28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 21, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania na Iran zasaini Hati 11 za Makubaliano ya kibiashara

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Serikali ya Tanzania na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimesaini hati 11 za makubaliano ya kibiashara, ambapo sita ni baina ya serikali na mitano ni ya sekta binafsi. Lengo la makubaliano hayo ni kukuza diplomasia na uchumi kati ya mataifa hayo mawili.

Akizungumza Oktoba 19, 2024, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, baada ya kushuhudia utiaji saini wa makubaliano hayo katika ufunguzi wa mkutano wa tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu (JPC), alisema ushirikiano huo ni fursa muhimu kwa Tanzania. Aliongeza kuwa makubaliano hayo yatasaidia kukuza uchumi na kuboresha sekta mbalimbali za nchi.

Balozi Kombo alieleza kuwa kufikiwa kwa makubaliano hayo ni matokeo ya jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kupanua uchumi wa Tanzania na kuimarisha uhusiano wa kimataifa.

“Niwashukuru Marais wa Tanzania na Iran kwa kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia, hususan katika maeneo ya biashara, uwekezaji, kilimo, nishati, ulinzi na usalama, na elimu,” alisema.

Aidha, Balozi Kombo aliwataka wafanyabiashara wa Tanzania, ikiwemo Chemba ya Biashara na Taasisi ya TanTrade, kuchangamkia fursa zinazotokana na makubaliano haya ili kuendelea kuimarisha uchumi wa nchi.

Maeneo mengine ambayo Tanzania na Iran yatashirikiana ni afya, sayansi na teknolojia, pamoja na utamaduni. Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo wa Iran, Golamreza Nouri Ghezelcheh, alisema kuwa ushirikiano huu utakuwa na manufaa makubwa kwa sekta ya kilimo, na utaboresha shughuli za kilimo kwa manufaa ya wananchi wa nchi zote mbili.

“Marais wa pande zote mbili wanasisitiza umuhimu wa kuendeleza uhusiano wa Afrika. Ni matumaini yangu kuwa hati hizi za ushirikiano zitaleta uhusiano mzuri zaidi katika awamu mpya,” alisema Nouri Ghezelcheh.

Hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo ilifanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, ikihusisha wizara za kisekta, taasisi za umma, na taasisi binafsi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles