwa vitendo dhalili kama kulawitiwa nikimaanisha kuingiliwa kimwili kinyume cha maumbile na kupigwa viboko wanapokosea?
Nani wa kuwafariji wazazi walioathirika kisaikolojia baada ya kuwapoteza wana wao ili waridhike kwa kuamini kuwa watoto wao wakiumwa njaa wanapatiwa chakula kwa wakati na wakiugua wanapatiwa matibabu kwa haraka?
Wakati tukio la kuteka mabinti wa shule likiwa limefanyika Nigeria pamekuwapo kushambuliwa taasisi za elimu maeneo mbalimbali duniani. Aprili 2, 2015 kikundi cha Al-Shabaab kilivamia Chuo Kikuu cha Garisa nchini Kenya na kuua wanafunzi wapatao 148 huku 79 wakiwa wamejeruhiwa.
JANUARI 21, 2016 kikundi cha Taliban kilivamia Chuo Kikuu cha Bacha Khan nchini Pakistan na kuua watu wapatao 22 huku wengine wengi wakibaki wamejeruhiwa. Hayo ni matukio machache kati ya mengi.
Mei 3, mwaka huu katika maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani yaliyofanyika kitaifa jijini Mwanza, Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Edda Sanga alisema kuwa kwa siku za karibuni watoto wa kike nchini wamekuwa wakikabiliwa na mikasa ya kulawitiwa, kubakwa na kuteswa.
Hayati Nelson Mandela aliwahi kusema: ‘‘Maji yakianza kuchemka ni ujinga kujifanya unazuia mvuke’’ Serikali itakapolifanyia mzaha suala la ulinzi wa watoto wa kike ijue ipo siku italaumiwa. Naamini jukumu la usalama wa raia na mali zao ni la Jeshi la Polisi.
Ulinzi na usalama ambavyo vimebeba dhima ya uhai wa binadamu ambao kimsingi huwezi kuununua dukani hata kama ungekuwa bilionea kama Donald Trump wa Marekani havina mbadala wake
‘‘Kama huwezi kujifunza mwenyewe kamwe hutaweza kujenga nyumba kwa sababu utatumia pesa zako kwa uamuzi wa kipumbavu’’ Hayo ni maneno aliwahi kusema Raia wa Marekani, Mjasiriamali, Mwekezaji na Mtunzi wa Vitabu, Daymond John.
Ni uvivu wa kufikiri endapo Serikali itasema haina uwezo wa kuajiri askari polisi wa kutosha tena wenye mafunzo mahiri na zana bora kutokana na ufinyu wa bajeti. Ni mara mia barabara na viwanja vya ndege vikachelewa kujengwa lakini mabinti wetu wakawa salama.
Ni mara elfu waheshimiwa wabunge, mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa, wakurugenzi na makatibu tawala wakalipwa mishahara kiduchu kama ya walimu wa shule za msingi, lakini shule zilizoko kwenye mazingira hatarishi zikapewa ulinzi wa uhakika.
Nasema mazingira hatarishi kwa maana ya kwamba zipo baadhi ya shule hapa nchini kijiografia zilipojengwa panatia shaka. Kwa mfano Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Bwiru pamoja na kujengwa mbali na mji bado imo ndani ya miti mingi huku ikiwa imepakana na Ziwa Victoria ambalo linaweza kuwa nyezo kwa wahalifu kama magaidi, maharamia na majambazi wa ndani na nje ya nchi.
Kwenye kitabu cha ‘‘Ckear World’’ ukurasa wa 80 kuna Methali na Zaburi ambapo methali mojawapo inasema : ‘‘Watu makini hufikiri kabla ya kutenda, lakini watu wapumbavu huonyesha ujinga wao.’’
Wabunge wanapotukanana mjengoni kama wendawazimu na kushindana kwa hoja dhaifu ili kujiongezea umaarufu wa kuendelea kuumega mkate wa walalahoi, huku viongozi wa Serikali wakiwa kwenye raha ya shibe, hawana budi kutambua kuna makundi maalumu kama watoto wa kike, walemavu wa ngozi na wanawake vikongwe wanaohitaji kulindwa usiku na mchana.