26.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali inaposhindwa kuwalinda wanafunzi wa kike!

wanafunzi wa kikeAPRIL 28, 2016 ni siku ambayo Shule ya Wasichana ya Bwiru iliyoko Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza ilifanya mahafali ya kuwaaga wanafunzi wa Kidato cha Sita baada ya safari ndefu ya masomo.

Akisoma risala  kwa mgeni rasmi,  Makamu Mkuu wa Shule, Mark Paul alisema  tangu kuanzishwa kwa shule hii mwaka 1952 mpaka sasa kuna mafanikio mengi yaliyopatikana kama vile ongezeko la wanafunzi na ufaulu wao.

Penye mafanikio hapakosi changamoto ndivyo ilivyo kwa Shule ya Wasichana ya Bwiru. Makamu Mkuu huyo  katika risala yake aliendelea kusema baada ya kuona usalama wa shule ni mdogo, uongozi wa  shule pamoja na bodi yake waliamua kuchukua hatua madhubuti.

Hatua  zilizochukuliwa  ili kuweka usalama  katika  eneo hilo  ni kuingia mkataba na kampuni ya ulinzi ya ‘Mara Security Company Ltd’ ambayo walinzi wake hulipwa kwa michango inayotokana na wazazi.

Kitendo cha uongozi wa shule kutafuta suluhisho la usalama kinastahili pongezi lakini swali la kujiuliza ni Je, hawa walinzi wa kampuni binafsi wanayo mafunzo ya kutosha ili kukabiliana na uhalifu uliokomaa kutokana na nguvu ya Sayansi na Teknolojia?

Inawezekana walinzi wakawa na mafunzo ya kutosha kwa maana ya kwamba pengine wamepitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) au baadhi yao ni  wastaafu wa vyombo vya ulinzi na  usalama kama vile JWTZ, Polisi, Magereza nakadhalika.  Lakini cha kujiuliza wanapatiwa  zana za kisasa  ili kuupiku uhalifu mamboleo?

Hatuombei mabaya yatokee katika Taifa letu lakini ikumbukwe Tanzania siyo kisiwa  kwani kutokana na kasi ya mawasiliano dunia  imekuwa kijiji  na hivyo yanayotokea katika mataifa mengine yanaweza kutokea  kwetu.

Usiku wa Aprili 14 kuamkia Aprili 15, 2014 ni siku ambayo watoto wa kike wapatao 276 katika Shule ya Sekondari ya Serikali  walitekwa na kikundi  cha Boko Haram  katika Mji wa Chibok Jimbo la Borno nchini Nigeria.

Kati ya wasichana 276 waliotekwa ni wasichana 57 tu waliofanikiwa kutoroka na tangu wakati huo mpaka sasa imepita zaidi ya miaka miwili mateka hao wameendelea kuwa mikononi mwa magaidi mbali  na kelele za kimataifa bila kusahau kauli mbiu ya  ‘‘Bring back our girls’’ kuwapo.

Ni kama ndoto lakini inaumiza kwamba inawezekana vipi watoto zaidi ya 200 watekwe ndani ya nchi halafu Serikali na jamii ya kimataifa ikiwamo Marekani iliyotuma wataalamu wa masuala ya utekaji na upelelezi vishindwe!

Shule nyingi za sekondari zenye  kidato cha kwanza mpaka sita  wanafunzi  wengi  huwa  na miaka kati ya 15-18. Hapa unaweza kujiuliza katika umri huu wa kitoto, wanafunzi  hao wameathirika kisaikolojia na kibaolojia kiasi gani?

Hivi juzi  kituo cha luninga cha CNN kutoka Marekani kimeonyesha kuwa wasichana waliotekwa huko Nigeria bado ni hai wakiwa wenye  afya nzuri na wangetamani kurudi nyumbani kwao,  lakini nani mwenye uhakika kama mabinti hao  hawajaingiliwa kimwili kwa nguvu?

Nani aielezee dunia kinaga ubaga kwamba mabinti hao kwa muda wa miaka miwili waliyotekwa hawakuwahi kufanyiwa vitendo dhalili kama kulawitiwa nikimaanisha kuingiliwa kimwili kinyume cha maumbile na kupigwa viboko wanapokosea?

Nani wa kuwafariji wazazi walioathirika kisaikolojia baada ya kuwapoteza wana wao ili waridhike  kwa kuamini  kuwa watoto wao wakiumwa njaa wanapatiwa chakula kwa wakati na wakiugua wanapatiwa matibabu kwa haraka?

Wakati tukio la kuteka mabinti wa shule  likiwa limefanyika Nigeria pamekuwapo kushambuliwa taasisi za elimu maeneo mbalimbali duniani. Aprili 2, 2015 kikundi cha  Al-Shabaab kilivamia Chuo Kikuu cha Garisa nchini Kenya na kuua wanafunzi wapatao 148 huku 79 wakiwa wamejeruhiwa.

JANUARI 21, 2016 kikundi cha  Taliban kilivamia Chuo Kikuu cha Bacha Khan  nchini  Pakistan na kuua watu wapatao 22 huku wengine  wengi wakibaki wamejeruhiwa. Hayo ni matukio machache kati ya mengi.

Mei 3, mwaka huu katika  maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani yaliyofanyika kitaifa jijini Mwanza, Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Edda Sanga alisema kuwa kwa siku za karibuni watoto wa kike nchini wamekuwa wakikabiliwa na mikasa ya kulawitiwa, kubakwa na kuteswa.

Hayati Nelson Mandela aliwahi kusema: ‘‘Maji yakianza kuchemka ni ujinga kujifanya unazuia mvuke’’  Serikali  itakapolifanyia mzaha  suala la ulinzi wa  watoto wa kike ijue ipo siku italaumiwa.  Naamini  jukumu la usalama wa raia na mali zao ni la Jeshi la Polisi.

Ulinzi na usalama ambavyo vimebeba dhima ya uhai wa binadamu ambao kimsingi huwezi kuununua dukani hata kama ungekuwa bilionea kama Donald Trump wa Marekani havina mbadala wake

‘‘Kama huwezi kujifunza mwenyewe kamwe hutaweza kujenga nyumba kwa sababu utatumia pesa zako kwa  uamuzi wa kipumbavu’’ Hayo ni maneno aliwahi kusema Raia wa Marekani, Mjasiriamali, Mwekezaji na  Mtunzi wa Vitabu, Daymond John.

Ni  uvivu wa kufikiri endapo Serikali itasema haina uwezo wa kuajiri askari polisi wa kutosha tena wenye mafunzo mahiri na zana bora  kutokana na ufinyu wa bajeti. Ni mara mia barabara na viwanja vya ndege vikachelewa kujengwa  lakini mabinti wetu wakawa salama.

Ni mara elfu waheshimiwa wabunge, mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa, wakurugenzi na makatibu tawala wakalipwa mishahara kiduchu  kama ya  walimu wa shule za msingi, lakini  shule zilizoko kwenye mazingira hatarishi zikapewa ulinzi wa uhakika.

Nasema mazingira hatarishi kwa maana ya kwamba zipo baadhi ya  shule hapa nchini kijiografia zilipojengwa panatia shaka. Kwa mfano Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Bwiru pamoja na kujengwa  mbali na mji bado  imo ndani ya  miti mingi  huku ikiwa imepakana na  Ziwa Victoria ambalo linaweza kuwa nyezo kwa wahalifu kama magaidi, maharamia na majambazi wa ndani na nje ya nchi.

Kwenye kitabu cha ‘‘Ckear World’’ ukurasa wa 80 kuna Methali na Zaburi ambapo methali mojawapo inasema : ‘‘Watu makini hufikiri kabla ya kutenda, lakini watu wapumbavu huonyesha ujinga wao.’’

Wabunge wanapotukanana mjengoni  kama wendawazimu na  kushindana kwa hoja dhaifu ili  kujiongezea umaarufu wa kuendelea  kuumega mkate wa walalahoi, huku viongozi wa Serikali wakiwa kwenye raha  ya shibe,  hawana budi kutambua  kuna makundi maalumu kama watoto wa kike, walemavu wa ngozi na wanawake vikongwe wanaohitaji kulindwa usiku na mchana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles