29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Sekta ya viwanda taabani, deni la Taifa lapaa

mpangoNa Bakari Kimwanga, Dodoma

WAKATI Serikali ya awamu ya tano, ikieleza mikakati yake ikiwemo kuijenga Tanzania ya viwanda, hali katika sekta hiyo ipo taabani kutokana na viwanda 30, vilivyobinafsishwa kufanya kazi kwa hasara.

Kutokana na hali hiyo, Serikali imesema imedhamiria kuondoa mambo yanayoonekana ni mzigo kwa Taifa hususan wananchi wanyonge.

Hayo yalisemwa bungeni jana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alipowasilisha Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa wa miaka mitano kwa mwaka 2016/17-2020/21.

Alisema tangu kuanza kwa ubinafsishaji wa mashirika ya umma mwaka 1992, viwanda 106 vilibinafsishwa kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Alisema kati ya viwanda 34, vinaendeshwa kwa ufanisi na kuongeza ajira na mapato ya Serikali, huku 33 vikiendeshwa kwa hasara na viwanda 39 vya bidhaa mbalimbali kama ngozi, korosho, zana za kilimo, sabuni na mafuta vikifungwa kabisa kutokana na kukosekana kwa mitaji na utendaji.

Licha ya hali hiyo, Dk. Mpango alisema hatua ya uchambuzi kwa lengo la kubainisha mfumo wa kuvifufua viwanda vilivyobinafsishwa zikifanyika katika mpango wa mwaka 2016/17.

“Mchango wa sekta ya viwanda katika pato la Taifa, ulikuwa wa wastani wa asilimia saba, ukiongezeka kutoka asilimia 6.6 mwaka 2005 hadi asilimia 7.3 mwaka 2014, ongezeko hili linachangiwa na uwekezaji mpya kuimarika upatikanaji wa nishati ya umeme na kuinua matumizi ya uwezo uliopo.

“Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2013, Tanzania ina viwanda 50,656 ambapo viwanda vya kati na vikubwa ni 1,769 sawa na asilimia 3.5 na viwanda vidogo 48,887 sawa na asilimia 96.5.,” alisema Dk. Mpango

Alisema katika mpango wa maendeleo wa awamu ya pili, msisitizo si jambo jipya kwani tangu uhuru maendeleo ya viwanda yamekuwa yakipewa kipaumbele, lakini utekelezaji wake umekuwa ukitumia mikakati inayotofautiana kwa kuzingatia mfumo wa sera na usimamizi wa uchumi.

“Kati ya viwanda vilivyobinafsishwa, viwanda 34 vinaendeshwa kwa ufanisi na 33 vinaendeshwa kwa hasara na hatua za uchambuzi kwa lengo la kubainisha mfumo wa kuvifufua viwanda vilivyobinafsishwa zinafanyika mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa mpango 2016/17,” alisema.

Alisema katika utekezaji wa mpango wa awamu ya pili uzoefu wa nchi mbalimbali umetumika kubainisha mwelekeo wa ujenzi wa viwanda nchini.

KAMATI

Akiwasilisha taarifa ya kamati, Mwenyeikiti wa Kamati ya Bajeti, Hawa Ghasia, alisema deni la Taifa limeendelea kukua na kufikia Sh trilioni 36.39 hadi kufikia Desemba 2015, ikiwa ni tofauti na ililivyokuwa Sh trilioni 14.4 kwa mwaka 2011/12.

“Kwa sasa deni limefikia takribani asilimia 44.9 ya pato la Taifa limeendelea kukua kutokana na Serikali kuendelea kukopa kwa ajili ya kugharimia nakisi ya bajeti,” alisema.

Akizungumzia kuhusu thamani ya shilingi, alisema mwenendo wake umeendelea kuwa si wakuridhisha.

“Thamani ya shilingi ilishuka kutoka Sh 1,401.79 mwaka 2010 hadi Sh 2,180 Desemba 2015. Kamati inaona suluhisho la kudumu la kutengemaa kwa thamani ya shilingi ni kupungua kwa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho wa mali nchi za nje. Hii itawezekana tu endapo tutapunguza mauzo yetu nje ya nchi yaoangezeka na kuziba pengo hilo,” alisema.

Alisema katika kipindi cha utekelezaji wa mpango wa kwanza, sekta ya viwanda ilikuwa kwa wastani wa asilimia 6.6 chini ya lengo la kufikia wastani wa asilimia 11 mwaka 2015.

Kambi ya Upinzani yaonya

Akiwasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani Bungeni, msemaji wa kambi hiyo, David Silinde, alisema hali ya deni la Taifa inatisha na nchi inapoelekea kama hazitachukuliwa hatua madhubuti la wenye jukumu la kuisimamia Serikali ambao ni Bunge, nchi inaweza kufilisika kama ilivyotokea kwa nchi ya Ugiriki.

“Katika miaka ya 80 Tanzania ilikopa dola za Marekani milioni 49 kutoka Brazil ili kugharimia mradi wa ujenzi wa barabara inayounganisha Morogoro na Dodoma. Deni hilo halikulipwa ilipofikia mwaka 2010 liliongezeka hadi kufikia dola za Marekani milioni 240,” alisema.

Akichangia mpango huo, Mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka (CUF), aliibua mjadala mzito baada ya kudai jimbo lake halina maendeleo kwa miaka mingi, hali inayomfanya atamani jimbo lake liwe nchi nyingine.

Kutokana na kauli ya mbunge huyo, alisimama Naibu Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Dk. Hamis Kigwangalla, ambaye alimpa taarifa na kumwambia hatua ya kusema angekuwa na uwezo jimbo lake wangejiunga na nchi nyingine ni kukosa uzalendo kwa wapiga kura wake waliomchagua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles