25.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 30, 2024

Contact us: [email protected]

‘Utashi wa kisiasa kikwazo mabadiliko sheria ya ndoa’

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Mabadiliko ya Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 hayajatekelezwa kwa sababu mbalimbali ikiwamo kukosekana kwa utashi wa kisiasa kutoka kwa baadhi ya viongozi pamoja na kuwapo kwa mila na desturi potofu kwenye jamii, imeelezwa.

Mwaka 2016 Mwanaharakati, Rebecca Gyumi alishinda kesi aliyofungua mahakamani kupinga Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 na mwaka 2019 Serikali ilipewa muda wa mwaka mmoja hadi mwaka 2020 kufanyia marekebisho sheria hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Koshuma Mtengeti, akizungumza kuhusu sheria ya ndoa na utekelezwaji wa programu ya kurudi shule kwa watoto waliokatisha masomo.

Aidha mwaka 2021 ulipelekwa muswada bungeni kuweka umri wa kuolewa kuwa miaka 18 na baadaye Serikali ilielekezwa na Bunge kurudi kwa umma kupata maoni lakini mpaka sasa bado mchakato huo umekwama.

Wadau mbalimbali kutoka mashirika yasiyokuwa ya kiserikali (SCO) wanapaza sauti zao wakihimiza Serikali kuharakisha mchakato wa mabadiliko ya sheria hiyo.

Wakizungumza Oktoba 28,2024 wakati wa mkutano ulioandaliwa kwa ushirikiano wa Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) na Chama cha Wanasheria Wanawake (TAWLA) kwa ufadhili wa Equality Now wamesema kunahitajika marekebisho ya sheria ya ndoa hasa vifungu vya 13 na 17 ambavyo vinaruhusu mtoto wa kike kuolewa chini ya umri wa miaka 18.

“Tangu mahakama ilipotoa maagizo kwa Bunge na Serikali kubadilisha sheria hiyo bado imekwama, Serikali ina jukumu kubwa la kutengeneza mazingira salama kuhakikisha watoto wote wanapata haki zao na kuwe na sheria kali wazuiwe wasiolewe,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa CDF, Koshuma Mtengeti.

Amesema pia kumekuwa na unyanyapaa kwa mabinti ambao tayari wameshapata watoto kurudi shuleni na kwamba bado hakuna mazingira stahiki kama vile walimu kujiandaa na kuwapo kwa mitazamo hasi ya kijamii.

“Kuna tatizo pia la ukatili wa kingono, Asilimia 33 ya watoto wa kike wanapitia ukatili wa kingono kulinganisha na asilimia 17 ya watoto wa kiume, kama wadau tuhakikisha kwamba matukio haya yanatolewa taarifa katika vituo vya polisi na hatua stahiki zinachukuliwa, kesi zinafika mahakamani ili watoto waweze kupata haki stahiki,” amesema Mtengeti.

Mkurugenzi Mtendaji wa TAWLA na Mwenyekiti wa Kupinga Ndoa za Utotoni Tanzania, Tike Mwambipile, amependekeza sera, mifumo na sheria zizuie ndoa za utotoni ili kuwawezesha watoto wa kike kupata haki za msingi na kutimiza ndoto zao.

“Tunajaribu kupaza sauti kwenye jamii itambue madhara ya ndoa za utotoni na mimba za utotoni kwa sababu ni makubwa sana hasa ya kiafya,” amesema Mwambipile.

Mkutano huo unachagiza majadiliano ya wazi katika kukabiliana na ukatili wa kijinsia na kingono katika mazingira ya shule ambapo mapendekezo yatakayokusanywa yanatarajiwa kuwasilishwa kwenye kamati na wizara mbalimbali za serikali.

Washiriki wengine katika mkutano huo ni Mtandao wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni Tanzania (TECMN), TEN/MET na The SRHR Coalition.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles