31.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 22, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania yapiga hatua uchumi wa Kidigitali, yasaini makubaliano na kampuni ya CECIS ya China

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeingia makubaliano muhimu na Kampuni ya Huduma za Mawasiliano ya Kielektroniki ya China (CECIS LTD) ambayo yanatarajiwa kuleta uwekezaji mkubwa na kutoa mafunzo kwa Watanzania.

Kupitia makubaliano hayo, zaidi ya makampuni 600 ya vifaa vya kompyuta yataweza kuwekeza nchini Tanzania, lengo likiwa ni kukuza ujuzi kwa vijana na kuifanya nchi kuwa kitovu cha utengenezaji wa kompyuta kimataifa.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dk. Nkundwe Moses Mwasaga.

Makubaliano hayo yamesainiwa, Oktoba 21, 2024, jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Abdulla, pamoja na Mwenyekiti wa Kampuni ya CECIS, Guo Zhaoping.

Hafla hiyo ilishuhudiwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Maryprisca Mahundi, ambaye alieleza kuwa makubaliano hayo ni hatua kubwa kwa Tanzania katika kujenga uchumi wa kidijitali.

“Makubaliano haya ni matokeo ya ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini China aliyoifanya hivi karibuni. Kampuni hii ni mabingwa wa masuala ya usalama wa mitandao, hivyo elimu waliyonayo itawafaidisha vijana wetu kujifunza. Tunahitaji wataalam wengi zaidi wa TEHAMA nchini,” alisema Naibu Waziri Mahundi.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mohammed Abdulla, aliongeza kuwa uwekezaji huu utatoa fursa kwa Watanzania kupata ujuzi mpya na ajira, hasa katika sekta ya TEHAMA. “Makubaliano haya yatasaidia vijana wetu kujifunza, kupata ajira, na kuongeza uwezo wa nchi katika sekta ya kompyuta na teknolojia ya kidijitali,” alisema Abdulla.

Mwenyekiti wa CECIS, Guo Zhaoping, ambaye pia ni Naibu Mkurugenzi wa Sayansi na Teknolojia katika kamati ya kampuni hiyo, alisema uwekezaji huu unazingatia misingi ya ushirikiano kati ya Tanzania na China.

“Lengo letu ni kuchochea maendeleo ya uchumi wa kidijitali na kuhakikisha kuwa tunakuza uhusiano wa kiuchumi baina ya nchi zetu. Kwa hapa Tanzania, tutafanya kazi kulingana na mahitaji ya soko la ndani,” alisema Zhaoping.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dk. Nkundwe Moses Mwasaga, alisema kuwa makubaliano haya pia yatawezesha kuvutia makampuni mengi zaidi ya teknolojia ya kielektroniki kuwekeza nchini. Aliongeza kuwa mwaka 2025 Tanzania itakuwa mwenyeji wa maonesho makubwa ya utengenezaji wa vifaa vya kompyuta barani Afrika, tukio litakaloimarisha nafasi ya Tanzania katika uwanja wa teknolojia.

Makubaliano haya ni hatua nyingine ya kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na China, na yanatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya TEHAMA, huku yakiongeza ajira na kuongeza ujuzi kwa Watanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles