Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Saba wa Kimataifa wa Jumuiya ya Mamlaka za Usimamizi wa Usafiri Majini Barani Afrika. Mkutano huo utaanza Novemba 29 hadi Desemba 1, 2024, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limepewa jukumu la kuandaa tukio hili la kimataifa, ambalo linalenga kujadili masuala muhimu ya usalama, maendeleo, na udhibiti wa usafiri majini barani Afrika.
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, akizungumza Dar es Salaam Novemba 25, 2024, amesema mkutano huo utatoa fursa ya kujadili teknolojia na ubunifu katika sekta ya usafiri majini, huku kipaumbele kikiwa ni kuboresha usalama, mazingira, na kushirikiana kwa maendeleo ya uchumi wa buluu.
“Mkutano huu ni jukwaa muhimu la wadau kujadili teknolojia za kisasa, kuimarisha usalama wa usafiri majini, na kuingia makubaliano ya kibiashara. Pia, ni nafasi ya kukuza mitandao na ushirikiano wa kimataifa,” alisema Profesa Mbarawa.
Mkutano huo wa kihistoria utafunguliwa rasmi na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati wa Tanzania, Dk. Doto Biteko. Pia, utahudhuriwa na Katibu Mkuu wa Shirika la Bahari Duniani (IMO), Antonio Dominguez, pamoja na wataalam wa sekta ya usafiri majini na viongozi kutoka nchi 50 za Afrika zenye bahari, maziwa, na mito.
Profesa Mbarawa alisisitiza kuwa ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo ni sehemu ya jitihada za kutekeleza Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu.
“Kama nchi, tunapigia mstari matumizi endelevu ya rasilimali za bahari na maziwa ili kukuza uchumi wa Taifa na kuleta maendeleo kwa wananchi,” aliongeza.
Kauli mbiu ya mkutano huu ni “Kuimarisha mustakabali wa sekta ya usafiri majini barani Afrika: Ushirikiano katika Teknolojia na Ubunifu ili kupunguza hewa ukaa, kuimarisha usalama, na mazingira ya sekta ya usafiri majini kwa mustakabali endelevu.”
Profesa Mbarawa alitoa wito kwa wadau wa sekta ya usafiri majini, wakiwemo wasafirishaji, wamiliki wa vyombo vya majini, na viongozi wa mashirika ya kimataifa, kushiriki kwa wingi ili kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha usafiri wa majini Tanzania na Afrika kwa ujumla.