32.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Wanafunzi Benjamin Mkapa wachangisha Sh 800,000 kuwasaidia wenzao wasiojiweza

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Zaidi ya Sh 855,000 zimechangwa na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa ili kusaidia wenzao wanaoishi kwenye mazingira magumu.

Fedha hizo zimechangwa kupitia unadishaji keki iliyoandaliwa wakati wa mahafali ya 24 ya Kidato cha Nne yaliyofanyika shuleni hapo Oktoba 4,2024.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Joseph Deo, amesema wanafunzi hao wamejiwekea utaratibu wa kuwasaidia wenzao wasiojiweza ili waweze kupata mahitaji muhimu kama vile sare, nauli na chakula.

“Kuna wanafunzi wana changamoto wengine wanashindwa kupata hata nauli ya kuja shule kwahiyo wanafunzi wenzao wamekuwa wakipita darasani na kuchangishana kuwasaidia. Pia wanatumia sherehe kama hizi za mahafali kutengeneza keki na kuinadisha…ukiwiwa kutoa sadaka ni afadhali uilete hapa shuleni isaidie watoto wasiojiweza,” amesema Mwalimu Deo.

Katika mahafali hayo mgeni rasmi, alikula keki kwa Sh 300,000, mwenyekiti wa bodi Sh 100,000, Mkuu wa shule Sh 100,000, Makamu Mkuu wa Shule, Sh 20,000, Makamu Mkuu wa Shule – Taaluma Sh 20,000, Mkuu wa Shule ya Sekondari Bangulo Sh 20,000, Mwenyekiti wa Wazazi wa Kidato cha Nne Sh 50,000 pamoja na wazazi, walezi na wageni mbalimbali waliohudhuria sherehe hiyo.

Shule hiyo inajivunia mafanikio kitaaluma ambapo imekuwa ikifaulisha wanafunzi kwa zaidi ya asilimia 90 kwenye mitihani ya taifa ya kidato cha nne na sita.

Takwimu za matokeo ya kidato cha nne zinaonyesha mwaka 2020 ufaulu ulikuwa asilimia 96, mwaka 2021 na 2022 (97) na mwaka 2023 (98) wakati kidato cha sita mwaka 2021 ilifaulisha kwa asilimia 100, 2022, 2023 na 2024 (99).

“Tunaamini kwa mwaka 2024 kutokana na jitihada za walimu na wanafunzi tutapunguza sifuri ikiwezekana kupata daraja la kwanza wanafunzi 150 au zaidi,” amesema Mwalimu Deo.

Hata hivyo amesema wana changamoto za uhaba wa kompyuta na projekta, uhaba wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia, uhaba wa vitabu vya kiada na ziada, uhaba wa walimu wa masomo ya akaunti, fizikia na hisabati, uchakavu wa miundombinu na kukosekana kwa eneo rafiki la kujisomea wanafunzi katika muda wa ziada wawapo shuleni (vimbweta).

Mkuu huyo wa shule amesema ujenzi wa ukumbi na maktaba uko katika hatua za mwisho wakati kwenye uwanja mkandarasi anaendelea na kazi ya kuweka nyasi bandia.

Amewataka wahitimu kuendelea kusoma hadi ngazi ya elimu ya juu na kuwaasa wazazi na walezi kutambua kuwa elimu ndio urithi bora wanaoweza kuwapatia watoto wao.

Katika mahafali hayo wanafunzi 273 walihitimu kidato cha nne.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles