29.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 25, 2024

Contact us: [email protected]

Zaidi ya Nchi 30 zathibitisha kushiriki Maonesho ya Kimataifa ya Utalii SITE 2024

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Zaidi ya nchi 30 zimethibitisha kushiriki Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Swahili International Tourism Expo (SITE), yanayotarajiwa kufanyika nchini Tanzania kuanzia Oktoba 11 hadi 13, 2024. Maonesho hayo yanafanyika kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji endelevu katika sekta ya utalii, huku kaulimbiu ya mwaka huu ikiwa “Tembelea Tanzania kwa Uwekezaji Endelevu na Utalii Usioharibu Mazingira.”

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mnamo Septemba 24, 2024, Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ephraim Mafuru, alisema maandalizi ya maonesho hayo, yatakayofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, yako katika hatua za mwisho. Alieleza kuwa maonesho haya ni fursa muhimu kwa Tanzania kufungua masoko mapya ya watalii kutoka nchi ambazo bado hazileti idadi kubwa ya watalii licha ya kuwa na idadi kubwa ya watu.

“Kuanzia Oktoba 11 hadi 13, tutakuwa na maonesho makubwa, yanayojulikana kama Swahili International Tourism Expo (SITE 2024), ambayo yatafanyika Mlimani City jijini Dar es Salaam. Lengo kuu ni kuimarisha mtandao wa kibiashara kwa wafanyabiashara wa sekta ya utalii,” alisema Mafuru.

Mafuru aliongeza kuwa maonesho hayo yanatoa fursa kwa watoa huduma na wanunuzi wa bidhaa za utalii kukutana na kubadilishana mawazo, huku zaidi ya washiriki 145 kutoka nchi 33 wakiwa tayari wamethibitisha ushiriki wao. Alitaja baadhi ya nchi ambazo zimethibitisha kushiriki kuwa ni pamoja na China, Denmark, Finland, Japan, Afrika Kusini, Kenya, Ethiopia, India, Oman, Uholanzi, Nigeria, Brazil, Ujerumani, Uganda, na Lesotho.

“Sekta yoyote ya biashara ina mnyororo wa thamani. Upande mmoja kuna watoa huduma na bidhaa, huku upande mwingine wakiwa ni wanunuzi. Maonesho haya yatakuwa kiungo muhimu katika kuimarisha mtandao huu,” aliongeza Mafuru.

Aidha, shughuli zitakazofanyika katika maonesho hayo ni pamoja na maonesho ya bidhaa na huduma mbalimbali zinazohusiana na utalii, ambapo wanunuzi watapata fursa ya kukutana na wazalishaji na watoa huduma ili kuimarisha mnyororo wa thamani. Pia, kutakuwepo na jukwaa la uwekezaji litakalotoa taarifa muhimu kwa wawekezaji wanaotaka kuingia katika sekta hiyo.

“Maonesho haya ni ya kipekee, kwani ni makubwa zaidi kwa Tanzania na hata kwa ukanda wa Afrika Mashariki,” alibainisha Mafuru.

Katika kuhakikisha washiriki wanapata taarifa sahihi za uwekezaji, Mafuru alieleza kuwa TTB itashirikiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kutoa taarifa za kina kuhusu mazingira ya uwekezaji, kodi, na masuala ya kifedha yanayohusu sekta ya utalii.

Maonesho haya yanatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kukuza sekta ya utalii nchini Tanzania, huku yakilenga kuhamasisha uwekezaji endelevu unaozingatia utunzaji wa mazingira na maendeleo ya kiuchumi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles