22.9 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

Waliobomolewa nyumba  Kibamba walala nje

MAULI MUYENJWA NA FLORIAN MASINDE, DAR ES SALAAM

WAKAZI wa eneo la Mloganzila, Kibamba katika Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam wameanza kulala nje kutokana na ubomoaji wa nyumba zao unaoendelea.

MTANZANIA jana ilishuhudia wananchi hao wakiwa maeneo hayo wengi wakiwa wameanza kulala nje kwa siku ya pili.

Wananchi hao wanawalalamikia viongozi wa serikali za mitaa kwa kushirikiana na matapeli na kuwadhulumu fedha zao kwa kuwauzia viwanja vyenye migogoro.

Mmoja wa waathirika wa ubomoaji huo, Elisha Isha alisema wanaiomba serikali iwapatie msaada wa kibinadamu kikiwamo chakula na mahema kwa   kuwa hawana mahali popote pa kwenda wakati huu.

“Vyakula vyote vimeharibika hatuendi kazini, watoto shuleni hawaendi na  mpaka sasa hakuna msaada wowote tulionao na hatujui mahali pa kwenda.

“Viongozi waliokuwapo awali walijua matatizo haya lakini hawakutwambia na sasa hawaonekani wameingia mitini,” alisema Isha.

Naye Diwani wa Kata ya Kwembe, Dweza Kolimba (Chadema) alisema amesikitishwa na hali hiyo ya wananchi hao kudhalilika kiasi hicho wakati tayari walikwisha kujipatia makazi.

Alisema mpaka sasa hakuna msaada wowote walioupata na kitengo cha maafa hakijafanya lolote hata   kufika maeneo hayo.

“Tulichofanya ni kuwagundua wakazi walioathirika lakini makosa yalifanywa na viongozi wa kwanza ambao walijua matatizo ya maeneo haya lakini kwa kuwa walikuwa wanapata asilimia 10 walitamani fedha na kuacha utu wa mtu na mwenye eneo anataka eneo lake na watu wanavunjiwa,” alisema Kolimba.

Mmiliki wa eneo hilo, Henry Kashangaki alisema   serikali ndiyo ya kulaumiwa kwa vile ilikuwa inajua   eneo hilo ni lake lakini ilitoa vibali kupitia serikali za mitaa na watu wakaanza kuuziana na kutapeli wananchi wasiokuwa na hatia.

Nyumba zaidi ya 400 zinatakiwa kuvunjwa katika eneo la ekari 33 mali ya  Kashangaki. Eneo hilo lilivamiwa na watu 10 ambao baadaye waliwauzia wengine zaidi ya 600 ambao ndiyo wameathiriwa na ubomoaji huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles