WAKATI dunia ikiadhimisha siku ya Uhuru wa Habari duniani jana, Bazara la Wazee la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) limesema uhuru wa habari na upatikanaji wa taarifa nchini unapitia wakati mgumu kuliko kipindi cha ukoloni.
Siku ya Uhuru wa Habari Duniani huadhimishwa Mei 3 kila mwaka kwa madhumuni ya kujikumbusha misingi muhimu na kutathmini mwenendo wa uhuru wa habari, kuutetea na kuulinda dhidi ya vitisho na mashambulio na kuwakumbuka waandishi wa habari waliokufa wakati wakitimiza majukumu yao.
Akizungumza Dar es Salaam jana kwa niaba ya wazee, Katibu Mkuu wa Baraza la Wazee wa Chadema, Roderick Lutembeka, alisema hujuma, vitisho, vipigo, mauaji na mashambulio dhidi ya haki ya kupata taarifa ni miongoni mwa viashiria vya kutoweka kwa uhuru wa habari nchini.
“Watanzania wanaadhimisha siku hii wakiwa katika sintofahamu kwa sababu uhuru wa habari na upatikanaji wa taarifa kwa ujumla unapitia wakati mgumu kuliko hata ilivyokuwa wakati wa ukoloni au enzi za utawala wa udikteta,” alisema Lutembeka.
Alisema watawala wana hofu ya kuhojiwa na wananchi, wengine hawapo tayari kukubali fikra mbadala na mazingira ya aina hiyo ni hatari kwa ustawi wa taifa.
“Sheria zinazominya uhuru wa habari na kukandamiza upatikanaji wa taarifa sharti zifanyiwe marekebisho.
“Zipo sheria mbovu kama vile sheria ya magazeti, sheria ya takwimu na sheria ya makosa ya mitandao ambazo zote zinaminya uhuru na haki ya kupata taarifa,” alisema Lutembeka.
Wazee hao walionya kuzuiwa kwa vyombo vya habari kurusha matangazo ya bunge moja kwa moja (live) na kusema hivyo ni viashiria vya taifa kurudi nyuma kuliko hata zama za ukoloni.