30.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Ushindi wa Trump unatufundisha nini?

Donald TrumpWAGOMBEA wawili waliokuwa wamesalia kwenye kinyang’anyiro cha kutafuta mgombea urais kwa Chama cha Republican, Seneta Ted Cruz na Gavana wa Jimbo la Ohio, John Kasich, wamejitoa.  Hii inamaanisha kwamba mfanyabiashara mwenye makeke, Donald Trump, ndiye aliyesalia na hakuna tena njia ya kumuondoa asiwe mgombea Urais wa Marekani kwa tiketi ya chama chake.

Niliwahi kuandika katika safu hii, kwamba nilikuwa nasubiri kwa hamu kuona namna ‘wazee’ wa Republican watakavyomkata Donald Trump.  Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kwa jinsi mfanyabiashara huyo alivyo, pamoja na kauli zake tata, inawezekana kabisa asifae kuwa Rais wa Marekani.  Hata hivyo, kura za maoni zimesema tofauti.

Kwa kifupi, Donald Trump ameandika historia. Alipokuwa akianza harakati zake za kutaka kuteuliwa na chama chake kuwa mgombea urais, wengi walimdhihaki.  Huenda  dhihaka hizi zilitokana na Trump mwenyewe kuwa na dhihaka dhidi ya makundi mbalimbali ya watu.

 

Alishawahi kuwadhihaki Wamarekani wenye asili ya Mexico, akidai kwamba ni wahalifu.  Aliwadhihaki pia Wamarekani wenye asili ya Afrika kwa kuwaita wavivu.  Aliwadhihaki pia Waislamu kwa kudai kwamba ndio wanaosababisha ugaidi.  Na alienda hata nje ya mipaka ya nchi yake, kwa kuwadhihaki viongozi wa Afrika na kudai kwamba atakapokuwa Rais, atawafunga Yoweri Museveni wa Uganda na Robert Mugabe wa Zimbabwe.

Trump ni mtu ambaye amekwisha kuzungumza mambo mengi sana wakati wa kampeni zake ndani ya chama cha Republican, na ilifika hatua hata watu wakamuita mbaguzi wa rangi kutokana na kauli zake tata.  Hata maswahiba wa Marekani – Uingereza – walianza kupata wasiwasi juu ya kauli za Trump, kufikia hatua ya mjadala kuanza endapo mfanyabiashara huyo anastahili kuruhusiwa kuingia katika ardhi ya Uingereza.

Ilifika hatua hata wazee wa chama cha Republican wenyewe walikuwa wakisema kwamba Trump hafai kuwa mpeperusha bendera yao kwenye uchaguzi wa Urais wa Marekani unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.  Walikuwa na tumaini kwa Marco Rubio, lakini baada ya kushindwa kupata ushindi kwenye majimbo aliamua kujitoa.  Hilo lilitokea pia kwa Seneta, Ted Cruz ambaye naye alijaribu kubaki kwenye kinyang’anyiro  hicho, lakini ushindi wa Trump kwenye majimbo mengi zaidi wakati wa kura ya maoni, ulimfanya naye ajitoe wiki iliyopita.

Demokrasia ni kitu cha ajabu sana.  Na pengine hili linatupa funzo sisi Waafrika, hususan Watanzania, kwamba mwisho wa siku, demokrasia inatakiwa kuwa kile ambacho watu wengi wanakitaka na si tu lazima yawe mapenzi ya kundi fulani la watu, ama mapenzi ya mtu mmoja, au mapenzi ya chama.  Mwisho wa siku, anayekuwa Rais anatakiwa kuwa Rais wa watu wote.  Huenda wazee wa Republican wanalifahamu hilo vizuri, na ndio maana kwa sasa wamebaki wanashangaa shangaa, hawajui la kufanya.

Ushindi wa Donald Trump ndani ya chama chake cha Republican unanikumbusha siasa zetu tulizonazo sisi wenyewe.  Mwaka 1995, Jakaya Mrisho Kikwete ndiye aliyekuwa kipenzi cha wengi.  Bado sijaelewa kwanini watu walimpenda.  Hakuwa na kauli kama za Trump, wala hakuwa mzungumzaji sana.  Pengine kupendwa huko kulitokana na haiba aliyokuwa nayo, ama pengine kilichokuwa kikisemwa kuwa ‘mvuto’ aliokuwa nayo.

Sisi hatuna utaratibu wa kuwa na kura za maoni za Urais kijimbo kama ilivyo kwa wenzetu wa Marekani.  Lakini ni ukweli usiopingika kwamba endapo kura hizo zingekuwapo mwaka 1995, basi Jakaya Kikwete angeshinda bila matatizo yoyote na kuwa mgombea wa kiti cha Urais kupitia CCM.  Hata ndani ya chama chake, alishinda, lakini kura ikabidi zipigwe tena kutokana na ‘ushauri’ wa Mwalimu Julius Nyerere, ili Benjamin William Mkapa apitishwe kuwa mgombea.  Sina hakika kama Republican bado wana nafasi kama hiyo kwa sasa.

Mwaka 2015, Edward Ngoyai Lowassa ndiye aliyekuwa kipenzi cha wengi.  Watu walimuunga mkono hadharani na ilifika hata hatua kwamba baadhi ya wakuu wa mikoa wakaenda kumwona ili kuonyesha kumuunga mkono kuwa mgombea Urais kwa tiketi ya CCM.  Hata wale viongozi wa chama na Serikali waliokuwa kwenye jukwaa kuu siku alipotangaza kuchukua fomu jijini Arusha, walithibitisha kwamba nguvu yake ya kupendwa ilikuwa ni kubwa mno kuliko mwanachama mwingine yeyote ndani ya CCM.

Si hivyo tu.  Alipopita mkoa kwa mkoa kutafuta sahihi za wanachama kwa ajili ya kumdhamini kuwa mgombea wao, hakupata shida hata kidogo.  Wakati wagombea wengine walipata wakati mgumu sana kupata wadhamini, kwa Edward Lowassa lilikuwa ni suala la wadhamini kumtafuta yeye, kuona ufahari wa kuweka sahihi zao pale ili yeye ndiye awe chaguo la chama.

Hata hivyo, ‘wazee’ wa chama walikuwa na mipango mingine.  Licha ya sahihi zote, licha ya burudani zote za jijini Arusha, licha ya kelele zote za mashabiki wake, licha ya kususa kote kwa wafuasi wake…Chama Cha Mapinduzi kilikata jina la Edward Lowassa, tena mapema kabisa asubuhi.

Kwa chama, demokrasia haikumaanisha kile ambacho walio wengi wanakitaka.  Kwa chama, demokrasia haikumaanisha kwamba ukipata wadhamini wengi zaidi basi wewe ndiye utakayekuwa mwakilishi wa chama kwenye uchaguzi mkuu.  Kwa chama, demokrasia ilimaanisha kwamba mgombea wa kiti cha Urais lazima awe mtu waliyemuita wao mwadilifu, mchapakazi na mfuatiliaji.  Chama kilikuwa radhi kukata jina la Lowassa na kumpitisha John Pombe Magufuli ambaye wala hakujisumbua kutafuta wadhamini wengi kuliko idadi iliyotakiwa.

Donald Trump angelikuwa raia wa Tanzania, wala asingefikiriwa kuwa mgombea wa kiti cha Urais.  Hata kama angependwa namna gani kutokana na kusema ukweli kwa njia tata, wala asingepitishwa.  Hata kama angekusanya sahihi za wadhamini milioni moja, wala asingefikiriwa. Hata chama chake cha Republican wanalitambua hilo, lakini hawakuweza kujifunza kutoka kwa chama kama CCM, kwani wanaogopa kupindisha ‘demokrasia’ ambayo kwayo, wamekuwa wakiwanyooshea vidole nchi zingine, hususani hizi zetu za Afrika.

Binafsi, bado sijafahamu kama demokrasia iliyoonyeshwa na Marekani ni jambo jema ama la.  Ninachokifahamu mimi ni kwamba Urais wa nchi ni zaidi sana ya mtu mmoja kusimama jukwaani na kutoa kauli tata ambazo zinaleta hisia mbaya miongoni mwa wale anaotarajia kuwaongoza.  Ninachokijua pia ni kwamba chama cha siasa lazima kiangalie mtu anayefaa kuwa mwakilishi wake kwenye kinyang’anyiro cha kugombea urais wa nchi, kwani kama Mwalimu Nyerere alivyowahi kusema juu ya watu kumpenda mgombea fulani ambaye huenda hana sifa: “kama ni ni mzuri, nenda kanywe naye chai.”

Sina uhakika kama tunatakiwa kujifunza kutoka kwenye siasa hizi za Marekani.  Bado natafakari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles